Umuhimu wa Kufanya Maamuzi Sahihi Kwa Dunia ya Leo
NI wiki nyingine tena tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba kwa rehema zake Mwenyezi Mungu umzima, bukheri wa afya na unaendelea vyema na mishemishe za kila siku za kuyaboresha maisha yako. Aidha, nichukue fursa hii pia kuwashauri ndugu zangu Waislam na Wakristo kwa jumla kwamba, ifike wakati tuseme inatosha kumkasirisha Mungu wetu kwa kutenda maovu.
Tuseme tu inatosha kwa ulevi, uzinzi na mambo mengine ambayo mafundisho matakatifu yanatufundisha kutoyafanya. Naamini kabisa kwa kufanya hivyo Mungu atatujalia heri katika maisha yetu ya kila siku na kutupa uwezo wa kuyatimiza yale ambayo tumekuwa tukiyaota maishani mwetu. Huwezi kuwa unatamani kufanikiwa halafu ukawa unamsahau Mungu anayeweza kukubariki katika hilo. Mshike Mungu wako, mshirikishe katika unayoyafanya na umuombe awe nawe katika safari yako. Kwa kufanya hivyo hakuna litakalokushinda.
Baada ya kusema hayo sasa nirudi katika mada yangu ya leo ambayo inahusu umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ambayo yatatufanya tupate kile tulichokitarajia hasa kutokana na ukweli kwamba, dunia yetu ina vitu vingi ambavyo vinatulazimisha kuwa makini katika kuchagua ili tupate vilivyo bora. Duniani kuna wanawake wengi wazuri, lakini si wote wanaofaa kuoa, wanaume wapo wengi, kazi ziko nyingi, elimu, vitu, mavazi, vyakula, dawa na shule.
Kila unaloweza kuwaza linapatikana kwa wingi.
Hivyo ni jukumu la mwanadamu mwenyewe kufanya maamuzi sahihi ili aweze kufikia kilele cha ubora anaouhitaji katika maisha yake. Hii ni kwa sababu, maamuzi yaliyo sahihi ndiyo yanayoweza kukupatia majibu sahihi na maamuzi ya kukurupuka siku zote mwisho wake ni kujuta. Ikiwa mwanamke alikuwa akiota kuwa na mume mpole, mwenye kumhesimu na kumpenda kwa dhati na akajikuta amempata aliye tofauti, ajue kwamba alifanya maamuzi mabaya ya kuwa na uhusiano na mwanaume huyo. Huu ndiyo ukweli kwamba watu wengi wameshindwa kuchagua mazuri na sasa wanalia na mabaya waliyoyachagua wenyewe.
Kadhalika, juhudi wanazotumia wanaume waliooa wanawake wasiojua nini maana ya ndoa ni kubwa zaidi ukilinganisha na zile ambazo wangetumia kuchagua wanawake wema wa kuwafaa maishani mwao. Ndiyo maana mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kuwa, mtu mwenye busara lazima aitumie kabla ya kufanya maamuzi na siyo baada ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Wachache sana hutumia busara wanapochagua, wengi wao wanapopata matokeo mabaya ndipo huanza kutumia busara kuyakabili wakati walikuwa na nafasi ya kufanya hivyo kabla na wakaona mafaniko sahihi. Tunapobahatika kupata pesa nyingi kwa mfano, tunakuwa na mipango ishirini au zaidi. Mara kununua gari la biashara, mara kufungua duka, hoteli na hata kulima, lakini tunazembea katika kuchagua na kujikuta tumeangukia kwenye uchaguzi mbaya ambao mwishowe hutuhuzunisha.
Niseme tu kwamba ili tuweze kuwa na maisha mazuri tuna kila sababu ya kuwa makini sana katika kuamua na kuwa na uhakika kwamba mwisho wa maamuzi tunayoyafanya leo ni kupata kile tulichokitarajia. Tunaweza kufikia maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi wetu kwa kuzingatia yafuatayo. Kwanza, ni kutambua mahitaji yetu na kuyaorodhesha kwa lengo la kupata dira ya kuelekea kwenye uchaguzi mzuri. Pili, kwa kuwa dunia ina vitu vingi vya kufanana sawa na unavyohitaji ni vema ukatulia katika mawazo kwa muda mrefu kabla ya kufikia maamuzi. Tafakari kwa kulinganisha vitu unavyoviona na malengo yako kisha hakiki majibu unayopata kwa kila hatua.