The House of Favourite Newspapers

UNAACHA NYAMA NYUMBANI, UNAKIMBILIA MISHKAKI BAA !

NIPO tena nimejaa tele kama tui la nazi, ushindwe wewe tu uniungie kwa samaki au maharage! Halooo ehhhh! Mama matashtiti nimerudi mjengoni, mama wa kujiachia upo nyonyo?  Shoga wiki iliyopita nilikuwa na waleee wakinababa ambao wanageuza wake zao kama vile umeme wa luku au vocha za kukwangua, wanachojua wakifunga ndoa ni kuweka ndani, utakuta mwanamke mzima hana hata sehemu ya kuingiza kipato, kageuzwa mama wa nyumbani.

Waswahili wanasema, jiko la gesi tangu lini likachoma mahindi? Sasa kama nilivyowaambia leo bado nipo na hawaaa wakinababa wale ambao kumshirikisha mkewe mshahara anaona kama analetewa nuksi ndani ya nyumba, shuuuutuuuu!

Ninayosema nayaona shoga! Waliyosema tembea uone wala hawakukosea na embe lililoiva linaanguka lenyewe, hivi jamani ifike mahali basi hata tuoneane aibu kwenye ndoa, janaume zima umeolewa nalo, mna watoto, mmebarikiwa kupata kazi bado linakuficha mshahara wakati wako linaujua inahu?

Mbaya zaidi sasa, katika kupanga majukumu utakuta ndilo la kwanza kukuelemea, linataka watoto msaidiane kusomesha, kununua vyakula vya ndani ni wewe, kama kuna dada wa kazi wewe ndiyo umlipe mshahara bado una kausafiri kako kila kitu anataka wewe ndiyo uhudumie, loooo! Aibuuuuu! Heee heeeiya nicheke miye, papai na ukubwa wake linashindwa bei na tufaha japo ni dogo, shoga na hamu ya kumjua aliyeleta huu

msemo wa mwanaume suruali maana wala hakukosea, hivi kwanza unaanzajeanzaje kuishi na mwanamke humuweki wazi mshahara wako? Ndiyo kusema atakuibia au atakuteka! Hiviiii! Tangu lini kuku wa kuchora akawika au kutaga mayai? Badilikeni bwana, mkiamua kuishi maisha ya mume na mke ni vizuri basi

kuwekana sawa mambo ya msingi, kwanza inasaidia kurahisisha maisha yenu, mwanamke kujua mshahara wa mumewe inasaidia hata matumizi mabaya ambayo pengine ungeyafanya bila manufaa yoyote, au nadanganya? Sawa hatukatai, mwanaume ni kichwa cha familia lakini kumbuka mwanamke naye ndiyo kiwiliwili, kuna majukumu mengine yanatosha kabisa kuyafanya baba na mengine madogo-madogo yanatosha kuyafanya mama na hii ni pale mnapowekana vitu wazi au siyo nyonyo?

Kutomuweka wazi mwanamke mshahara ni sawa na kuacha nyama nyumbani na kukimbilia kwenda kula mishikaki baa sasa jiulize hiyo akili au matope? Wengine kwa mkewe anaficha lakini akiwa kwa mchepuko anamuambia mshahara wake tena hadi matumizi anapangiwa, heee heeeiyaaa hukushiba kwa tonge unataka kushiba kwa kulamba!

Nimeongea sana hadi nahisi koo kunikauka, badilikeni wanaume nyie maneno yangu kama sukari, usiponikorogea kwenye chai basi utaniweka kwenye maandazi, tangu lini muwasho wa ulimi ukakunwa kwa kidole! Na nimewawasha sana ili tu mbadilike.

Maoni na ushauri namba zangu hizo hapo juu, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri zaidi, ni mimi Anti Naa Shangingi Mstaafu

Comments are closed.