The House of Favourite Newspapers

Uso kwa uso na mtoa roho!-4

0

ILIPOISHIA:
“Kumbe ni kweli!” nilijikuta nimeropoka kwa sauti kubwa, kauli iliyosababisha wanafunzi wote pamoja na mwalimu wanigeukie pale nilipokuwa nimekaa, nikasikia miguno ya chinichini ikitawala darasa zima.
SASA ENDELEA…

“Ni kweli nini?” mwalimu wetu wa darasa, Madam Timbuka alihoji huku akinifuata pale nilipokuwa nimekaa. Nilijisikia aibu kubwa iliyochanganyikana na hofu, sikujua nimjibu nini mwalimu huyo kwani ndani ya akili yangu, nilikuwa nimezipokea tofauti taarifa hizo za ugonjwa wa mwalimu Mwashambwa na kile alichoniambia baba kwamba mwalimu huyo alikuwa mchawi na walikuwa wakishirikiana na marehemu Mwankuga.

“Naongea na wewe Togolai, ni kweli nini?” alihoji tena Madam Timbuka, safari hii akiwa amenikaribia kabisa pale nilipokuwa nimekaa, nikaanza kubabaika huku hofu kubwa ikishindwa kujificha kwenye uso wangu.

“Kwamba mwalimu wetu anaumwa. Nilisikia asubuhi nikawa siamini,” nilidanganya, nikamuona mwalimu Timbuka akishusha pumzi ndefu, wanafunzi wenzangu waliokuwa wakinitazama kwa shauku, nao walionesha kuridhika na majibu yangu.

Baada ya kutoa taarifa hizo, mwalimu Timbuka alitutaka tusipige kelele bali tuutumie muda huo kujisomea, akatoka na kutuacha wote tukiwa kimya. Moyoni mwangu niliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

“Kwa hiyo mwalimu Mwashambwa naye atakufa?” nilijiuliza moyoni wakati nikiendelea kutafakari taarifa za ugonjwa wa mwalimu wetu. Nilijaribu kuunganisha matukio, hofu ikazidi kuongezeka ndani ya moyo wangu. Bado sikutaka kuamini kwamba baba alikuwa mchawi na alikuwa akihusika na kilichokuwa kinaendelea.

Muda ulizidi kusonga mbele, hatimaye ukawadia muda wa mapumziko. Kwa kawaida, ilikuwa ikifika muda wa mapumziko, kengele inagongwa mara mbili kuashiria wanafunzi wote tutoke madarasani lakini siku hiyo, kengele iligongwa tofauti. Iligongwa mfululizo huku walimu wakiwa wameshatoka na kusimama mstarini, kila mmoja akionekana kuwa ‘siriasi’.

“Kuna nini kwani?” nilijiuliza wakati nikisimama na kutoka pamoja na wanafunzi wenzangu, tukaelekea mstarini huku kila mmoja akiwa na shauku kubwa ya kusikia kilichofanya tukusanyike muda huo, jambo ambalo siyo la kawaida.
Mwalimu mkuu wetu, Nyerema alisimama na kututaka wote kutuliana kumsikiliza alichokuwa anataka kutuambia.

“Ni siku mbaya kwetu, najua wote mnajua kwamba mwalimu wenu, Mwashambwa alikuwa anaumwa sana, taarifa mbaya ni kwamba hatunaye tena, tumepokea taarifa za kifo chake muda huu, nawaomba nyote mtulie na muwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, taratibu nyingine mtatangaziwa baadaye,” alisema mwalimu Nyerema, vilio vikaanza kusikika kutoka kwa wanafunzi.

Siyo siri nilipatwa na mshtuko mkubwa sana, sikutaka kuamini kwamba mwalimu Mwashambwa ameondoka. Niliunganisha matukio na kile nilichoelezwa na baba, nikawa siamini.

“Ina maana baba ndiye anayehusika na kifo cha mwalimu wetu pia?” nilijiuliza moyoni nikiwa bado nimesimama palepale. Nikiwa katika hali ile, nilihisi kuna mtu ananitazama, nikageukia kule mtu huyo alipokuwepo.

Hakuwa mwingine bali mwalimu Timbuka ambaye alikuwa akinitazama kwa makini. Kwa ilivyoonesha, alikuwa akinitazama kwa muda mrefu, nikabaki kubabaika kwa sababu sikuelewa kwa sababu gani ananitazama namna ile.

Ili kuvunga, nilijichanganya na wanafunzi wengine na kuondoka eneo hilo, nikarudi darasani ambako wanafunzi wengi walikuwa wakiendelea kulia kwa uchungu. Baadaye kengele iligongwa tena, tukatoka na kwenda mstarini ambapo tulipewa utaratibu wa namna ya kushiriki msiba wa mwalimu wetu.

Wakati wanafunzi wengine wakifunga safari kuelekea kwa mwalimu Mwashambwa, mimi nilichepuka na kukimbilia nyumbani, moyoni nikiwa na dukuduku kubwa.
“Amekufa kama ulivyosema.”

“Si nilikwambia? Umeamini sasa!”
“Kwa hiyo wewe ndiyo umemuua? Kwani baba wewe ni mchawi?” nilijikuta nikimuuliza baba swali ambalo hata yeye hakulitegemea, akanitazama kwa macho ya ukali.

Je, nini kitafuatia? Usikose wiki ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply