The House of Favourite Newspapers

Ubingwa Wa Simba Taifa Haijawai Kutokea

Wachezaji wa Simba wakifanya yao.

 

WACHEZAJI wawili wa zamani wa Simba, Juma Kaseja na Edward Christopher, jana Jumamosi waliharibu sherehe za ubingwa wa timu yao ya zamani baada ya kuiongoza Kagera Sugar kushinda bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Taifa katika moja ya mechi za kukamilisha ratiba.

 

Kaseja ambaye ndiye kipa pekee aliyeiongoza Simba kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2006, alizuia mashuti ya mastraika wa Emmanuel Okwi na John Bocco huku Edward akifunga bao pekee kwenye mchezo huo dakika za mwisho.

Kabla ya kuwakabidhi Simba kombe lao jana, Rais John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi alitema cheche huku akisisitiza kwamba yeye ni shabiki wa Taifa Stars lakini ataisapoti klabu yoyote ambayo itashinda kama Simba ilivyofanya msimu huu.

 

Simba ilipoteza mechi yake ya kwanza ya ligi, siku chache baada ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ambayo Yanga haina uhakika hata wa nafasi ya pili. Bao pekee la Kagera lilifungwa na Edward Christopher dakika ya 85 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Japhet Makarai.

 

Simba katika mchezo wa jana walionekana kushambulia lakini walipoteza nafasi nyingi za wazi huku Kagera ikitulia zaidi na ikihamasishwa na Kaseja ambaye aliwajaza upepo wenzake akiwaambia hakuna kupoteza mchezo na hilo lilidhihirika alipopangua penalti ya Okwi dakika za nyongeza.

 

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, kombe hilo linagharimu zaidi ya Sh.10milioni ambazo zinalifanya liwe ghali kuliko lile ambalo Yanga walikuwa wakilitwaa misimu mitatu mfululizo iliyopita. Rais Magufuli alilikabidhi kombe hilo mbele ya umati wa mashabiki wa Simba ambapo uwanja ulikuwa umatapakaa rangi nyekundu.

Simba imetwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa kwa miaka mitano, jambo ambalo limewapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambayo inaanza Desemba mwaka huu.


Huo ni ubingwa wa 19 wa Simba, ambapo kabla ya mchezo wa jana walikuwa hawajapoteza mchezo wowote tangu msimu huu uanze huku Yanga na Azam ambazo zilikuwa zikiibabaisha Simba misimu iliyopita zikiwa zimepoteza michezo minne kila moja kabla ya michezo ya jana.

Simba sasa imecheza michezo 29 ikiwa imefunga mabao 61 ambayo ni wazi hakuna timu ambayo itafanya hivyo msimu huu na imeruhusu mabao 14 pekee na kutoa sare nane ikiwa imepoteza mchezo mmoja na imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Majimaji.

 

Halina ubishi msimu huu kombinesheni ya Okwi na Bocco pamoja na Kichuya ndiyo imekuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo kutokana na ushirikiano ambayo walifanya vyema na wachezaji wenzao.

Simba ina uhakika wa Sh. 84 milioni baada ya kutwaa ubingwa huo wa Bara na zawadi kutoka kwa SportPesa Sh100milioni kwa kushinda kombe hilo.

RAIS ATAKA KOMBE

Rais Magufuli amezitaka klabu za Tanzania kuongeza umakini na kuondokana na aibu ya kuwa wasindikizaji kila mwaka kwenye michuano ya Afrika huku akiwasisitiza kuwekeza zaidi kwenye vijana.

“Tumepata uhuru tangu mwaka 1961, timu zetu hazifanyi vizuri sana, mimi sina timu, napenda michezo kwa ujumla. Nataka timu zangu zishinde, Yanga ikichukua kombe nitakuja.

“Sijawahi kuhudhuria uwanjani kwa sababu timu zetu ni kushindwa tu, timu zetu sasa tushinde. Ifike mahali sasa tushinde, tuweke mikakati ya ushindi na tuongeze umakini kwenye kila kila jambo.

“Tumechoka, tumechoka kufungwa. Simba mkawe wa kwanza kuleta Kombe la Afrika hapa Tanzania, nimewaheshimu nimekuja hapa uwanjani, huu usiwe mwisho wenu, mkabadilishe mchezo,”alisisitiza Magufuli ambaye wakati fulani alivyokuwa akitamka neno ‘sisi’ kwenye mazungumzo yake mashabiki wa Simba walishangilia kwa kutokana na tetesi zilizokuwa zimeenea kwamba yeye ni Simba damu.

 

“Kwa mpira wa leo hamwezi kuchukua Kombe la Afrika, ni lazima mbadilike, ni lazima mbadilike. Nimeambiwa Yanga wanashiriki michuano ya Shirikisho ni lazima washinde,”aliongeza Magufuli ambaye katika mchezo huo pia alikabidhi vikombe vya timu za taifa za Serengeti Boys na kikosi cha Wanawake kinachoishi kwenye mazingira magumu.

 

Hii inakuwa mara ya pili kwa Simba kufungwa mbele ya rais wa nchi, mwaka 1993, Simba walifungwa mabao 2-0 mbele ya rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Caf dhidi ya Stella Abdjan ya nchini Ivory Coast kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

Comments are closed.