The House of Favourite Newspapers

Uingereza Yatoa Bilioni 307.5 Kuunga Mkono Juhudi za JPM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development – DFID – ), Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018.
Magufuli akimpa zawadi ya kinyago cha “Umoja”, Mhe. Mordaunt.
Magufuli akipeana mikono na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke aliyeongozana na Waziri Mordaunt.

 

Magufuli akimuonesha albamu ya picha Waziri Mordaunt inayoonesha Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa na Tetemeko la Ardhi mkoani Kagera lililotokea Septemba 10, 2016 ambayo imejengwa upya na serikali ya Uingereza kupitia mpango wake wa maendelo ya elimu kupitia UKAid/DFID. Picha hizo zinaonesha shule hiyo baada ya tetemeko, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi siku ya mwaka mpya wa 2017 na inavyoonekana sasa baada ya kujengwa upya.

Wakitoka nje ya Ikulu baada ya mazungumzo.
Magufuli akizungumza baada ya kutoka nje ya Ikulu akiwasindikiza na wageni wake (Picha na Ikulu).

Uingereza imetoa msaada wa Sh bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi Rais John Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

 

Akitangaza msaada huo Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa agosti 10, baada ya kukutana na Rais Magufulu, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Penny Mordaunt amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Rais Magufuli ambapo kati yake Sh bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu.

 

Aidha, Sh bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa na Sh bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo,” amesema Mordaunt.

 

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi” amesema Rais Magufuli.

 

Hata hivyo, Rais Magufuli amemuahidi Mordaunt kuwa fedha zilizotolewa zitatumika vizuri na kwamba Serikali itahakikisha uhusiano wa Tanzania na Uingereza unazidi kuimarishwa kwa kuwa inatambua kuwa Uingereza ndiyo mwekezaji mkubwa hapa nchini na imekuwa ikitoa misaada mikubwa ya fedha za walipa kodi wa Uingereza kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

Comments are closed.