The House of Favourite Newspapers

Unending Love (Penzi lisiloisha)-82

2

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.
Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa msichana huyo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.

Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India.
Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Wanafunga safari ya kurejea Tanzania na hatimaye wanawasili jijini Mwanza ambapo mjadala mkubwa unaendelea kuhusu hatima ya wawili hao wanaoonesha kupendana kwa dhati. Wazazi wa Anna wanafikia muafaka wa kuwatafutia wote wawili chuo kingine nchini Marekani, na hatimaye wanaelekea kijijini Rwamgasa kwa wazazi wa Jafet ili kuwaeleza walichoamua.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Baada ya usiku wa kipekee kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa wazazi wa Jafet, hatimaye watu wote walilala, kila mmoja akiwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake mpaka asubuhi ya siku iliyofuatia. Bila kupoteza muda, maandalizi ya kurejea jijini Mwanza yakaanza kufanyika. Wazazi wa Jafet waliridhia kwa mioyo yao yote kwamba mtoto wao apelekwe kusoma Marekani pamoja na Anna, wakawapa baraka zote na kuwaombea kwa Mungu kusitokee tena vikwazo vinavyoweza kusababisha matatizo kati yao.

“Baba yako anachekesha sana, hasa akiwa amelewa,” alisema baba yake Anna wakati safari ya kuelekea jijini Mwanza ikiwa imeanza. Jafet hakuwa na cha kujibu zaidi ya kucheka kwani wao walishamzoea baba yao huyo ambaye siku nyingine akilewa alikuwa akibadilika na kuwa mbogo wakati siku nyingine alikuwa akifurahisha sana.

Usiku uliopita, mzee huyo alikuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake, jambo lililomfanya awachekeshe sana majirani na wageni waliofika nyumbani kwake kwenye tafrija ndogo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na wazazi wa Anna.

“Ukinioa nitataka tuwe tunakuja mara kwa mara nyumbani kwenu ili baba mkwe wangu anichekeshe,” alisema Anna, kauli iliyowafanya wazazi wake wagune na kutazamana.
Mara kwa mara Anna alikuwa akizungumzia masuala ya kuoana na Jafet, tena bila hofu wala kujali kwamba wazazi wake walikuwepo. Penzi la Jafet lilimfanya awe kama mwendawazimu.

Safari iliendelea huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea ndani ya gari. Kwa jinsi wazazi wa Anna walivyokuwa wakimchukulia Jafet, ungeweza kudhani naye ni mtoto wao wa kumzaa kwa sababu walikuwa wakimpenda pengine kuliko kipindi chote maishani mwao na wakawa wanatamani aendelee kuwa karibu na Anna siku zote, waliona binti yao anakuwa na afya njema zaidi akiwa karibu naye.

Baada ya safari ndefu hatimaye waliwasili jijini Mwanza na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye nyumba ya kifahari ya akina Anna, iliyokuwa kwenye mtaa wa watu wenye uwezo mkubwa kifedha jijini humo, Capri Point.

Kutokana na uchovu aliokuwa nao kila mmoja, walipofika kila mmoja alienda kuoga, Jafet akapelekwa kwenye chumba cha wageni na Anna chumbani kwake kwa ajili ya mapumziko. Walikuja kujumuika tena pamoja wakati wa chakula cha usiku. Baada ya kula pamoja kama familia, mazungumzo yalianza.
Baba yake Anna aliwaeleza kwamba ameshawasiliana na rafiki yake waliyesoma pamoja anayeishi nchini Marekani na kwamba alikuwa akiendelea na kazi ya kuwatafutia chuo kizuri ambacho kitakidhi vigezo walivyokuwa wanavihitaji.

“Nafikiri mpaka kesho jioni tayari majibu yatakuwa yameshapatikana kwa hiyo kama ni maandalizi yaanze kufanywa usiku huuhuu, mmekaa muda mrefu bila kwenda chuo, tena kama wewe Anna naona utakuwa umeshasahau kila kitu ulichosoma,” alisema baba yake Anna na kusababisha wote waangue vicheko.

Ilibidi Jafet naye awaeleze kwamba ni lazima arudi mpaka chuoni kwao, Muhimbili jijini Dar es Salaam ili akafuatilie vyeti vyake vya uhamisho kwa sababu hakutaka kwenda kuanza upya anakoenda kuhamia.

“Na mimi nataka kwenda na Jafet,” alidakia Anna na kusababisha mjadala mwingine. Wazazi wake walikuwa na hofu kubwa ya kumruhusu Jafet aongozane na Anna mpaka chuoni kwao kwa sababu walikuwa wanajua kwamba tayari kijana huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana mwingine waliyekuwa wanasoma naye chuo kimoja, Suleikha, jambo ambalo lingeweza kusababisha hali ya sintofahamu kati yao.

“Basi ili kumaliza utata itabidi twende pamoja na mimi ndiyo nitakayesimamia kila kitu kuhusu uhamisho wake Jafet, au unaonaje?” alisema baba yake Anna, wazo ambalo liliungwa mkono na kila mmoja.

Hakukuwa na muda wa kupoteza, kesho yake ilibidi baba yake Anna asafiri na Jafet pamoja na binti yake mpaka jijini Dar es Salaam kwa ndege, muda mwingi wawili hao wakiwa wamegandana kama ruba. Ili kuzuia hali ya sintofahamu, ilibidi wachukue chumba hotelini kisha baada ya hapo Jafet akaongozana na baba yake Anna mpaka chuoni hapo, wakimuacha Anna hotelini.

Walipofika chuoni hapo, walienda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya mlezi mkuu wa wanachuo (Dean of Students) ambako baba yake Anna ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkubwa. Akamueleza mlezi huyo kwamba walifuatilia nyaraka za uhamisho za Jafet kwenda kusoma nje ya nchi.

Mlezi huyo aliwaelekeza sehemu zote muhimu za kupita ili kukamilisha walichokuwa wanakitaka. Jafet akawa anajitahidi kufanya kila kitu kwa usiri mkubwa akikwepa kuonekana na Suleikha kwa sababu hakuwa na majibu ya kumpa na kumfanya amuelewe.
Ilichoona kinafaa, ilikuwa ni kumuandikia ujumbe mzito.
“Mpendwa Suleikha!

“Ni mimi Jafet! Nimerejea kutoka India lakini habari mbaya kwako ni kwamba nahama chuo, naenda kusoma nchini Marekani. Najua nakufanyia kitu kibaya sana Suleikha, hujawahi kuniudhi hata mara moja tangu tufahamiane.

“Umekuwa mfariji wangu mkubwa katika kipindi nilichokuwa mpweke lakini sina jinsi zaidi ya kuondoka na kwenda mbali nawe. Najua nawe utapitia maumivu kama niliyoyapitia mimi wakati Anna aliponikimbia lakini sina jinsi, nampenda zaidi Anna na moyo wangu unaniambia hivyo, nakuomba usinielewe vibaya.

“Nakuombea Mungu akupe ujasiri wa kukubaliana na hali halisi na usonge mbele kwenye maisha yako, naamini utapata mwanaume atakayekupenda na wewe ukampenda zaidi ya ilivyokuwa kwangu.

Nakutakia kila la heri!
“Ni mimi Jafet!”
Jafet alipomaliza kuandika ujumbe huo, aliuweka mfukoni na kuanza kutafakari kwa kina. Kila alipokuwa anamuona mwanachuo anayefahamiana na Suleikha na kutaka kumpa, moyo wake ulikuwa ukisita sana, kijasho chembamba kikawa kinamtoka.

Je, nini kitafuatia? Suleikha ataupokeaje ujumbe huo? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

2 Comments
  1. hanifa mwinyi says

    nobody can stop you as long as youou love each. nawapenda bure

  2. monica says

    Moyo wa mtu KICHAKA.

Leave A Reply