The House of Favourite Newspapers

Ukweli wa Viumbe Waishio Angani-13

0

Scary_Movie_Aliens.jpgVIUMBE WA AJABU WASITISHA SAFARI ZA MWEZINI

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Mpenzi msomaji wangu wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nikielezea namna ambavyo Aliens na UFO vilivyoanza kuonekana kwenye anga la Israel, Iran na Australia. Ukweli ni kwamba tukio hilo lilishuhudiwa na maelfu ya watu ambao waliona UFO zikisafiri mita 200 kutoka ardhini. SASA ENDELEA…

Watafiti wengi duniani wameendelea kulishughulikia suala la Aliens na UFO ili kupata majibu ya maswali kuhusiana na asili yake ni nini na tija au madhara yake kwa binadamu wa sasa ni yapi.

Hakuna kati ya watafiti hao aliyekuja na majibu ya kuridhisha au majibu rasmi kuhusiana na suala hilo.
Kama UFO zitakuwa ni kweli zipo na asili yake hasa ni kutoka nje ya Sayari ya Dunia, ukweli huo, hapana shaka utakuwa ni changamoto ya namna yake kwa binadamu wote.

Kwa upande mwingine, ikiwa UFO si hivyo vitu tunavyoambiwa na si hivyo inavyoelezewa na wale walioshuhudia, basi vyombo hivyo vitakuwa ni ushahidi wa kutosha wa mpango kabambe ambao mabilioni ya binadamu hawafahamu hatima na malengo yake ni nini na ambao athari yake huenda ikamuathiri kila binadamu aliyepo kwenye sayari hii.

Wakati hayo yakiendelea, kuna kabrasha linaloelezea kwamba, baadhi ya wanaanga wa Marekani walifikia hatua ya kusitisha safari za kwenda mwezini baada ya kudaiwa kugundua kwamba kuna viumbe wa ajabu wenye makazi yake huko.

Takriban miaka 50 iliyopita, mwanaanga wa Marekani, Neil Armstrong alitua na kutembea mwezini na hivyo kuwa mwanadamu wa kwanza kuchukua hatua hiyo.Kwa mujibu wa Armstrong, hatua aliyochukua yeye ilikuwa ndogo kwa mtu, lakini ilikuwa kubwa sana kwa binadamu wote na ilijaa vitisho na hofu kubwa.

Kwa kumpeleka mwanadamu mwezini, Marekani iliishinda Urusi katika mashindano ya kudhibiti anga za mbali lakini ghafla Marekani ikawa kwenye mshtuko na inaelezwa kwamba hawakuwa wazi kueleza kwa kina walichokutana nacho ambacho walidhani kingeweza kuwa tishio kwa wanadamu.

Ilikuwa Julai 20, mwaka 1969 ambapo chombo cha anga cha Apollo 11 kiliwapeleka angani wanaanga watatu wa Marekani, Neil Armstrong, Buzz Aldrin na Michael Collins na kuweka historia hiyo kubwa duniani kwa kusimika bendera yao huko lakini baadaye ilizua maswali kwani bendera yao ilikuwa ikipepea, jambo ambalo si kweli kwani hakuna upepo wa kuifanya ipepee.

Licha ya matatizo ya kompyuta au teknolojia ya wakati huo, chombo cha Apollo 11 kilifanikiwa kutua mwezini. Wanaanga hao walikabiliwa na chaguo la kugeuza na kurudia au kuendesha mitambo kwa mikono yao. Walitumia mikono yao kuendesha mitambo. Armstrong alikuwa wa kwanza kuteremka na kutembea mwezini.

Watu zaidi ya nusu bilioni duniani kote walifuatilia tukio hilo kwenye televisheni na video zilizosambaa baadaye.
Vitabu vya historia vinaonesha kwamba mradi huo wa kwenda mwezini ulianza Mei 25, mwaka 1961 wakati John Kennedy (aliyewahi kuwa Rais wa Marekani) alipotamka:

“Marekani imechagua kwenda mwezini, siyo kwa sababu ni rahisi kufaya hivyo, bali kwa sababu ni vigumu.”
Huo ulikuwa ni wakati ambapo vita baridi baina ya Marekani na Urusi vilikuwa vimeshamiri. Urusi ilikuwa mbele katika utafiti wa anga na ndiyo ilikuwa ya kwanza kupeleka satelaiti angani na mwanaanga- Yuri Gagarin lakini hakutua mwezini. Kutokana na hayo, Marekani ilipania kwa kila hali kumpeleka mwanadamu kwenye mwezi na ilifanikiwa.

Safari zingine tano zilifuatia. Kwa jumla, Wamarekani 12 wamepata kutua mwezini. Lakini shangwe zote zilitoweka ghafla. Mmarekani wa mwisho kwenda mwezini alikuwa Eugene Cernon mnamo mwaka 1972. Baada ya hapo mradi wa Apollo ulimalizika.

Leave A Reply