The House of Favourite Newspapers

Uchunguzi wa Polisi Kulipuliwa Bomu Ofisi za IMMMA Advocates

0
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya.
 
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo limesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa watu wasiojulikana utambulisho wao na idadi yao walifika katika ofisi za Mawakili wa IMMMA Advocates wakiwa katika magari mawili na kujifanya ni maaskari na kuwarubuni walinzi na kuondoka nao katika gari mojawapo kabla ya kulipua jengo hilo.
 
Walinzi hao wanadaiwa kukutwa baadaye maeneo ya Kawe wakiwa hawajitambui.
 
Imedaiwa kuwa kundi lililobaki liliingia katika ofisi hizo na kuweka vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji, ambavyo vililipuka muda mfupi baada ya watu hao kuondoka eneo hilo na kusababisha uharibifu wa wa mali na jengo la ofisi hiyo pamoja na majengo ya jirani.
Ofisi hizo zilivyolipuliwa.
 
Jeshi hilo limesema kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu waliofanya tukio hilo na kujua dhamira yao ili wafikishwe katika vyombo vya sheria kwani wajibu wa jeshi la polisi ni kulinda raia na mali zao na kamwe haliwezi kuhujumu maisha ya watu na mali za wananchi
 
Aidha, jeshi hilo limewaomba waathirika wa tukio hilo na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi wa tukio hilo.

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

JESHI LA POLISI TANZANIA

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

28/08/2017

 

TUKIO LA MLIPUKO KWENYE OFISI ZA MAWAKILI WA IMMA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 26/8/2017 lilitoa taarifa ya awali ya tukio la mlipuko uliotokea katika ofisi za mawakili wa IMMA zilizopo katika eneo la Upanga jijini Dar Es Salaam.

 

Hivyo Jeshi la Polisi linapenda kuufahamisha umma kuwa  uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kwamba usiku wa kuamkia tarehe 26/8/2017 majira kati ya saa 7:00-8:00 watu wasiojulikana utambulisho wao na idadi kamili, walifika katika ofisi za mawakili wa kampuni ya IMMA (IMMA ADVOCATES) wakiwa na magari mawili wakijifanya ni askari na kuwarubuni kisha kuwachukua walinzi wa jengo hilo na kuondoka nao kwenye moja ya gari walilokwenda nalo,ambapo baadaye walinzi hao walikutwa maeneo ya Kawe wakiwa hawajitambui.

 

Aidha, kundi lililobaki liliingia ndani ya Ofisi hizo na kuweka milipuko iliyotengenezwa kienyeji ambayo baada ya watu hao kuondoka ililipuka na kusababisha uhalibifu wa mali na jengo la ofisi hiyo pamoja na majengo ya jirani.

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu hao waliofanya tukio hilo pamoja na kujua dhamira yao ili wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.

 

Aidha tunapenda ifahamike kuwa wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda maisha ya watu na mali zao  hivyo kamwe haliwezi kutumika kuhujumu maisha ya watu na mali za wananchi.

 

Tunaomba waathirika wa tukio hili na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi wa tukio. Vilevile, tunatoa rai kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia katika upelelezi waziwasilishe kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi.

 

B.M. KITALIKA- SACP

KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

 

 

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

 

Leave A Reply