The House of Favourite Newspapers

Unending Love-44

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini. Moyo wake unabaki na majeraha makubwa yasiyopona na kujikuta akipata matatizo ya figo yake moja iliyosalia.

Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ghafla Anna alishtuka kama mtu aliyetoka ndotoni, harakaharaka akajitoa kwenye mikono ya William na kusimama, akatembea hatua kadhaa na kusimama pembeni yake huku akionesha kukerwa na kilichotokea.
“Kwa nini unanifanyia hivi William? Si tulikubaliana kuwa marafiki wa kawaida tu?”

“Ooh! Nisamehe Anna, ni shetani tu alinipitia,” alisema William huku naye akiinuka na kumsogelea Anna lakini msichana huyo hakutaka mazungumzo yoyote, harakaharaka akaanza kutembea kuondoka eneo hilo kuelekea kwenye hosteli aliyokuwa anaishi.

William alibaki amesimama palepale, akiwa amepigwa na butwaa. Kiukweli alikuwa anashindwa kumuelewa msichana huyo mrembo ana matatizo gani ndani ya kichwa chake, hata hivyo kwa upande mwingine alishaanza kuona dalili za ushindi zimeanza kunukia kwani kwa mara ya kwanza alikuwa amefanikiwa kumkumbatia msichana huyo na kumbusu kwenye midomo yake mizuri.

William aliendelea kumsindikiza kwa macho mpaka msichana huyo alipopotea kwenye upeo wa macho yake, akaachia tabasamu pana na kurudi kukaa palepale walipokuwa wamekaa awali. Akawa anaendelea kuchuma maua na kuyakatakata kwa mikono yake huku akiendelea kumfikiria Anna.

Japokuwa wasichana wengi walikuwa wakimpapatikia karibu kila siku, tena wengine wakiwa ni kutoka mataifa ya Ulaya, moyo wa William ulionesha kumuangukia msichana huyo. Akajiapiza kufanya kila kinachowezekana mpaka ampate na kuwa mpenzi wake.

“Na hivi anavyonisumbua akikubali kuwa wangu lazima nitangaze ndoa kabisa,” aliwaza William na baada ya takribani nusu saa, aliinuka na kuanza kutembea kimadaha kama kawaida yake kuelekea kwenye uwanja wa mpira wa kikapu, mchezo aliokuwa anapenda sana kuucheza. Siku hiyo ikapita.
***
Hatimaye Jafet aliwasili kwenye Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS), baada ya taratibu za usajili kukamilika, akapelekwa kwenye hosteli iliyokuwa ndani ya eneo hilohilo la chuo na kukabidhiwa chumba ambacho alitakiwa kuishi na wanachuo wenzake.

Ile ndoto yake ya siku nyingi ya kusomea udaktari ikawa imetimia. Akaanza rasmi masomo ya shahada ya udaktari (Bachelor Degree in Medicine) huku akijitahidi kuelekeza nguvu zake zote huko badala ya kuendelea kumuwaza Anna.
Kwa kuwa safari hii alikuwa karibu na huduma za afya za uhakika, aliendelea kufanyiwa vipimo vya hapa na pale vya figo yake na kila tatizo lilipokuwa likiibuka, lilikuwa likishughulikiwa haraka. Afya yake ikazidi kuimarika na kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo alivyokuwa akizidi kukazania masomo.

Taratibu yale mawazo juu ya Anna yakaanza kupungua ndani ya kichwa chake, ukichanganya na uchangamfu wake, ndani ya muda mfupi tayari alishapata marafiki wa jinsia zote chuoni hapo, jina lake likaanza kuwa maarufu.
Kingine kilichomuongezea Jafet umaarufu chuoni hapo, ni uwezo wake wa kuelewa mambo haraka darasani. Japokuwa masomo ya udaktari yalikuwa yakiaminika kuwa miongoni mwa masomo magumu, hali ilikuwa tofauti kwa Jafet.

Kila alichofundishwa alikielewa kwa haraka na kama ilivyokuwa katika ngazi zote za chini alizosomea, kila walipopewa majaribio au kazi za makundi, achilia mbali mitihani ya hapa na pale, alikuwa akishika nafasi za juu na kuwa miongoni mwa wanachuo wanaoogopwa sana chuoni hapo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kiakili.

Kutokana na uwezo mkubwa wa kiakili, ucheshi, upole, nidhamu na busara alizokuwa nazo, wanachuo wengi wa kike walionesha kuvutiwa naye kimapenzi na kuanza kujiweka karibu, kila mmoja akitamani kijana huyo amtongoze lakini kwa Jafet wala hakuwa na mawazo hayo.

Wote aliwaona kama rafiki zake wa kawaida na hata baadhi yao walipokuwa wakimvukia mipaka, alikuwa akiwabadilikia na kuwa mkali kwani walikuwa wakimtonesha kidonda ambacho bado kilikuwa hakijapona ndani ya moyo wake.

Kitendo alichofanyiwa na Anna kiliufanya moyo wake kufa ganzi na ndani ya nafsi yake alijiapiza kutompenda mwanamke yeyote. Huo ndiyo ulikuwa msimamo wake na alijiapiza kuusimamia kwa kadiri ya uwezo wake wote.
Mara chachechache alizokuwa akimkumbuka Anna, alikuwa akienda kujifungia ndani na kulia kwa muda mrefu.

Hata hivyo, kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, ndivyo hali hiyo ilivyokuwa inazidi kupungua. Mpaka muhula wa pili unaisha, Jafet alikuwa akishika nafasi ya kwanza kwa matokeo ya jumla, jina lake likazidi kuwa maarufu chuoni hapo.

Baada ya kumaliza mitihani, Jafet alifunga safari kurejea kijijini kwao, Rwamgasa kwani wazazi wake walikuwa wakimsisitiza mara kwa mara arudi ili wajue maendeleo ya afya yake. Baada ya safari ndefu ya kutoka jijini Dar es Salaam, aliwasili kijijini Rwamgasa ambako alipokelewa kwa shangwe na wazazi wake pamoja na ndugu zake wengine.

Kwa kuwa tayari yule mpangaji waliyekuwa wamempangisha kwenye nyumba yao kwa ajili ya kugharamia matibabu ya Jafet mkataba wake ulishaisha, walikuwa tayari wamerejea kwenye nyumba hiyo mpya.
“Utakaa na sisi kwa siku ngapi mwanangu?”

“Nitakaa wiki moja tu, baada ya hapo nina safari ya kwenda Mwanza kufuatilia vyeti vyangu vya sekondari kwenye shule niliyosoma kisha nitaondokea hukohuko kwenda Dar es Salaam,” alisema Jafet wakati wakizungumza na mama yake. Likizo hiyo ilikuwa nzuri sana kwa Jafet kwani alipata nafasi ya kukaa na familia yake.

Wiki moja baadaye, kama alivyokuwa ameahidi, Jafet alifunga safari mpaka jijini Mwanza, kufuata vyeti vyake vya elimu ya kidato cha tano na sita. Jafet aliposhuka kwenye stendi ya mabasi jijini Mwanza, alianza kutafuta usafiri wa kumpeleka shuleni kwake lakini ghafla, alisikia jina lake likiitwa kwa nguvu.
“Jafet! Jafet! Jafetiii!”

Harakaharaka aligeuka kutazama sauti ile ilikokuwa inatokea.
Je, nini kitafuatia? Anayemuita Jafet ni nani? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply