The House of Favourite Newspapers

Unatarajia kuoa/kuolewa? hii inakuhusu-3

0

Couple-in-BedNAAM tumekutana tena katika kona yetu hii ya Sindano za Mahaba. Kwa wale wagonjwa niwape pole Mwenyezi Mungu ataonesha njia na kwa wale wazima kama mimi ni jambo la kumshukuru Muumba.

Wiki iliyopita nilielezea vipengele ambavyo ukivifanyia kazi vizuri ni wazi utapata mwenzi ambaye atakupa furaha maishani. Endelea nami…

Mathalani, kuna baadhi ya watu wana viburi au dharau za kuzaliwa! Hata umfanyeje, habadiliki. Unaweza kumuuliza kitu akanyamaza. Ni tabia ya kiburi, lakini kwa sababu amezaliwa akiwa na tabia hiyo, hawezi kuiacha. Sasa hapo lazima ujiulize, utawezana naye?

Utaweza kumvumilia na kiburi chake kwa maisha yenu yote? Huu ni mfano tu msomaji wangu, zipo tabia nyingi za asili, ambazo kwa nafasi yako unaweza kuzichunguza kwa mpenzi wako kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa.

KUWA MKWELI

Ukweli ni silaha, ni haki na siku zote humfanya mtu awe huru. Kama kuna jambo ambalo hujalipenda kwa mpenzi wako, haraka mwambie. Acha kukaa na vitu moyoni. Si utaratibu mzuri.

Hata kama nguo zake hazikufurahishi mwambie; ‘Baby yaani kiukweli ukivaa hizo suruali zako za jeans hupendezi kabisa. Nadhani uanze kuvaa suruali za vitambaa.’

Hapo utakuwa umemwambia ukweli wako, kukubaliana na wewe au kukataa kutatokana na mapenzi yenu wewe na yeye. Kama anakupenda atakusikiliza.

UTARATIBU WA KAZI

Suala la kazi kwa baadhi ya wanandoa huwa ni tatizo. Utakuta mwanaume amemkuta binti wa watu anafanya kazi, wamependana na kufunga ndoa. Ghafla anamwambia mwenzake aache kazi!

Ndoa nyingi hasa changa huingia kwenye mgogoro huu. Kwangu mimi, wanandoa wote kufanya kazi ni bora zaidi, maana ile maana ya usaidizi wa mwanamke inakuwa imekamilika. Kwa maisha ya sasa mama kukaa nyumbani siyo dili tena.

Hata hivyo, ili kuepusha matatizo suala hili ni vyema mkajadiliana mapema. Kaa na mwenzako, mwulize; ‘Lakini baby, vipi kuhusu kazi baada ya kufunga ndoa?’

Anzisha huu mjadala na mwisho muwe na majibu yenye usawa. Mkubaliane kwa pamoja. Vijana wa mtaani wanasema, ‘kiroho safi’.

VIPI NDUGU ZAKE?

Kama ni kweli una matarajio mazuri kutoka kwa mwenzako, kipengele hiki ni muhimu kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa.

Lazima uijue vizuri familia yake. Anatoka katika familia ya namna gani? Kabila gani? Ukiachana na hilo, hapa lazima ufahamiane na ndugu zake, japo kidogo na upate muda wa kuwazoea.

Kuna familia nyingine ni wakorofi, kama ukiolewa huko ni tabu tupu. Pengine ukiona katika familia yao, labda wana tabia ya udokozi…si ajabu ukaibiwa hata wewe.

Kweli umempenda na unataka kuishi naye, lakini utaratibu mbaya wa ndugu zake ni kielelezo cha matarajio ya maisha yenu ya ndoa. Kuwa makini.

UNAIJUA AFYA YAKE?

Baadhi ya watu kwa bahati mbaya wana matatizo ya kiafya ya kudumu. Utakuta huyu ana udhaifu wa kusumbuliwa na shinikizo la damu, mwingine vidonda vya tumbo, kifafa n.k.

Vipo vipengele vingi, vilivyobakia ambavyo ni mila na desturi, imani za dini na mwisho ni kuwa na nia moja kwa kila mnachokipanga.

Naomba tuishie hapa kwa mada yetu hii.

Tukutane tena wiki ijayo kwa mada mpya na nzuri zaidi.

Leave A Reply