The House of Favourite Newspapers

Unataka kuolewa, kuoa au kufunga ndoa?-2

0

KARIBUNI sana wapendwa wasomaji wangu katika safu hii ya kuelimishana kuhusu maisha na mapenzi kwa ujumla wake. Ni Jumanne nyingine ambayo namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufika salama kwa sababu ya neema yake.
Mada yetu inatoka wiki iliyopita ikisema; unataka kuolewa, kuoa au kufunga ndoa?
Katika mada ile nilizungumza mengi lakini niliishia kwenye wawili wanaposahau ahadi ya kiapo siku ya ndoa yao.
Nilisema kwamba, inakuaje wakati wa tabu wanandoa  wanasahau kiapo? Au tabu zinazotegemewa na wanandoa wengi ni zipi? Kama zipo zaidi ya hizi zinazojulikana, basi kuna umuhimu wa wafungisha ndoa wanapouliza waziambatanishe na tabu zenyewe ili maharusi wachague kuingia au la!
Wiki hii tunaendelea hapa…

KUOLEWA, KUOA AU KUFUNGA NDOA
Katika utafiti wa kawaida utabaini kuwa, wengi wanapenda kuolewa au kuoa lakini hawako tayari kufunga ndoa.
Ninaposema kufunga ndoa ndiyo hitimisho la maisha ya wawili waliokubaliana kuishi pamoja. Hakuna lingine. Watu wanaopendana, wakakubaliana kuishi katika shida na raha siku zote hushikamana kuanzia siku ya kwanza ya maisha yao hadi siku ya kifo cha mmoja wapo.

Waliofunga ndoa, mmoja anapoibua tatizo la kusababisha ndoa kuvunjika, mfano mke kumfumania mumewe au usaliti mwingine wowote ukiwemo wa mke kubainika kuzaa nje ya ndoa, husigana lakini baadaye huendelea na safari. Hiyo ndiyo ndoa.
Waliofunga ndoa, inapotokea labda mume hana kazi, hivyo ndani ya nyumba ugumu wa maisha unaingia, kula kwa tabu, kuvaa kwa tabu, huwa mke hakimbii kwani ndiyo ahadi ya ‘niko tayari kuishi naye katika tabu na raha’.

KUOLEWA NA KUOA
Wanandoa walioolewa au waliooa siku zote huwa hawavumilii tabu ya aina yoyote ile. Wapo wanawake ambao, mumewe akikosa kipato na hivyo ndani ya nyumba kuwa na uhaba wa chakula tofauti na zamani, huanza vitimbi ili waachike au wafukuzwe.

Wapo wanaodiriki hata kusema; ‘maisha haya mimi siyawezi.’ Kundi la wanawake hawa ni wale waliotaka kuolewa na si kufunga ndoa.

Wapo wanaume ambao akigundua mkewe hapendi ndugu, si msafi, ni mchoyo, hana majibu mazuri kwake, anamuacha. Na anasema; ‘bora nitafute mwanamke mwingine’. Hao ni wale wanaume waliotaka kuoa na si kufunga ndoa.

TAFSIRI YA KUFUNGA NDOA
Kufunga ndoa ni kujiingiza kwenye maisha mengine yasiyopanguliwa njiani. Kuachana katika ndoa hakupo kwa sababu yoyote ile, lakini kwa vile kuna ugumu ndani ya mioyo ya watu ndiyo maana wanaachana lakini tangu mwanzo Mungu alipomuumba  mtu mume na mtu mke hakukuwa na kuachana na katika maandiko anasema anachukia sana kuachana!
Baadhi ya wasomaji wangu waliosoma mada hii wiki iliyopita, walinitumia meseji za kunipongeza, wengine za kuniponda. Meseji zenyewe ni kama hizi:
“Kaka Ndauka unaonekana wewe ni mume bwege, haiwezekani mwanamke anifanyie figisufigisu nyumbani kwangu halafu nimwache atanue eti kwa sababu ya ndoa…aaa wapi!” Ezekiel, Mabibo- Dar.

“Nimependa mada yako ya leo kaka. Wengi tumeingia kwenye ndoa tukiamini kuwa, tabu tunazokwenda kukutana nazo ni za kibinadamu. Lakini kufika tukakuta kuna ngumi, mateke, manenomaneno, tukashindwa.” Kudura, Kusani- Dar.

“Bwana Ndauka mzima? Endelea kutupa mada moto kama hizi. Naunga mkono mada yako ya leo, imesimama.” Mecky, Tabora.

Leave A Reply