The House of Favourite Newspapers

Uchawi wa Shangazi Ulivyoteketeza Ukoo Wetu! -01

0

Mpenzi msomaji, kabla sijaanza kuwaletea mkasa mpya niliowaandalia napenda kuwapa pole wasomaji wangu wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na kifo cha dada Dorcas ambaye mkasa wake ulifikia tamati wiki iliyopita.

Miongoni mwa ninaowapa pole kwa kuguswa na kifo hicho ni dada Loveness mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye ni daktari aliyeshindwa kujizuia kulia nilipozungumza naye baada ya kunipigia simu, Irene wa Iringa, kaka Leonard wa Arusha na wengine wengi ambao nisingeweza kuwataja wote kwa majina.

Kwa kweli kifo cha Dorcas ambaye sehemu kubwa ya maisha yake ilikuwa ni mateso, kimewaliza wasomaji wengi.
Hata hivyo, watu wengi waliofuatilia mkasa wa Dorcas wamempongeza dada Stellah aliyeamua kuishi na msichana huyo mdogo ambaye hakuwahi kumuona baba yake mpaka naye alipokumbwa na mauti Aprili 5, mwaka huu. Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya mpendwa wetu Dorcas.

Wapo baadhi ya wasomaji walioomba namba ya simu ya dada Stellah kwa ajili ya mawasiliano, itabidi wawe wavumilivu kwani amesema kufuatia msiba huo bado kichwa chake hakijakaa sawa hivyo waendelee kuwasiliana nami, dada Stellah atakaponifahamisha niwape namba yake nitafanya hivyo mara moja bila kipingamizi chochote.

Baada ya kusema hayo, sasa narejea kwenye kisa hiki kipya kinachohusu uchawi wa shangazi mmoja katika ukoo fulani ambao kwa ombi la msimuliaji sitautaja kwa jina kutoka mkoani Morogoro.
Msimuliaji wa kisa hiki namtambulisha kwenu kwa jina la Rosemary siyo jina lake halisi, hajapenda kuweka wazi kila kitu kwa sababu maalum ambapo anaanza kusimulia kama ifuatavyo:-
“Mimi ni uzao wa ukoo wa kichifu uliopo mkoani Morogoro, kwa mujibu wa mama yangu ambaye tangu alipofariki dunia sasa ni miaka tisa imepita, babu yetu mzaa baba alikuwa chifu.

Mama alinieleza kwamba, enzi za uhai wa babu yetu alikuwa akiheshimiwa sana kwa sababu alikuwa akitegemewa kwa mambo mengi katika ukoo wetu na eneo aliloishi.

Kutokana kuwa chifu, mama aliniambia lilipotokea balaa kama ukame, maradhi, vifo na mambo mengine babu na machifu wenzake walikutana na kufanya mambo yao ya jadi na mambo kuwa sawa.
Alinieleza kuwa hata ulipofika msimu wa mavuno ambao ni mwezi wa 10 hadi wa 12 watu walisherehekea kwa kucheza ngoma.

Katika kunielezea huko historia ya babu yetu, alisema alikuwa na wake watano aliokuwa akiishi nao kwenye makazi yake.

Alisema babu alifanikiwa kuzaa na wake zake hao, mke mkubwa alizaa watoto kumi na mbili, aliyefuatia tisa, aliyefuatia sita, aliyefuatia watano, aliyefuatia watano miongoni mwao walikuwepo mapacha na wa mwisho alizaa watoto watatu.

Mke mkubwa alizaa watoto wa kiume watano na saba wa kike, wa pili alizaa wa kiume watano na wanne wa kike, wa tatu alizaa wa kiume watano na wa kike mmoja.

Mama aliongeza kuwa, mke wa nne alizaa watoto watano miongoni mwao walikuwepo mapacha wa kike na wa kiume watatu na wa mwisho alizaa watoto wakike pekee ambapo jumla yake alikuwa na watoto arobaini.
Aliongeza kuwa, licha ya babu kuwa na wake hao watano aliwapenda sana na wao walimheshimu na wote aliwagawia mashamba ya kulima na mifugo.

Mama alinieleza kuwa, babu yetu alikuwa akiogopwa na kuheshimiwa sana kufuatia kuwa na nguvu za kichifu na aliweza kuamuru mtu ambaye hakuwa akifuata maadili ahame katika eneo lake.
Miongoni mwa watoto aliokuwa akiwapenda sana alikuwa mtoto wake wa kwanza wa kiume ambaye aliitwa Samweli siyo jina lake halisi.

Kwa upande wa watoto wa kike alimpenda sana mtoto wa kike wa mwisho kwa mkewe mdogo, kwa kuwa msimuliaji hajapenda kuyaweka wazi majina yao nampa jina la Sabina, siyo halisi.
Mama aliniambia kwamba, licha ya machifu kuwa viongozi wa kimila kwenye maeneo yao, alisema babu alikuwa akisifika kwa uchawi aliourithi kutoka kwa babu yake enzi hizo.
Aliendelea kunieleza kuwa, kutokana na nguvu za kijadi alizokuwanazo babu, aliweza kuwaona watu wabaya waliokwenda kwenye makazi yake na kuwasambaratisha.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua. Maoni piga namba hapo juu.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply