UKIONA DALILI HIZI, TAMBUA WEWE SIYO CHAGUO LAKE -2

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko vizuri! Ni wiki nyingine tunapokutana jamvini, ikiwa ni wiki ya kwanza ya mwezi wa mwisho kwa mwaka 2018, mwaka ndiyo huo unaelekea ukingoni! Wiki iliyopita tuliianza mada hii kama inavyojieleza hapo juu, asante kwa wewe uliyeshiriki kutoa maoni yako. Kama nilivyosema, nasisitiza tena kwamba siyo kila ombi la kutaka mtu fulani awe mpenzi wako litakubaliwa, unaweza kuwa na malengo mazuri na mtu lakini kwa bahati mbaya ukawa siyo chaguo lake.

Wachache huwa na ujasiri wa kukueleza mapema kwamba HAIWEZEKANI lakini wengi huwa wanakufikishia ujumbe kwa vitendo na miongoni mwa vitendo hivyo, ni vile tulivyojadili wiki iliyopita; haishiwi na visingizio mnapopanga appointment, anasisitiza kuhusu urafiki wa kawaida, hataki uuguse mwili wake, anakupa majibu ya mkato na ya kukatisha tamaa na hataki watu wake wa karibu wakujue.

Nilichokibaini ni kwamba kumbe kuna idadi kubwa ya watu ambao huwa wanatokewa na hali hii na pengine kwa sababu ya kutojua kusoma alama za nyakati au kuwa ving’ang’anizi tu, hujikuta wakiishia kwenye mateso makubwa ya nafsi au kuingia kwenye ugomvi usio na maana.

Mwanamke kumzungusha mwanaume anapomtamkia kwamba anamhitaji kimapenzi, ni jambo la kawaida kwa sababu ya ile haiba ya kike. Kuna ule uzungushaji wa kawaida ambao ni lazima utakuwepo kutokana na wanawake kuwa na kasumba kwamba unapomkubalia mwanaume haraka, anaweza kudhani kwamba hujatulia au wewe ni ‘maharage ya Mbeya’.

Hapa sizungumzii uzungushwaji huu ambao ni wa kawaida, bali ule ambao mtu anakuwa hakutaki kabisa lakini anaogopa kukwambia moja kwa moja kwamba wewe siyo chaguo lake, kwa hiyo matokeo yake anakufikishia ujumbe kwa njia ya mkato. Unapogundua kwamba hana taimu na wewe, hajavutiwa na wewe wala wewe si chaguo lake, unachopaswa kukifanya kwanza ni kukubaliana na hali halisi. Huna haja ya kujenga uhasama na uadui na aliyekukataa, ichukulie hiyo kama changamoto na jipange upya.

Wakati mwingine unatakiwa kumshukuru Mungu kwa sababu hujui amekuepusha na kitu gani katika siku za mbele, wala huna haja ya kujisikia vibaya kwa sababu ni jambo la kawaida. Baadhi ya watu wana tabia za hovyo, kwamba inapotokea mtu fulani amekataa ombi lake la kuwa naye kwenye uhusiano, basi atamfanyia visa mpaka akome, katika mapenzi huo ni ushamba na unyanyasaji ambao unapaswa kukemewa. Huna sababu ya kumlazimisha awe na wewe wakati wewe siyo chaguo lake. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Loading...

Toa comment