The House of Favourite Newspapers

Unending Love -69

0

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet akaletwe. Baadaye, baba yake Jafet anafunga safari mpaka Tanzania na kumchukua Jafet, anafunga naye safari mpaka nchini India na hatimaye Jafet na Anna wanakutanishwa tena hospitalini hapo.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Jafet!”

“Naam!”

“Kwanza naomba nianze kwa kukushukuru kukubali kuja kuniona. Najua kuna umbali mrefu kutoka nyumbani Tanzania mpaka huku ugenini.

“Najua ulikuwa na majukumu mengi, isitoshe sasa hivi nimeambiwa mnakaribia kufanya mitihani lakini umeweza kuacha kila kitu kwa ajili yangu, hata kama mwenyewe unakataa najua kwamba bado unanipenda ndiyo maana umeweza kufanya yote haya,” alisema Anna kwa sauti ya upole huku akimtazama Jafet.

“Nataka kukwambia jambo moja Jafet. Tangu nilipotenganishwa na wewe, maisha yamekuwa magumu sana kwa upande wangu, kila kitu kinapoteza mwelekeo, ndoto zote zimefutika, malengo yote yamevurugika na mwisho nimebaki kama maiti inayotembea. Sioni tena sababu ya kuendelea kuishi,” alisema Anna na alipofikia hapo, alishindwa kuendelea kumtazama Jafet, akajiinamia huku machozi yakimtoka kwa wingi.

“Huna haja ya kulia Anna, tafadhali naomba ujikaze uendelee kunieleza kila kitu, zungumza na mimi jinsi unavyojisikia ndani ya moyo wako na mimi nitakwambia ninavyojisikia,” alisema Jafet kwa sauti iliyotulia kabisa.

“Uamuzi wa mwisho niliofikia, nimeona siwezi kuendelea kuteseka hapa duniani wakati maisha yangu yameshapoteza mwelekeo. Nimeamua kuyakatisha maisha yangu,” alisema Anna na kuendelea kumwaga machozi kwa wingi.

“Whaaat!?” (Niniii?)

“Ni bora nife Jafet, sioni sababu yoyote ya kuendelea kuishi. Nimeshapoteza kila nilichokuwa nacho, ni bora nife,” alisema Anna huku akimkumbatia Jafet, machozi yakiendelea kumtoka kwa wingi. Ilibidi Jafet naye amkumbatie kwa hisia, akawa anampigapiga mgongoni kama ishara ya kumbembeleza.

Japokuwa ni kweli msichana huyo alikuwa ameuvunja sana moyo wake, Jafet alijisikia vibaya sana ndani ya nafsi yake kwa jinsi Anna alivyokuwa anapitia kipindi kigumu. Wakaendelea kukumbatiana kwa muda mrefu huku kumbukumbu za mambo mengi mazuri waliyowahi kuyafanya pamoja zikipita ndani ya kichwa cha Jafet.

“Anna!”

“Abee!”

“Hakuna sababu yoyote ya kuyakatisha maisha yako mpenzi wangu.”

“Eeh! Umeniitaje?”

“Mpenzi wangu.”

“Wewe siyo wangu tena Jafet, najisikia vibaya sana kukubaliana na ukweli kwamba tayari unaye mwanamke mwingine anayekupenda pengine kuliko hata mimi.”

“Huna haja ya kujisikia vibaya, wewe unanijua vizuri pengine kuliko mtu yeyote. Mimi pia nakujua vizuri tangu ukiwa msichana mdogo. Amini kwamba siwezi kukuacha ukaangamia wakati uwezo wa kukusaidia ninao.”

“Utanisaidiaje Jafet? Huna cha kunisaidia, kama ni makosa mimi na wazazi wangu ndiyo tulioyasababisha, acha dunia iniadhibu,” alisema Anna huku akiendelea kulia, safari hii akamvutia Jafet kwenye kifua chake na kusababisha kila mmoja awe anasikia mapigo ya moyo ya mwenzake.

“Can you give me a last kiss please!” (Unaweza kunipa busu la mwisho tafadhali)

“I can kiss you a million time but not a last kiss…” (Naweza kukubusu hata mara milioni moja lakini siyo busu la mwisho) alisema Jafet lakini kabla hajamalizia kauli hiyo, Anna alimbusu kwa hisia nzito kisha wakagusanisha ndimi zao.

Hakuna aliyejali kwamba walikuwa wamekaa hadharani na kuwa uwezekano mkubwa wazazi wa Anna wakawa wanawatazama. Waliendelea kugandana kwa dakika kadhaa, kila mmoja akionesha kuzama kwenye hisia nzito za kimapenzi.

Japokuwa Jafet tayari alikuwa na uhusiano na msichana mwingine, Samantha, hali aliyokuwa anajisikia akiwa na Samantha ilikuwa tofauti kabisa na alivyokuwa anajisikia muda huo akiwa na Anna.

“Before i die, would you please do me a favour!” (kabla sijafa, unaweza kunisaidia kitu tafadhali?)

“Hey! Stop that nonsense! You are not going to die soon as you wish, i will be by your side to support and protect you.” (Hey! Hebu acha mambo yako yasiyo na maana! Hutakufa mapema kama unavyofikiria, nitakuwa pembeni yako kukusaidia na kukulinda).

“Unasema kweli Jafet? Kwani umenisamehe?”

“Nilishakusamehe Anna ndiyo maana nipo na wewe. Tafadhali naomba uniamini,” alisema Jafet kwa sauti ya upole, kauli ambayo iliufanya moyo wa Anna ulipuke kwa furaha kubwa. Hakuna kitu kilichokuwa kinamuumiza moyo wake kama kulikosa penzi la Jafet.

Kauli hiyo ikamfanya amkumbatie tena Jafet na kumbusu kwa hisia nzito. Ndani ya muda mfupi tu waliokaa pamoja, Anna alionesha mabadiliko makubwa ambayo yaliwashangaza wazazi wake mpaka madaktari wa Hospitali ya Apollo alikokuwa amelazwa.

Baada ya kuzungumza kwa kirefu, Anna alimuomba Jafet wakanyooshe miguu pamoja kwenye bustani nzuri za maua zilizokuwa hospitalini hapo. Anna ambaye saa chache zilizopita alikuwa na hali mbaya kiasi cha kuanza kujitabiria kifo chake mwenyewe, sasa alikuwa amebadilika kabisa.

Uso wake ambao kwa muda mrefu ulikuwa umemezwa na simanzi na huzuni nzito vilivyosababishwa na kumkosa Jafet na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua, sasa ulibadilika na kuanza kuonesha matumaini makubwa, tabasamu pana likianza kuchanua.

Taratibu wawili hao wakawa wanatembea kwenye bustani za maua, wakipiga stori za hapa na pale na kukumbushana mambo waliyowahi kuyafanya pamoja siku za nyuma, furaha kubwa ikatawala kwenye mioyo ya wote wawili.

“Unaona mwanao alivyochangamka ghafla?”

“Mh! Yaani huyu Jafet sijui anampa nini maskini! Huwezi kuamini kama ndiyo yule Anna wa saa kadhaa zilizopita. Nimeamini wanapendana sana lakini makosa niliyoyafanya mimi ndiyo yametufikisha hapa tulipo,” alisema mama yake Anna wakati wakiwatazama Jafet na Anna waliokuwa wakipiga stori na kufurahi pamoja.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave A Reply