The House of Favourite Newspapers

Tigo Yajitosa Tena Kudhamini Kilimanjaro Marathon 2022

0
Meneja chapa wa Tigo, Anna Loya akizungumza kwenye uzinduzi huo.

 

 

MBIO za Kilimanjaro Premium Lager Marathon maarufu kama Kili marathon kwa mwaka 2022, zimezinduliwa Jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana huku Kampuni ya mawasiliano ya Tigo ikijitosa tena kudhamini mashindano hayo ya 20 tangu kuanzishwa kwake.

Picha baada ya uzinduzi huo.

 

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ambao ulifanyika katika Hoteli ya Four Points Sheraton, mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji Thomas Mihayo (mstaafu) aliwapongeza waandaaji na wadhamini ikiwemo Kampuni ya Tigo kwa ushirikiano wao ambao umeyafanya mashindano hayo kuwa maarufu ndani na nje ya nchi.

Mgeni rasmi Jaji mstaafu Thomas Mihayo (kulia) akimpongeza Meneja wa Chapa ya Tigo, Anna Loya kufuatia kampuni yake kuendelea kudhamini mbio hizo.

 

 

Alisema Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini kupitia utalii wa michezo (sports tourism) jambo ambalo alisema inaunga mkono juhudi za serikali katika utekelezaji wa sera za utalii na michezo.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (mwenye suti) akikata keki ya uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon pamoja na miaka 20 mbio hizo katika hafla iliyofanyika hoteli ya Four Point By Sheraton Jumatano iliyopita. Kulia ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro na kinywaji cha Grand Malt Irene Mutiganzi, Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo na Utamaduni, Yusuf Singo na Meneja chapa wa Tigo, Anna Loya. Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Februari 27 mwakani mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

 

 

“Nichukue fursa hii muhimu kuwapongeza wadhamini wote wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager, Tigo ambao ni wadhamini wa 21km (Half Marathon) na Grand Malt ambao ni wadhamini wa mbio za kujifurahisha za 5km”, alisema na kuongeza bila wadhamini hao mashindano hayo yasingefana.

Mgeni rasmi Jaji mstaafu Thomas Mihayo akizungumza kwenye hafla hiyo.

 

 

 

Alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa ya mbio hizo katika kukuza biashara zao sambamba na mapato yao kwa kuhakikisha wanatoa huduma bora na kuuza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu huku pia akiwataka washiriki wote pamoja na watazamaji kuhakikisha wanatumia msimu huo wa Kilimanjaro Marathon kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na vivutio vingine.

 

 

Naye Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Michezo na Utamaduni, Yusuf Singo alitoa wito kwa wandaaji wa mashindano mengine kama hayo kuhakikisha wanaiga mfano wa Kilimanjaro marathon ambao alisema wamekuwa wakizingatia mwongozo wa Shirikisho la Riadha Ulimwenguni (IAAF) na ule wa Chama cha Riadha nchini RT hatua ambazo zimewavutia wadhamini kutoka ndani na nje ya nchi kudhamini mbio hizo.

 

 

“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wake kwa waandaaji wa Mbio za Kilimanjaro Marathon ili kuhakikisha yanaendelea kuwa bora kutokana na umuhimu wake katika kuitangaza Tanzania na hata katika kukuza utalii kupitia michezo”, alisema.

 

 

Kwa upande wake, Meneja wa Chapa ya Tigo, Anna Loya, alisema Tigo imekuwa mstari wa mbele kudhamini mbio za Tigo Kili Half marathon kwa miaka saba sasa na kwamba kuwepo kwao kuendelea kuchangia kukuza vipaji  vya wanamichezo na sekta ya michezo kwa ujumla hapa nchini.

 

 

“Kwa miaka mingi tumeweza kutekeleza majukumu yetu kwa kudhamini mipango mbalimbali ndani ya jamii; kwa mwaka 2022, tunatarajia kufanya makubwa zaidi haswa kupitia mradi wetu wa kuboresha mazingira (Tigo Green) ambao tuliuzindua mwaka huu na ambao umelenga kupunguza athari zinazotokana na ongezeko la joto duniani”, alisema.

 

 

Aliwapongeza waratibu, waandaaji na wadhamini wa mbio za Kilimanjaro Marathon kwa kuweza kufanikisha hadi kufikia kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na ambayo amesema yamejenga umaarufu kwa kuwashirikisha wanariadhaa na wapenzi wa mbio hizo kutoka sehemu mbalimbali duniani.

 

 

“Nichukue fursa hii kuwahimiza wanaotarajia kushiriki mbio za Tigo Half Marathon kwa mwaka 2022, kujiandikisha mapema Tigo Pesa ili kuepuka usumbufu wa kung’ang’ania kufanya hivyo dakika za mwisho”, alishauri.

 

 

Kwa mujibu wa wandaaji wa mbio za Kilimanjaro premium lager marathon, ambazo zitafanyika Jumapili ya Februari 27, 2022, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), usajili utafunguliwa rasmi Oktoba 17, 2021 na unafanyika kwa njia ya mtandao (www.kilimanjaromarathon .com) au kwa njia ya Tigopesa kwa kubonyeza *149*20#.

 

 

Mbio hizi zimeandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Limited na kuratibiwa na  Kampuni ya Executive Solutions Limited.

Leave A Reply