The House of Favourite Newspapers

Umuhimu wa mbogamboga mwilini

0

Mbogamboga (vegetables) sehemu yake kubwa ni maji (asilimia 84-96). Kwa upande wa virutubisho vingine, mbogamboga ni chanzo kizuri cha madini ya Phosphorus na Calcium. Vilevile ni chanzo kizuri cha vitamini A na C.

Vitamini C inapatikana zaidi kwenye mbogamboga za majani ambazo zina rangi ya kijani, kama vile mchicha, kisamvu, matembele, majani ya kunde na yale ya maboga na kadhalika. Kwa upande wa vitamini A inapatikana kwa wingi kwenye karoti.

Zaidi ya hayo, baadhi ya mbogamboga zina protini na kabohaidreti (wanga) kwa mfano mapeyasi, maharage na viazi. Nyuzi nyuzi za kilishe (dietary fibres) pia zinapatikana kwa wingi katika mbogamboga hasa mboga za majani.

Vitamini C ni kirutubisho kinachopotea kwa haraka wakati wa upikaji wa mbogamboga. Ili kupunguza tatizo hilo, mbogamboga zipikwe kwa dakika chache, kama vile dakika tano mpaka kumi. Kwa utaratibu huu, maji yachemshwe kwanza. Yaani osha mboga zako vizuri kwa maji safi halafu zitie katika maji yanayochemka. Baada ya dakika hizo tano mpaka kumi zitakuwa zimeiva kwa kiasi ambacho hakitapoteza vitamini C kwa wingi.

Sambamba na hatua hiyo, mbogamboga lazima zipikwe kwenye chombo kilichofunikwa ili vitamini zisiondoke na mvuke. Pia watu wajilazimishe kunywa ule mchuzi (supu) unaopatikana baada ya kupika hizo mbogamboga. Hii ni kwa sababu, mchuzi huo unavitamini nyingi inayotoka kwenye mbogamboga.

Vitamini na madini ni muhimu sana mwilini. Kwa sababu zinasaidia kuupa mwili kinga ya maradhi mbalimbali, na madini kama ya chuma yanahitajika kwa utengenezaji wa damu. Bila damu hakuna binadamu atakayeweza kuishi.

Nyuzinyuzi za kilishe nazo ni muhimu ili chakula kiweze kusagwa vizuri tumboni. Pia zinasaidia kunyonya sumu iliyoko tumboni ambayo inaweza kusababisha ugonjwa wa saratani (kansa). Vilevile nyuzinyuzi zinasaidia mtu kupata choo kikubwa mara kwa mara. Yaani huondoa tatizo la kutopata choo yaani Constipation.

Kwa sababu mbalimbali, hasa umaskini na ujinga, baadhi ya watu hawataki kula mlo wenye nyama na  maharage au  mboga za majani. Kwa mfano nyama na mchicha au maharage na mchicha maana yao ni kuwa, nyama ni kitoweo na mchicha pia ni mboga, kwa hiyo hawawezi kula mboga mbili kwa wakati mmoja ni kujiongezea gharama isiyo ya lazima!
Mtazamo kama huo ni potofu, iachwe kwani una madhara ambayo huwezi kuyaona kwa macho kama yamesababishwa na tabia mbaya ya kula vyakula. Kwa mfano kuzaa watoto wenye akili nzito (wasioelewa jambo kwa haraka) na ulemavu mwingine, au kutoona vizuri.

Leave A Reply