The House of Favourite Newspapers

Unending Love 64

0

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa lakini matatizo mengine ya figo yanazuka upya na kusababisha asafirishwe mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet atafutwe mahali popote alipo na kupelekwa hospitalini hapo. Kazi hiyo inafanyika na hatimaye Jafet anaenda kuonana na Anna hospitali. Baba yake Anna anambembeleza kijana huyo ajifanye amemsamehe Anna na kurudiana naye ili kumfariji kwenye kipindi kigumu alichokuwa anapitia, jambo linaloonekana kumkwaza sana Suleikha.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Jafet humalizi tu? Nimechoka kusubiri nje,” Suleikha alisema huku akisukuma mlango wa wodi na kuingia ndani, akapigwa na butwaa kwa mkao aliowakuta wawili hao wamekaa.

“Jafeeet!” aliita Suleikha kwa sauti kubwa akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona.
“Suleikha! Please there is an explanation,” (Suleikha, tafadhali kuna ufafanuzi inatakiwa nikupe)

“I don’t need any explanation, I’ve seen it with my naked eyes,” (sihitaji ufafanuzi wa chochote, nimeshuhudia mwenyewe kwa macho yangu) alisema msichana huyo huku machozi yakianza kumchuruzika kwa kasi na kulowanisha uso wake. Akageuka na kuanza kuondoka, jambo lililomfanya Jafet ainuke pale alipokuwa amekaa na kuanza kumfuata nyuma kwa kasi.

“Suleikha! Suleikha! Hebu punguza hasira mpenzi wangu, kwani nini tatizo?”
“Kwani wewe huoni kama kuna tatizo si ndiyo? Bado unampenda Anna, inaonesha bado mnapendana lakini nashukuru sana kwa kuutesa moyo wangu kiasi hiki,” alisema Suleikha huku akilia kwa uchungu, Jafet akawa anaendelea kumkimbilia kwa nyuma huku akimbembeleza.

Wazazi wa Anna waliokuwa wamekaa nje ya wodi aliyokuwa amelazwa binti yao, walishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea, wakajikuta wakitikisa vichwa vyao kwa masikitiko kwa sababu walijua wao ndiyo chanzo cha matatizo yote hayo.

“Suleikha, nakuomba unisikilize mpenzi wangu,” alisema Jafet lakini msichana huyo hakutaka kusikia la muadhini wala mchota maji. Akaendelea kutembea harakaharaka mpaka alipotoka kwenye geti la hospitali hiyo, akawa anaelekea kwenye hosteli aliyokuwa anaishi.

Jafet aliendelea kumfuata nyumanyuma mpaka alipofika chumbani kwake, akataka kujifungia ndani peke yake lakini Jafet alimuwahi na kuingia, akaendelea kumbembeleza huku akimtaka ampe nafasi ya kumsikiliza.

“Utaniambia nini nikuelewe Jafet? Unajisumbua tu.”
“Siyo hivyo mpenzi wangu, ukinipa nafasi ya kunisikiliza hata kwa muda mfupi tu utaelewa nataka kukwambia nini,” alisema Jafet kwa sauti ya kubembeleza, Suleikha akatulia na kuanza kumsikiliza.

“Sina mapenzi tena na Anna na kamwe haiwezi kutokea nikampenda tena lakini wazazi wake wameniomba niwasaidie kumtuliza Anna, ndiyo maana unaona baba yake alinifuata chuoni na hata pale hospitalini tulizungumza kwa muda mrefu sana ama unakumbuka,” alisema Jafet na kuendelea kumfafanulia Suleikha kila kitu.

Kutokana na uwezo wa kipekee aliokuwa amejaliwa Jafet, alifanikiwa kumtuliza msichana huyo, akaendelea kumpa maneno matamu ambayo yalimtuliza kabisa Suleikha, akaacha kulia na kujifuta machozi.

“Kwa hiyo unataka kusema huna hisia naye kweli?”
“Sina hisia kabisa, nimeshakuchagua wewe Suleikha na hakuna kitakachonirudisha nyuma, amini nakupenda Suleikha na kamwe sitaweza kukuumiza, mwenyewe unajua umenitoa kwenye hali gani mpaka leo kila mtu ananisifia, hii yote ni kwa sababu yako mpenzi,” alisema Jafet na kumbusu Suleikha kwenye shavu lake la kushoto, kitendo kilichomfanya msichana huyo mrembo atabasamu. Jafet akaendelea kumueleza jinsi wanavyotakiwa kumsaidia Anna kwa pamoja.

Baada ya maelezo marefu, hatimaye Suleikha alimuelewa Jafet, wakakumbatiana na kubusiana kimahaba kisha wakatoka na kurudi hospitalini kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Anna. Kabla ya kwenda, walimnunulia zawadi ndogondogo yakiwemo matunda na juisi, Suleikha akabeba kifurushi hicho kisha wakaingia getini.

Kwa kuwa walinzi walikuwa wakiwafahamu kama wanafunzi wa udaktari, hakukuwa na mtu yeyote wa kuwahoji, wakaenda mpaka wodini na kuwakuta wazazi wa Anna wakiwa wamemzunguka binti yao aliyeonekana kuwa na huzuni kubwa.

“Jafet! Umerudi? Ooh! Ahsante kwa kuja,” alisema Anna huku akitanua mikono yake kama ishara ya kutaka kumkumbatia Jafet, bila hiyana naye akamsogelea na kumkumbatia huku Suleikha akishuhudia. Safari hii hakuwa tena na wivu kwa sababu tayari alikuwa anajua kinachoendelea.

Uwepo wa Jafet ulikuwa ukimbadilisha mno Anna, jambo ambalo hata Suleikha mwenyewe aliligundua. Baada ya kukaa muda mrefu na Anna, wakipiga stori za hapa na pale, hatimaye waliaga na kuondoka na kumuacha Anna akiwa ameridhika kwa kiasi kikubwa.

Kesho yake asubuhi, madaktari walipopita kuwatazama wagonjwa, mjadala mkubwa ulizuka walipofika kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Anna kwa sababu ilionekana kwa jinsi hali yake ilivyokuwa, hakukuwa na uwezekano wa kutibiwa na kupona akiwa nchini Tanzania.

“Inatakiwa arudishwe India kwenye hospitali aliyofanyiwa upasuaji wa kumbadilishia figo, wao ndiyo wanaoweza kujua nini cha kufanya,” alisema daktari mmoja aliyeonekana kuwa na mamlaka kuliko wenzake.

Baada ya maelezo hayo, wazazi wake walikubaliana na kila kitu kwani walichokuwa wanakitaka ni binti yao kupona. Bila kupoteza muda, maandalizi ya kurudi nchini India yakaanza ambapo suala lililoanza kuwasumbua ni baada ya Anna kuanza kushinikiza kwamba anataka kusafiri na Jafet.

“Mwenzio yupo chuoni na kama sikosei amewahi kusema kwamba wanakaribia kufanya mitihani, inabidi tutangulie halafu yeye atafuata,” alisema baba yake Anna, kauli iliyoungwa mkono na mkewe, Anna akakubali kwa shingo upande.

Siku tatu baadaye, Anna na wazazi wake wote wawili, walikuwa ndani ya ndege kwa safari ya kuelekea nchini India kwa matibabu zaidi ya binti yao ambaye kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo afya yake ilivyokuwa inazidi kudhoofika.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply