The House of Favourite Newspapers

Tigo Yapokea Miche ya Miti 10,000 Kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu

0

KILIMANJARO: Aprili 21 2021 Kampuni inayoongoza katika mageuzi ya kidigitali Tanzania, Tigo imepokea miti jumla ya miti 10,000 kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kama utekelezaji wa ahadi iliyotolewa wakati wa uzinduzi wa mradi wa upandaji miti wa Tigo Green for Kili uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika jitihada za kutunza Mlima Kilimanjaro mradi wa Tigo Green for Kill umelenga kupanda jumla ya miti 28,000 katika eneo la mlima huo mkoani Kilimanjaro.

Katika mkakati huo ambao ulianza mwishoni mwa Februari mwaka huu umepata muitikio mkubwa kutoka kwa jamii na wadau mbalimbali ambao hadi sasa wameahidi kuchangia jumla ya miti 2,000.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya kukabidhi miche hiyo katika Shule ya Sekondari ya Boma iliyopo Hai mkoani Kilimanjaro, Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya alisema;

Tigo imejikita katika kutekeleza azma hii njema katika kutunza na kurejesha theluji ya Mlima Kilimanjaro ambayo imekuwa ikitoweka kwa miaka minne iliyopita kutokana na ongezeko la joto duniani, ukataji wa miti kiholela, uchomaji moto na shughuli za ukataji nguzo.

“Napenda kuwapongeza sana TFS kwa kuchangia miti 10,000 kwenye mradi huu.

Pia napenda kuwakumbusha wadau mbalimbali kuwa tunaendelea kupokea miti ambayo tunategemea kuipanda siku ya mazingira duniani ambayo itafanyika Juni 5 mwaka huu”.

Naye Meneja wa TFS Kanda ya Kaskazini, Edward Shilogile aliipongeza Tigo kwa kuanzisha mradi huo wa kutunza na kupanda miti katika eneo la Mlima Kilimanjaro.

“Kama wakala wa misitu tumepewa dhamana ya kutunza miti katika nchi yetu ya Tanzania na tulivutiwa sana na mradi huu wa Tigo Green for Kili na ndio maana tumeamua kuchangia miti 10,000 ili kufanikisha azma hii njema”.

“Tunatarajia kuona tunapanda miti katika eneo zima la mkoa wa Kilimanjaro na kwa kuanza kwa mradi huu wa Tigo, naamini tupo karibu sana kufikia malengi ili kuchangia kuifikia Kilimanjaro ya kijani kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

“Nitoe wito kwa wadau wengine wote kuunga mkono jitihada hizi kwa kuchangia miche ya miti ili Mlima Kilimanjaro uweze kurudi katika hali yake ya awali”, alisema Shilogile.

Leave A Reply