The House of Favourite Newspapers

Un ending love -72

5

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Cha ajabu, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, Jafet anapowasili nchini India, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Anna anakuwa gumzo kila sehemu.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Nakushukuru sana mpenzi wangu, haya yote yasingewezekana kama na wewe ungeamua kunilipa mabaya. Hata sijui namna ya kukushukuru,” alisema Anna na kumkumbatia Jafet kwa nguvu kifuani kwake.

“Usijali Anna, niliahidi kuwa na wewe katika shida na raha. Uzima wako ndiyo kitu chenye thamani kubwa kuliko vyote kwa sasa,” alisema Jafet, kauli iliyomfanya msichana huyo aendelee kumganda kama ruba huku machozi yakimtoka kwa wingi na kumlowanisha Jafet.

“Inabidi tumshukuru Mungu kama mchungaji alivyotuambia, haya inuka tusali,” alisema Jafet huku akimfuta machozi msichana huyo. Wakapiga magoti na kuanza kusali.

Siku hiyo ilipita, Anna akaendelea kuwa gumzo kila sehemu, watu wengi wakitaka kujua ni kitu gani kilichomsaidia mpaka akapata ahueni kubwa ya maradhi ya figo yaliyokuwa yanamsumbua.

Madaktari nao waliendelea kumchunguza Anna kwa karibu, wakifuatilia maendeleo yake hatua kwa hatua. Kama walivyokubaliana, hawakuendelea tena kumfanyia Dialysis kutokana na kuimarika kwa afya yake. Hata idadi ya dawa alizokuwa anapewa, pia ilipunguzwa sana kwa sababu hakukuwa tena na ulazima.

“Hali ikiendelea hivi nadhani tutawaruhusu mrudi nyumbani.”
“Ooh! Tutashukuru sana daktari,” alisema baba yake Anna wakati akizungumza na daktari aliyekuwa akisimamia matibabu ya mwanaye.

Siku kadhaa baadaye, Anna aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo, wakaondoka pamoja mpaka kwenye hoteli waliyokuwa wamefikia wazazi wake pamoja na Jafet. Kila mmoja alikuwa na furaha kubwa kutokana na maendeleo ya Anna. Alibadilika na kunawiri vizuri, urembo wake wa asili ukawa unajionesha dhahiri.

“Unajua wewe ni mrembo sana Anna, ukikaa na kutulia unapendeza sana,” alisema Jafet wakiwa wamekaa kwenye ngazi za kuingilia kwenye chumba cha Jafet hotelini hapo, muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini. Kauli hiyo ilisababisha Anna acheke kwa furaha, akamkumbatia Jafet na kumbusu.

“Asante sana Jafet, hakuna kitu kinachonipa raha kama kukusikia ukinisifia,” alisema Anna kwa sauti ya kudeka.
“Na leo namwambia baba nataka kulala na wewe chumbani kwako,” alisema Anna na kumfanya Jafet ashtuke. Kwa kipindi chote alichokuwa karibu na Anna, japokuwa makubaliano kati yake na baba yake Anna ilikuwa ni ‘kuekti’ kama anampenda binti yao, Jafet alijikuta katika wakati mgumu sana kihisia.

Japokuwa Anna alimkosea, ndani ya nafsi yake alishamsamehe na kubwa zaidi alikuwa anapenda kumuona akifurahi. Awali alikuwa anachukulia kawaida lakini kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, alianza kuhisi hali ya tofauti anapokuwa na Anna; bado alikuwa anampenda.

Kilichomfanya abaki njia panda ni ukweli kwamba nchini Tanzania, tayari alikuwa ameanzisha uhusiano wa kimapenzi na msichana mwingine, Suleikha ambaye alionesha kumpenda kwa dhati kutoka ndani ya moyo wake.

Kibaya zaidi, tayari alishakutana kimwili na Suleikha na kwa hali ilivyokuwa, hakukuwa na namna anayoweza kuitumia kusitisha uhusiano wake wa kimapenzi na Suleikha.
“Naongea na wewe Jafet, mbona kama unawaza sana?” kauli hiyo ya Anna ndiyo iliyomzindua Jafet kutoka kwenye lindi la mawazo, akawa ni kama amemwagiwa maji ya baridi.

“Hujanisikia au? Nasema leo namwambia baba nataka kulala na wewe, au hutaki?”
“Hakuna shida Anna, sema chochote unachokitaka, siwezi kukubishia chochote,” Jafet alivunga, wakaendelea na stori za hapa na pale. Muda mfupi baadaye, baba yake Anna aliyekuwa ametoka na mkewe kwa ajili ya kwenda kushughulikia masuala ya safari ya kurudi nchini Tanzania, alirejea na kuwakuta Jafet na Anna wakipiga stori za kawaida.

Kama alivyoahidi, kweli Anna alimwambia baba yake kwamba wasihangaike kukodi chumba kingine kwa ajili yake kwa sababu anataka kulala na Jafet. Kauli hiyo ilimshtua kidogo baba yake Anna lakini kwa kuwa hakutaka kumkasirisha kwa chochote, alimkubalia lakini akatoa masharti.

“Najua mnapendana lakini ‘no sex before marriage’ (hakuna kukutana kimwili kabla ya kuoana), sawa Jafet,” alisema baba yake Anna na kusababisha wote wacheke kwa aibu. Anna akainuka pale alipokuwa amekaa na kumkumbatia baba yake kwa furaha. Baba yake Jafet naye alitumia muda huo kumpa ishara fulani Jafet ya kumtaka aendelee kuigiza kama anampenda sana Anna hata kama haikuwa kweli.

Siku hiyo ilikuwa ya furaha sana kwa Anna, kitendo cha baba yake kumpa ruhusa ya kulala na Jafet kilimfanya ajihisi kama anapaa bila mbawa. Japokuwa baba yake alitoa masharti, Anna alikuwa akiwaza mambo tofauti kabisa, alijiapiza kuutumia usiku huo kuweka mambo sawa kati yake na Jafet.

Kwa kuhofia kinachoweza kutokea wawili hao wakilala pamoja, baba yake Anna aliamua kutumia akili za kiutu uzima, akawachanganyia dawa ya usingizi kwenye juisi wakati wa chakula cha usiku. Muda mfupi baadaye, wote wawili walianza kusinzia, akasaidiana na mkewe kuwapeleka kwenye chumba cha Jafet huku wakipongezana kwa kuwazidi ujanja Anna na Jafet.

Hakuna aliyezinduka mpaka kesho yake asubuhi walipoenda kuamshwa kwa ajili ya kujiandaa kwa safari ya kurejea Tanzania.

“He! Kumeshakucha? Imekuwaje tumelala namna hii? Haiwezekani,” alisema Anna akionesha kushangazwa sana na kilichotokea. Hakukuwa na muda wa kupoteza, maandalizi ya safari yakapamba moto na muda mfupi baadaye, walitoka mpaka uwanja wa ndege.

“Nilipanga kukufanyia mambo mazuri sana usiku, sijui shetani gani akatupitia,” alisema Anna wakati wakiingia uwanja wa ndege na kusababisha wote wawili wacheke kwa furaha. Hakuna aliyekuwa na majibu ya kilichotokea usiku huo.

Baada ya kukamilisha taratibu zote uwanjani hapo, wote wanne waliingia mpaka ndani kabisa na kwenda kwenye ndege kubwa ya Fly Emirates waliyopanga kuondoka nayo. Wakaungana na abiria wengine kupanda kwenye ngazi za ndege hiyo na muda mfupi baadaye, kila mmoja alikuwa amekaa kwenye siti yake, Anna akiwa amekaa siti moja na Jafet. Safari ya kurejea Tanzania ikaanza.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

5 Comments
  1. hussein hasaani says

    bonge la story suleigha nafas yako ipo bado

  2. hussein hassani says

    suleigha hataari

  3. VITUS AIDAN says

    lkn baba aliwaania hakutenda haki kabisa juu yao

  4. Bongoman says

    Stori hii inayo contradiction moja. Kama Anna alikuwa na matatizo ya figo, does it make sense for her parents kuweka dawa ya usingizi kwenye juice? Which is better for Anna, to make love or to end up in a hospital again after being drugged?

  5. David Bupilipili says

    Iko poa

Leave A Reply