The House of Favourite Newspapers

Ufaulu mzuri unahusisha kusoma, michezo na kulala

0

Wanafunzi wengi wanaweza wakatatizika na uhusiano uliopo kati ya masomo yao, michezo na kulala ambapo kisayansi imethibitika kuwa vyote hivyo vikifanywa kwa wakati maalum huongeza uwezo wa akili na hatimaye kufaulu vizuri kwa mwanafunzi husika kama atafanya kwa kiasi kinachotakiwa.

Kwa kawaida wengi hudhani kusoma muda mrefu zaidi na kulala muda mchache au pengine kutojihusisha kabisa katika michezo ndiyo kunakoweza kumfanya akafaulu mitihani yake jambo ambalo siyo kweli na mwishowe huweza kumfanya mtu anayefuata ratiba hiyo kusinzia darasani au kuchoka zaidi na mwishowe kusahau kwa urahisi yale aliyojifunza muda mfupi uliopita.

Ukweli ni kwamba unaposoma kwa muda mrefu na kulala muda mfupi kunachosha akili na kupunguza uwezo wa ubongo kupokea vitu vipya hali ambayo inahitaji kitu kingine kichangamshe ubongo kwa kuwa kitu kimoja kikifanyika kwa muda mrefu akili huchoka.

Moja ya shughuli inayoweza kufanya ubongo uchangamke kwa haraka ni aidha kwa kushiriki michezo mbalimbali ya vitendo kama mpira wa miguu au michezo ya kutumia akili kama vile drafti, karata na michezo ya aina hiyo.

Mbali na michezo hiyo pia mwanafunzi anashauriwa pindi anapochoka kwa kusoma apate muda wa kutosha wa kupumzisha akili yake kwa kulala ili kuupa ubongo nafasi ya kuhifadhi yale aliyojifunza na kutayarisha sehemu nyingine mpya ya kuhifadhi mambo mapya.

Mwanasayansi mmoja wa Marekani wa karne ya 18 aliyeitwa Benjamin Franklin aliwahi kusema: “Early to bed, early to rise makes a man healthy, wealthy and strong” akiwa na maana: “Kulala mapema, kuamka mapema kunamfanya mtu awe na afya, utajiri na nguvu.” Hapa alimaanisha kuwa hata mwanasayansi huyu alijua nini maana ya usingizi hasa ikiwa mtu atalala mapema na kuamka mapema na kufuata ratiba hiyo kila siku.

Miaka michache baada ya Benjamin kuyasema maneno hayo mitaala ya shule katika nchi mbalimbali ilibadilisha ratiba zao za shule na kuweka ratiba mbalimbali za masomo hasa kwa kuwepo kwa muda wa mapumziko huku shule za awali zikitoa muda wa wanafunzi kulala bila kuacha michezo angalau kwa wiki mara moja jambo ambalo linazingatiwa hata kwenye mitaala yetu nchini kutokana na umuhimu wake kwa wanafunzi.

Hivyo basi hata baada ya kutoka katika vipindi vya kawaida vya masomo ya mchana, mwanafunzi mwenyewe anatakiwa awe ameandaa ratiba yake maalum itakayohusisha mchezo wowote na baadaye masomo atakayojisomea kwa siku na kumaliza ratiba kwa kulala mapema na kuamka mapema ambapo pia atapata nafasi ya kuwahi shuleni na kupitia yale aliyojifunza hapo awali.

Leave A Reply