The House of Favourite Newspapers

CUF, CCM kaeni tena na tena

0
ZIFF chief guest, 1st vice president, Maalim Seif Sharif at ZIFF 2013
Na Mwandishi Wetu, Risasi

DAR ES  SALAAM. Siku mbili baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza msimamo wa Chama cha Wananchi (Cuf) wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio, wananchi wa kada mbalimbali wametaka viongozi wa chama hicho na wale wa Chama Cha mapinduzi (CCM), kukaa tena chini ili kulinusuru taifa.

Wakizungumza mara baada ya hotuba ndefu ya Maalim Seif juzi jijini Dar es Salaam, watu hao walisema endapo kila mmoja atashikilia msimamo wake, ipo hatari kubwa kwa taifa, kuliko faida itakayopatikana miongoni mwa viongozi.

“Suala hapa siyo masilahi binafsi ya Maalim Seif wala Dk. Shein (Mohamed, Rais wa Zanzibar), bali tunaangalia ustawi wa taifa, tunawasihi warejee tena mezani kwa mazungumzo zaidi. Hakuna kinachoshindikana, tunao viongozi wetu wastaafu wenye busara zao, hawa watumike ili jambo hili limalizike kwa amani,” alisema Jamal Sith, mkazi wa Kigamboni.

Kwa upande wake, mkazi wa Kariakoo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Zainab, alisema taifa limepata sifa kubwa nje ya nchi kwa sababu ya amani, hivyo busara ya hali ya juu inapaswa kutumiwa na viongozi wa vyama vyote ili kuhakikisha mgogoro wa Zanzibar unamalizika kwa amani.

Juzi Jumatatu, Cuf kupitia Maalim Seif, ilitangaza kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) Jecha Salum Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kwa kile alichodai kuwepo kwa dosari.

Leave A Reply