The House of Favourite Newspapers

Unending Love-52

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.

Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa karibu na sasa William ameanza kumshawishi Anna wafanye mapenzi.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…J

afet hakutaka kufikikiria mapenzi tena, kitu kilichokuwa akilini mwake kwa wakati huo ni kusoma tu. Alitoka katika familia masikini, wazazi wake walipata tabu sana kijijini, ili wazazi wake hao wawe na maisha mazuri kama wengine, ilikuwa ni lazima asome sana na mwisho wa siku kupata kazi yenye mshahara mzuri na kuwasaidia wazazi wake.

Japokuwa kulikuwa na wasichana waliovutiwa naye lakini Jafet hakutaka kuelewa kabisa, walimfuata na kumwambia ukweli kwamba walimpenda lakini kwa Jafet, hakutaka kufikiria mapenzi, alikwishawahi kupenda, tena alipenda sana lakini mwisho wa siku alikuja kulia, alitamani hata kujiua.

“Jafet…”

“Unasemaje?”

“Kwa hiyo ndiyo hutaki kunielewa?”

“Sikiliza Victoria! Umekuja kufanya nini hapa chuo?”

“Kusoma!”

“Basi soma, mambo ya mapenzi achana nayo.”

“Kwa nini lakini? Au ushawahi kuumizwa?” aliuliza msichana huyo swali lililomfanya Jafet kuanza kutokwa na machozi.

“Vick….naomba uondoke,” alisema Jafet huku akionekana kukasirika. Hakutaka kabisa kuingia kwenye mapenzi, kwa kile alichofanyiwa na Anna, kwake kilikuwa fundisho.

****

Ilikuwa si sawa na kuonjeshwa asali, sasa alifakamia mzinga mzima. Anna hakupinga tena hakumzuia William kufanya kile alichotaka kukifanya usiku huo. Kitandani pale, alijikuta akimkaribisha mwanaume katika miguu yake na kulichofuata ni sauti za mahaba usiku kucha.

Mapenzi yakamteka, akawa ahambiwi wala hasikii kwa mwanaume huyo. Hawakuacha kula raha, kila ilipofika asubuhi ilikuwa ni lazima kwenda baharini na kuanza kuzunguka na boti mpaka pale walipoamua kurudi nyumbani.

Siku ziliendelea kukatika, mapenzi yao yakaendelea kuchangamka, marafiki zake William wakatambulishwa Anna, walimfurahia kwa kuwa alikuwa msichana mzuri, kwa kumwangalia tu, alionekana kuwa na mvuto wa kuwa na mtu kama William.

Katika kila kitu kilichoendelea, Anna hakumkumbuka kabisa Jafet, alisahau kama kulikuwa na mwanaume mwenye jina hilo ambaye alikutana naye kipindi cha nyuma, alisahau kabisa kama kuna siku alipata tatizo la figo na hivyo mwanaume huyo kutoa figo yake na kumpatia.

Vyote hivyo alivisahau kabisa na ndiyo maana leo hii aliamua kuwa na mwanaume mwingine kwa kisingizio kwamba alimpenda kwa mapenzi yote na pia alikuwa tayari kuona akiwa mume wake wa ndoa.

Pombe haikuwa chungu kwa Anna kama siku za nyuma, kila siku akawa mtu wa kunywa na kutoka kwenda kwenye kumbi mbalimbali na kucheza muziki. Maisha ya starehe yalimteka na akawa mnywaji mzuri wa pombe kitu ambacho kilimshangaza hata William mwenyewe.

“Leo wapi?”

“Wewe niambie unataka kwenda wapi,” alisema William.

“Popote pale, utakapopapenda, nitapapenda pia,” alisema Anna.

“Basi twende Leaders Club, Twanga Pepeta wanapiga pale kwenye uzinduzi wa pombe ya Saint Anna,” alisema William.

“Basi ngoja nijiandae mpenzi.”

“Sawa. Nakusubiri!”

Maisha ya starehe yaliendelea kumteka kila siku, Anna akachanganyikiwa, hakuwa mtu wa kulala usiku, kila siku ilikuwa ni lazima amwambie William kwamba alitaka kwenda kwenye klabu yoyote kwa ajili ya kucheza muziki, na kama ikishindikana basi wakae nyumbani wakinywa pombe na kufanya mapenzi usiku kucha.

Baada ya wiki mbili, Anna akaanza kujisikia tofauti, akaanza kujisikia uchovu mwingi mwilini mwake, kila alipokuwa, akawa na hamu ya kulala, hakutaka kufanya kazi na hata ile mizunguko ya mara kwa mara na William ikaanza kupungua.

Hali hiyo ilimshangaza, hakuwahi kujisikia hivyo kabla, akawa na hofu moyoni mwake, kuna kipindi alihisi kwamba inawezekana kwamba alikuwa na mimba lakini baadaye wazo hilo likaondoka kichwani mwake na kuona kwamba ni tatizo la kawaida, hivyo hakutakiwa kufikiria hilo.

Akakosa amani, akakosa furaha moyoni mwake, unyonge ukamwingia, kila alipokaa na kufikiria tatizo lilikuwa nini, alishindwa kupata jibu kabisa.

“Vipi tena?” aliuliza William.

“Poa,” alijibu Anna kwa kifupi.

“Haupo sawa Anna, tatizo nini?” aliuliza William.

“Hakuna tatizo.”

“Kweli?”

“Hakika.”

Leave A Reply