The House of Favourite Newspapers

Unataka Kuwa Bakhresa Mpya Bongo? Hujachelewa

0
Said Salim Bakhresa

 

NIMEKUWA nikitumia muda mwingi kutafiti maelezo kamilifu juu ya namna mabilionea mbalimbali walivyofanikiwa kufika kwenye kilele cha utajiri. Swali langu kwako ni je, ungependa kuwa bilionea kama Bhakhresa au Reginald Mengi? Ni rahisi mno, cha kufanya wewe fuatana nami kila wiki kwenye safu hii.

Ukifuatilia namna baadhi ya mabilionea walivyofanikiwa, utagundua kuwa walipitia kwenye vitu tunavyoviona vidogo au vya kawaida sana ambavyo wala huhitaji kuwa na mtaji mkubwa au mtaji wowote ili kuwa navyo. Ishu hapa ni namna walivyokomaa na mtaji kiduchu au kutokuwa na mtaji kabisa hadi kikaeleweka. Leo kupitia Bakhresa unaweza kupata njia ya wewe kuchomoka;

Nikiri kwamba haikuwa kazi rahisi kupata maelezo ya namna Bilionea Bakhresa alivyofanikiwa na kutajwa kama tajiri namba moja Bongo.

 

Said Salim Bakhresa akisalimiana na Rais Magufuli.

 

MZALIWA WA ZANZIBAR

Taarifa hizo zinaonesha kuwa, Said Salim Awadh Bakhresa alizaliwa mwaka 1949 visiwani Zanzibar. Alisoma elimu ya msingi hadi alipofikia umri wa miaka 14 ambapo aliacha shule kutokana na maisha ya familia kuwa magumu hivyo kujiingiza katika biashara ndogondogo ili aweze kuhudumia familia hasa ndugu zake katika mahitaji kama chakula baada ya baba yake kukabiliwa na madeni.

Katika miaka ya 1960, wakati Tanzania ilipokuwa nchi ya kijamaa na Kenya ikifuata siasa za kibepari, inaelezwa kuwa, Bakhresa alinunua mabaki ya mazao ya baharini kama mifupa na magamba ya viumbe wa baharini na kuyauza huko Mombasa, Kenya.

Kutokana na tofauti ya kifedha iliyokuwapo wakati huo kati ya Tanzania na Kenya, Bhakhresa aliweza kununua ngozi za viatu kutoka Kenya na kuzitumia kushonea viatu hapa Tanzania.

Said Salim Bakhresa akisalimiana na Rais Kikwete.

 

BIASHARA YA MGAHAWA

Badaaye inaelezwa kuwa, alifanya biashara ya viazi, mikate na ice cream.

Katika miaka ya 1970, Bakhresa alifungua na kuendesha biashara ya mgahawa jijini Dar.

Inaelezwa kuwa mgahawa huo aliununua kutoka kwa mgeni wa Kihindi ukiwa na jina la Azam ambalo analitumia kama brand (nembo) ya bidhaa zake kwa sasa.

Katika miaka ya 1990, Bakhresa alianza uwekezaji katika viwanda. Kwa sasa kiasi kikubwa cha mchele, unga na bidhaa nyigine za nafaka zinatoka katika Kampuni ya Bakhresa Group.

Nchi jirani ya Rwanda kwa mfano, inategemea tani 120,000 za unga wa wa ngano kwa mwaka kutoka kwa Bakhresa Group.

Bilionea Bakhresa ndiye Mwenyekiti wa Makampuni ya Bakhresa Group. Ndiye Mtanzania anayemiliki viwanda vingi vinavyozalisha bidhaa za vyakula zinazouzika ndani na nje ya nchi.

Kwa sasa kokote unapokuwa jijini Dar na mikoani, bidhaa za Bakhresa utasikia zikitajwa. Ni wazi kuwa Bakhresa amejijengea jina kubwa kibiashara.

ZAIDI YA TRILIONI 1

Mapato ya Bakhresa kwa mwaka yanatajwa kufikia dola milioni 520 (zaidi ya shilingi trilioni 1) huku akiwa na wafanyakazi zaidi ya 2,000 wenye ajira rasmi.

Bakhresa ni mtu mashuhuri katika harakati za mapinduzi na maendeleo ya viwanda Tanzania Bara na Visiwani.

Katika muda wa miongo mitatu tu ameweza kujenga timu imara ambayo inasimamiwa na wakurugenzi makini.

Bakhresa ana matawi katika nchi sita ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, Zambia na Msumbiji.

Amejikita zaidi katika usindikaji wa vyakula. Ana viwanda vya kusaga unga wa ngano na mahindi, viwanda vya ukoboaji wa mchele, uandaaji wa vyakula kama mikate, chapati, vinywaji kama maji, juisi za matunda, soda na ice cream.

Pia ana kiwanda cha vifungashio vya bidhaa mbalimbali, biashara ya mafuta ya magari na mitambo.

Vilevile ana boti za usafirishaji abiria ambazo hufanya safari zake katika Bahari ya Hindi.

Hali kadhalika, anafanya biashara ya usafirishaji mizigo na anamiliki hoteli za kitalii visiwani Zanzibar.

TIMU YA AZAM

Katika michezo, Bakhresa anamiliki timu ya mpira wa miguu ya Azam Footbal Club ambayo inashiriki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Unapomzungumzia Bakhresa unamzungumzia mtu

 anayesimamia maono yake na kuhakikisha yanatimia.

Ana uzoefu mkubwa katika usimamizi wa biashara, ni mtu anayefanya tafiti juu ya maendeleo ya viwanda na masoko katika kutambua mahitaji ya watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Licha ya kutangaza bidhaa zake kupitia redio na televisheni, anapata fursa ya kujitangaza kupitia timu yake ya mpira wa miguu anayoimiliki hivyo anatangaza bidhaa zake kupitia michezo.

Vilevile anawatumia wachuuzi au machinga katika kutangaza bidhaa zake, mfano ice cream.

Pamoja na mafanikio makubwa aliyonayo bado kuna vikwazo na changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo ili kufikia malengo yake.

Kwa mfano; sera za biashara zisizosimamiwa vizuri katika ushindani wa masoko, gharama za teknolojia katika uzalishaji na kadhalika.

Bakhresa ni mtu anayehamasisha Watanzania wasiogope kujifunza kwa vitendo, kwani wengi huhofia changamoto zinazoweza kusababisha anguko katika biashara, lakini mjasiriamali anapaswa kujiamini katika mawazo yake na kujiwekea mipango madhubuti.

Kwa sasa Bakhresa anaendelea kutanua wigo wa biashara katika kuweza kufikia nchi nyingi zaidi duniani.

Hata hivyo, anaamini kwamba bidhaa zake bado hazijatosheleza soko la ndani.

KWA NINI WEWE USHINDWE?

Pia anatoa ushauri kwa Watanzania, hususan vijana, wajitahidi kufikiri vizuri na kutazama fursa zilizopo nchini kwa kuanzisha miradi mbalimbali ambayo itawainua wao kiuchumi ili hatimaye kuondokana na umaskini unaolikabili taifa letu. Kama Bakhresa ameweza, kwa nini wewe ushindwe? Amka, kimbiza ndoto zako!

MAKALA: Nyemo Chilongani na mtandao

Leave A Reply