The House of Favourite Newspapers

Ujatijiri wa Kutisha wa Ndesamburo Waanikwa

0

Stori:Waandishi Wetu | IJUMAA WIKIENDA

Kilimanjaro: Ni wiki moja imekatika sasa tangu shujaa wa demokrasia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Philemon Kiwelu Ndesamburo ‘Ndesa Pesa’ azikwe nyumbani kwake, Mtaa wa KDC, Barabara ya Mbokomu, nje kidogo ya Mji wa Moshi.

Nyuma ya kifo cha Ndesa Pesa aliyefariki dunia ghafla akiwa ofisini kwake mjini Moshi, akiwa na umri wa miaka 82, mambo mengi mazuri aliyoyafanya yangali yanazungumzwa, ikiwemo utajiri aliouacha, jambo ambalo linalisukuma Wikienda kutafuta undani wake na hapa linakuletea ripoti kamili ya utajiri wa kutisha wa Ndesa Pesa.

HOTELI ZA KITALII HADI LONDON

Kwa mujibu wa mmoja wa watoto wa Ndesa Pesa ambaye hakutaka kuandikwa gazetini, miongoni mwa vitega uchumi vya baba yake ni pamoja na hoteli za kitalii zilizopo katika Jiji la London, Uingereza, Kariakoo jijini Dar es Salaam na mjini Moshi.

Baadhi ya hoteli hizo, mbili kubwa zipo mkoani Kilimanjaro maeneo ya Rau na Kiborloni mjini Moshi ambapo pia zina ‘apartments’ nyingi ambazo wateja wake wengi ni watalii wa nje ya nchi.

KAMPUNI ZA UTALII

Mbali na hoteli hiyo, Wikienda lilitonywa kuwa, pia mbunge huyo mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini anamiliki kampuni kibao za usafirishaji hasa zile za ‘tours’ zinazosafirisha watalii kwenda kwenye mbuga za wanyama zikiongozwa na Keys Hotels Travel & Tours.

DALA DALA NA SHUTTLE KIBAO

Ilielezwa kuwa, ukiacha magari ya kusafirisha watalii, pia mzee Ndesa ameacha daladala na ‘shuttle’ nyingi zinazotoa huduma kwa wananchi hususan Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambazo zote huwa zimeandikwa ‘Ndesa Pesa’ kwenye kioo cha nyuma.

VIWANDA, MA DUKA NA REDIO

Ilifahamika kuwa, pia Ndesa Pesa anamiliki viwanda vidogovidogo vya pombe na maji ya kunywa. Mtoto huyo pia alifafanua kuwa, baba yake pia alikuwa akimiliki maduka makubwa ya bidhaa za jumla na kituo cha redio cha Moshi FM cha mjini Moshi kinachohudumia Mikoa ya Kaskazini kwa matangazo.

MA GARI KIBAO , LIMO HUMMER

Kuhusu kumiliki magari binafsi, jamaa huyo alifunguka kuwa, si rahisi kupata idadi ya magari ya Ndesa Pesa lakini katika kurahisisha mambo, alilionesha Wikienda moja ya magari yake ya kifahari aina ya Hummer H2 likiwa limeegeshwa katika moja ya majengo ya mzee huyo mjini Moshi.

HELI KOPTA MBILI

Ukiachilia mbali hoteli,makampuni, viwanda, maduka, magari, maghorofa na jumba la kifahari alilokuwa akiishi Moshi Mjini, ilielezwa kuwa, ndiye mmili wa helikopta au chopa mbili zilizokuwa zikitumiwa na Chadema wakati wa kampeni na kwenye operesheni zake mbalimbali ikiwemo Movement For Change (M4C), Amshaamsha, Sangara na nyinginezo.

JINA LA NDESA PESA

Ukiachana na mtoto huyo wa marehemu, Wikienda lilizungumza na wazee waliomfahamu Ndesa Pesa tangu ujanani ambao walieleza namna alivyopata utajiri wake. “Alianza biashara hizi za retail (duka la rejareja) tangu akiwa kijana mdogo.

Alikuwa siyo mtu wa kutawanya fedha.

Alikuwa na nidhamu ya fedha. “Baadaye aliingia kwenye maduka ya jumla na hapo ndipo alipojikita kwenye utalii na biashara kubwakubwa,” alisema mmoja wa wazee wa Mbokomu aliyemfahamu Ndesa Pesa.

“Kuhusu jina la Ndesa Pesa, lilitokana na yeye mwenyewe kuwaambia watu kwenye mikutano yake ya kisiasa kwamba anaitwa Ndesa Pesa kwa sababu ana fedha nyingi,” alisema mzee mwingine na kuongeza: “Pia tabia yake ya kusaidia yeyote mwenye shida bila kusita ililifanya jina la Ndesa Pesa kumkaa vizuri.”

HARAKATI ZAANZA

Ndesa Pesa alianza harakati za kisiasa mwaka 1988 alipokuwa miongoni mwa Watanzania waliodai mabadiliko ya Katiba, miaka ya 90 akawa mmoja wa waanzilishi wa Umoja wa Demokrasia Tanzania (Udeta).

Zilipoanza harakati za vyama vya siasa nchini mwaka 1992, Ndesa alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Chademana kikao cha kwanza kilifanyika kwenyemgahawa wake uliokuwamaeneo ya Kisutu, Dar.

Ndani ya Chadema, Ndesa ndiye mmiliki wa kadi namba kumi ya chama akiwa mmoja wa waasisi wa chama hicho, ambaye alitumia muda na rasilimali zake katika kuimarisha chama hicho.

Mwaka 1994 aligombea udiwani katika Kata ya Kiborloni, lakini hakushinda na hakukata tamaa kwani aliendelea na harakati na mwaka 1995 aligombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, akaangushwa tena.

Ndesa hakukata tamaa bali alijikita kutekeleza ahadi zote alizozitoa kwa wapigakura wa jimbo hilo na ikawa ndiyo kama amewaloga kwa kuwa alivyorudi kueleza nia yake ya kugombea ubunge walimuunga mkono kwa kishindo.

Wakati huo Chadema ilikuwa na Jimbo la Rombo huku majimbo ya Moshi Mjini, Vunjo, Moshi Vijijini, Hai na Siha yakiwa na wabunge wa NCCRMageuzi.

Ndesa aliendelea na jitihada hizo na mwaka 2000 majimbo yote yaliyokuwa chini ya NCCR-Mageuzi yalirudi CCM na kubakiwa na Moshi Mjini ambako alishinda kiti cha ubunge kwa mara ya kwanza.

Ndesa aliendelea kuwa Mbunge wa Moshi Mjini hadi mwaka 2015 alipostaafu siasa za ubunge.

Leave A Reply