The House of Favourite Newspapers

UJUWE UGONGWA WA SARATANI YA TEZI DUME

TEZI ya prostate ni tezi yenye umbile la donati, iliyoko chini ya kibofu cha mkojo. Tezi hii huzungukwa na mirija ya mkojo na uhusika uzalishaji wa maji maji yanayohusika na urutubishaji na usafirishaji wa mbegu za kiume (semen).

 

Moja ya maradhi yanayoshuhudia kampeni kubwa kukabiliana nayo katika miaka ya hivi karibuni duniani ni pamoja na maradhi haya ya saratani ya tezi dume kutokana na ukubwa wa athari inazosababisha.

 

Ni maradhi yanayoshika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume duniani. Pia ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.

 

Hata hivyo, satarani ya tezi dume kwa sasa inawapata zaidi wanaume kuanzia miaka 25.Ni ugonjwa hatari ambao usipobainika na kutibiwa mapema inakuwa tiketi ya kifo. Lakini habari njema zilizoibuka sasa kuhusu ugonjwa huo ni kuwa moja ya majaribio makubwa kabisa ya kimaabara kwa ajili ya saratani ya tezi dume yametoa matokeo mazuri mno, kwa mujibu ya watafiti wa Uingereza.

 

Dawa ya kutibu saratani ya tezi dume ambayo imesambaa imebainika kuokoa maisha wakati ilipotolewa mapema kwa mgonjwa, kwa mujibu wa utafiti wao. Majaribio hayo yaliitazama tiba mpya ya homoni ijulikanayo kama abiraterone kama inayotolewa kwa ziada kwa matibabu wapewayo wagonjwa wenye saratani  ya tezi dume, ambao walikuwa waanze tiba ya kipindi kirefu ya homoni.

 

Haya ni matokeo yenye nguvu zaidi tuliyowahi kushuhudia kuhusu saratani ya tezi dume – ni kama vile hutokea mara moja katika safari yetu ya kikazi. Hii ni moja ya upunguzaji mkubwa wa vifo tuliyowahi kushuhudia katika majaribio ya kimaabara kwa wagonwa wazee wenye saratani. Abiraterone, ambayo pia huitwa Zytiga, ni tiba ya homoni. Ni tofauti na chemotherapy, ambayo huua seli za saratani, hii huzua zaidi homoni za testosterone kuzifikia tezi za kibofu zisije tengeneza uvimbe.

 

Majaribo hayo yalihusisha wagonjwa 2,000. Nusu ya wanaume waliotibiwa na tiba ya homoni wakati nusu wengine walipokea tiba ya homoni na abiraterone. Kati ya wanaume 1,917 walioshiriki katika jaribio hilo, kulikuwa na vifo 184 katika kundi la wale waliopewa mseto wa dawa kulinganisha na 262 waliopewa tiba moja tu ya homoni.

 

Abiraterone tayari inatumika kutibu baadhi ya wanaume, ambao maradhi yamesambaa lakini matokeo yetu yameonesha kuwa wengi zaidi wanaweza kunufaika nayo. “Abiraterone inaweza kabisa kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi wa saratani ya tezi dume kuliko ilivyodhaniwa kabla.

 

Saratani ya tezi dume ni nini? Neno saratani hutokea wakati chembe chembe za uhai au seli katika sehemu fulani ya mwili zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili na kutengeneza vijiuvimbe vidogo vidogo. Kwa kawaida seli huwa zinajigawa, kupevuka na baadaye kufa kwa kufuata taratibu za mfumo wa mwili. Lakini seli za saratani hazifuati mfumo huo.

 

Badala ya kufa, zenyewe huishi muda mrefu kuliko chembechembe za kawaida na wakati huo huo huendelea kutengeneza seli nyingine na kuwa uvimbe wa saratani. Tezi dume hutokea katika mwili wa mamalia wa kiume pekee pale seli katika kiungo hicho zinapoanza kukua bila kufuata utaratibu wa mfumo wa mwili hapo ndipo mtu hupata saratani ya tezi dume.

 

Ugonjwa huu pia hujulikana kama saratani ya kipofu cha mkojo. Kuna visababishi vingi vinavyochangia mwanaume kupata saratani ya tezi dume. Vifuatavyo ni baadhi yake: Kwanza kabisa ni umri. Nafasi ya kupata saratani ya tezi dume huongezeka sana hasa ukifikia umri wa karibu miaka 50 na kuendelea.

 

Nasaba ni kihatarishi kingine ambapo wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zao wamewahi kuugua ugonjwa huu huwa katika hatarini ya kupata kansa hiyo kutokana na kurithi jeni za ugonjwa huo. Suala jingie ni lishe ambapo wanaume wanaopenda kula nyama na walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume.

DALILI KUU

Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume . Dalili hizo ni pamoja na kupata shida wakati wa kuanza kukojoa, kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa, kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu. Kadhalika kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote na kutoa mkojo uliochanganyika na damu.

 

Pamoja na kueleza dalili hizo inapaswa kutambulika kuwa, mwanaume anapoanza kuona na kuhisi baadhi ya dalili hizo, anapaswa kujua kuwa, seli za saratani katika tezi dume lake huwa zina umri wa takribani miaka saba na kuendelea. Iwapo saratani imesambaa mwilini kiasi cha kuhusisha sehemu nyigine za mwili, mgonjwa anaweza kuwa na maumivu makali ya mifupa katika maeneo ya nyonga, mapajani na kiunoni.

 

Aidha mgonjwa huwa na dalili nyingine zinazoweza kumpata mgonjwa mwingine yeyote wa saratani kama vile kupungua uzito, kuhisi kichefuchefu, uchovu, kizunguzungu na kadhalika. Wanaume wanashauriwa kufanyiwa uchunguzi kwa kuwa imegundulika kuwa wanaume wengi wakiziona na kuzihisi dalili hizo huona soni kwenda kumwona daktari.

 

Baadhi ya watu huzihusisha na magonjwa ya zinaa au na dhana potofu za kishirikina. Wapo wanaokwenda mbali zaidi hata kuuita ugonjwa huo kuwa ni wanaume wanaopenda uhusiano wa kinyume na maumbile huku wengine wakiurahisisha kwa kuuita kuwa ni ugonjwa wa utu uzima kana kwamba saratani ya tezi dume ni jambo la kawaida kwa watu wazee.

 

Mambo kama hayo hupelekea wanaume wengi kujinyanyapaa wenyewe na hata wengine kujitibu kwa uficho au kwa kutumia waganga wababaishaji mpaka pale mambo yanapokuwa yamewazidi ndipo hupelekwa hospitalini na mara nyingine huwa wamechelewa na kupoteza maisha yao bure kwa ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa mapema.

Comments are closed.