The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi Umekwisha, Sasa Tufanye Kazi

0

Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

MUNGU ni mwema kwa sababu sehemu kubwa ya nchi hii tumefanya uchaguzi kwa amani, japokuwa sijapata taarifa za sehemu nyingine kutokana na ukubwa wa nchi yetu, hili ni jambo tulilokuwa tukiliombea.

Baada ya kusema hayo nianze kwa kuseme kwamba uchaguzi mkuu ambao ulikuwa ukituweka roho juu sasa umekwisha na tunawapa hongera wote walioshiriki kufanikisha kwa dhati uchaguzi huo na sasa tutakiane heri na kurejea katika shughuli nyingine za ujenzi wa taifa.

Kila Mtanzania sehemu alipo, angoje matokeo kwa amani huku akifikiria maendeleo yake na taifa hivyo afanye kazi ili kusukuma mbele taifa letu. Kuna mambo ya msingi takriban manne yamejitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Jumapili nimeyabaini mitaani nimeona ni vema kuyajadili, moja kubwa ni muendelezo wa hoja za kuwapo kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watu wenye upeo wa kufikiri, wamelijadili hili.

Kwa upande wangu, naamini kuwa hiyo ni hoja ya msingi na nashauri wahusika ikiwemo serikali itakayoundwa kuanza mchakato mapema ili kufikia safari ya kutungwa Katiba Mpya ya Tanzania itakayotokana na wananchi.
Ni busara zaidi kuanza mchakato huo uliokwamishwa mapema kabla ya kuanza kujitokeza kwa wimbi au shinikizo kutoka kwa umma.

Ni dhahiri kuwa Katiba ya Tanzania iliyopo imechoka kuendelea kuwekewa viraka na haiendani na uwanja mpya wa kidemokrasia ambao wote tunataka kuujenga na kwa ajili hiyo hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Katiba ambayo sehemu kubwa imekarabatiwa.

Lakini mbali na Katiba ya Tanzania, jambo lingine ambalo ni la msingi lililojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni suala la kuwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru. Ni dhahiri kuwa tume ya sasa ya uchaguzi imefanya kazi nzuri na kwa jumla imejitahidi sana katika mazingira haya tuliyonayo ambayo yamebadilika sana.

Vilio vya ucheleweshaji matokeo vitajitokeza kama ilivyokuwa mwaka 2010 na katika maeneo mengine ya nchi vilikuwa vikitishia kuzusha maafa, si mambo ya kuendelea kuishi nayo katika miaka ijayo.
Mazingira yamebadilika mno kiasi kwamba baadhi ya mambo, kama hodhi ya matokeo ya urais ama ubunge au udiwani, kubaki kuwa ya tume, wakati yanabandikwa vituoni na watu wanapelekeana kwa mtandao, ni mambo ya kuangalia upya.

Ni dhahiri pia kwamba sehemu fulani ya mamlaka ya tume imepoteza imani kutokana na kuonekana ikiegemea upande fulani kati ya vyama vilivyoshiriki uchaguzi inayoweza kuelezwa kuwa inajitokeza kwa baadhi ya watendaji wake kuwa wazito kutangaza matokeo yasiyokifurahisha chama kingine.

Lakini jambo lingine ni wito kwa wabunge wapya. Hawa tunawahimiza kutambua kuwa wamepewa dhamana kubwa na maisha yao ya ubunge ni mapya, yanayohitaji utulivu wa fikra na uwekezaji mkubwa wa maarifa.
Watambue kuwa vitendo na kauli zao zinapaswa kulenga kulijenga taifa na si vinginevyo, chonde punguzeni ushabiki wa kisiasa mkiwa bungeni na badala yake fanyeni kazi mkiweka itikadi zenu pembeni.
Penye ukweli muwe wazi kusema, kukosoa na kupongeza bila kusita.

Wananchi wanataka maendeleo siyo porojo za kisiasa maana watu wamechoka na umaskini.
Nawatakia kila la heri Watanzania wote, uchaguzi umekwisha Tanzania imebaki, sasa tumsubiri Rais Jakaya Kikwete amkabidhi nchi rais ajaye kwa amani na utulivu.

Leave A Reply