The House of Favourite Newspapers

UFISADI BIL 224 MLIMANI CITY ZIMEENDA WAPI?

Majengo ya Mlimani City.

 

SAKATA la ufisadi katika mkataba wa Mradi wa Majengo ya Biashara ya Mlimani City kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Mlimani City Holdings LTD iliyo chini ya Kampuni ya A Turnstar Holdings Group ya Botswana, sasa ni kaa la moto linaloweza kuwachoma wote waliohusika, Uwazi limedokezwa.

 

RIPOTI IMEKAMILIKA

Hatua hiyo inakuja kufuatia uongozi wa UDSM kukamilisha ripoti ya mkataba huo na kuikabidhi kwa Spika wa Bunge kabla ya kufikishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa ajili ya kuichambua na kuiwasilisha bungeni kwa hatua zaidi ikibidi za kisheria kama itathibitika kuna ufisadi.

Lakini kwa mujibu wa mwekezaji huyo, tayari amejenga maduka makubwa yenye hadhi ya kimataifa (Shopping Malls), ukumbi wa kimataifa wa mikutano, majengo manne ya ghorofa moja kila moja kwa ajili ya ofisi na nyumba za kuishi zipatazo 50 kwa jumla ya dola milioni 100 (zaidi ya shilingi bilioni 224 za Kitanzania), jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wa ubunifu wa miradi endelevu ya majengo walipingana nalo.

 

Kabla ya wachambuzi hao ambao ni wataalam wa majengo, kamati hiyo ya bunge ilinusa uwepo wa ufisadi katika mkataba huo ambapo pamoja na mambo mengine yaliyoacha watu midomo wazi, mwekezaji, wakati anaingia mkataba huo mwaka 2004, alipewa dhamana ya kuwekeza akiwa na mtaji wa dola 75 (takriban shilingi za laki moja na nusu za Kitanzania).

Jambo lililoshangaza wengi ni kwamba, UDSM ambacho ni kitovu cha wasomi nchini ilikubalije kumpa eneo mwekezaji aliyekuwa na shilingi 150,000 katika mradi huo mkubwa?

Lingine lililoibua maswali ni kwamba mwekezaji alitumia eneo la uwekezaji au upangishaji la UDSM kama dhamana ya kujipatia mkopo kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

 

 

Prof. Mukandala.

Pia kitendo cha serikali kupitia UDSM kuambulia asilimia 10 tu ya faida baada ya mwekezaji kutoa gharama zote za uendeshaji na mkopo wa mtaji wa Mlimani City kilisababisha sintofahamu.

Wakati UDSM wakiambulia asilimia 10, mwekezaji yeye anachota asilimia 90 ya faida ya mradi huo.

Pia ufisadi mwingine wa mradi huo ulitajwa kuwa ni kitendo cha mkataba huo wa Mlimani City kuwa ni wa miaka 50 ambapo ulianza mwaka 2004 na unatarajiwa kumalizika 2054.

Ilibainika pia kwamba, mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu yenye vyumba 100 na bustani havijaanza wakati mkataba ulionesha kuwa mradi huo uwe umekamilika mwaka huu.

 

UDSM WAFUNGUKA

Akizungumza na Uwazi juu ya sakata hilo, Afisa Uhusiano wa UDSM, Jackson Isdory alisema kuwa, mwanasheria wa chuo hicho, Profesa Bonaventure Rutinywa alifunguka kuwa suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa PAC ambao ndiyo wenye mamlaka ya kulitolea ufafanunuzi.

“Mwanasheria wetu amesema sisi kama chuo tulitakiwa kuandaa ripoti ya jambo hilo, nasi tumeshafanya hivyo kwa kujibu wa maswali ambayo yalihitaji majibu. Kwa hiyo hayo maswali yenu (waandishi) muiulize kamati ya bunge ndiyo yenye mamlaka ya kuiweka wazi,” alijibu Isdory kwa maelekezo ya Profesa Rutinywa.

 

PAC WANASEMAJE?

Baada ya kusikia upande wa UDSM, Uwazi lilimtafuta Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka bila mafanikio badala yake lilimpata makamu wake, Aesh Hilal ambaye alisema kuwa, inawezekana hiyo ripoti ikawa imemfikia Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye ataisoma kisha ataikabidhi kwenye kamati kwa ajili ya kuichambua na baadaye kuitolea uchambuzi ndani ya bunge.

“Kama umeambiwa na UDSM kuwa ripoti ipo tayari, itapita kwanza kwa spika kisha italetwa kwetu na kwa wabunge wote kwa ajili ya uamuzi wa bunge. Kwa hiyo ikitoka msijali mtapata ukweli wa sakata la Mlimani City,” alisema makamu huyo mwenyekiti ambaye pia ni mbunge wa Sumbawanga.

Naibu Mwenyekiti wa PAC, Aesh Hilal.

 

BIL. 224 INAENDANA NA MRADI?

Baadhi ya wataalam wa majengo waliozungumza na Uwazi walionesha shaka juu ya matumizi ya shilingi bilioni 224 kwa mradi wa majengo yaliyokamilika kwenye mradi huo na kutamani kujua mchanganuo wake kwa maelezo kwamba ni jambo lisilowezekana.

“Nimekuwa kwenye field (fani) ya ujenzi wa majengo marefu naya chini kwenye miji mingi mikubwa, lakini gharama zinazotajwa za ujenzi wa Mlimani City ni kubwa mno ukilinganisha na majengo yenyewe.

“Labda ninaweza kukubali kama wahusika (Mlimani City Holdings) wataonesha kitu kinachoitwa ‘Bills of Quantiy’. Hili ni kabrasha ambalo huonesha kila kitu kilichonunuliwa na sehemu kiliponunuliwa na hata ubora wa materials (vifaa vya ujenzi), lakini kwa mtazamo wa majengo ya Mlimani City na bilioni 224 ni mbingu na ardhi,” alisema mmoja wa wasanifu majengo wa Chuo cha Ardhi.

 

Mkaguzi wa Majengo, Theobald Wimile (kulia) akizungumza na Mhariri wa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Sifael Paul.

 

Mtaalam mwingine alisema: “Inawezekana Majengo ya Mlimani City yakawa yametumia gharama hizo kwa sababu kuna mambo mengi hapa ya kuandalia.

“Kwanza unaangalia eneo la mradi ambalo unataka kuweka majengo hasa suala la aina ya udongo.

“Ninavyojua pale Mlimani City kulikuwa na kitu tunachoita kwa kitaalam water table (mkondo wa maji), sasa lazima kuwe na gharama kuwa ya kushughulika kwanza na ardhi kwa ajili ya msingi imara kuliko hata jengo lenyewe.

“Pili kuna upatinaji wa materials (vifaa) za ujenzi kwa maana ya umbali. Sasa kama vifaa vinapatikana hapohapo ni tofauti na mradi ambao unaagiza vifaa kutoka mbali. Hapo lazima gharama zitofautiane.

“Na mwisho kuna suala la kiwango na ubora wa vifaa vya ujenzi. Mambo haya ndiyo yanayoweza kufanya gharama kuwa ndogo sana au kubwa sana. Kwa hiyo ishu ya Mlimani City inategemea na mkandarasi alitumia vifaa gani na kutoka umbali gani,” alisema mtaalam mwingine kwenye Chuo cha Ardhi kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa, hapendi kuhusishwa na suala hilo ambalo alidai limekaa kisiasa.

Mkaguzi wa Majengo, Theobald Wimile.

 

 

BODI YA WAKANDARASI WANASEMAJE?

Mbali na hao, Uwazi lilifika kwenye Ofisi za Bodi ya Usajili ya Ubunifu na Ukadiriaji wa Wakandarasi ambapo lilikutana na Mkaguzi wa Majengo, Theobald Wimile ambaye alisema kuwa, suala hilo linategemea na mahitaji ya mteja.

“Kuna aina mbili za miradi ambazo ndizo huamua kuhusu gharama za ujenzi. Mradi wa majengo ya bishara ni ghali mno ukilinganisha na majengo ya makazi.

“Tunachojua ni kwamba gharama ya ujenzi wa square meter moja ni shilingi laki tisa. Sasa inategemea pale Mlimani City wamejenga ukumbwa wa Square meter ngapi.

 

“Sasa ili kupata thamani ya majengo ya Mlimani City inabidi uzingatie mambo mengi sana kama uwepo wa water table (mkondo wa maji), ukubwa wa eneo na kiwango au ubora wa vifaa vya ujenzi.

“Lakini yote haya, unaweza kuyapata kwenye Kitabu cha Bills of Quantity ambacho kina orodha ya kila kitu na gharama zake, hapo ndipo unapoweza kupata thamani halisi ya majengo ya Mlimani City kama ni chini ya hizo bilioni 224 au ni juu yake,” alisema Wimile.

Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kuwa kuna baadhi ya maduka kama hayo ya Mlimani yaliyojengwa nchini Afrika Kusini na Kenya yana thamani chini ya dola za Kimarekani milioni 100, mengine hayazidi dola milioni 56.

 

STORI: WAANDISHI WETU, DAR

Comments are closed.