The House of Favourite Newspapers

Usisikie wewe, Ngumi si Mchezo!

0

Niwaambieni bila kumumunya wala figisufigisu kuwa kuanzisha mpambano wa ngumi ni jambo la hatari sana. Kuna watu wengi ukipita mitaani utasikia mtu anajisifu, ‘Ohh mi mbaya, mi napiga mpaka ndugu zako watauliza kama uligongwa na treni?’

Ukifuatilia utakuta maisha yake yote hajawahi kukinga hata ngumi, kazoea kuziona kwenye sinema basi naye anaona anaziweza. Bwana we ngumi mbaya. Sharti la kwanza baya kuhusu ngumi ni kuwa zikianza hazina poo, hakuna kusema tupumzike kidogo, hapo ni mpaka mtu apigwe ndiyo mchezo umekwisha, sinema zinadanganya sana.

Halafu Waswahili nao wabaya sana, wakiona mwenye kelele ndiye anapigwa, wanajichelewesha kuamulia. Sasa siyo kwamba naongelea mambo ya kusikia, naongelea yaliyonikuta, toka siku hiyo nikaapa sitaki tena ngumi.

Enzi hizo nikiwa bado kijana, najiona mjanja kwa kuwa nilikuwa naangalia sana sinema za Jems Bondi na Blus li, nilikuwa nina uhakika kabisa akijipendekeza mtu ntamng’oa meno bila tatizo. Basi siku hizo nikawa nikilewa tu naanza kuimba;

“Najisikia kuwatukana niwatukane? Shikeni adabu zenu mtaa mzima huu, au niwachane?” Basi hapo yeyote aliyepita mbele yangu mimi ni matusi na kashfa. Siku hiyo kakatokea kajamaa fulani kageni pale mtaani, hakanijui sikajui, kakanisogelea;

“We kwa nini unatukana watu hovyo?” Kaliponiuliza tu si ndiyo mzuka ukanipanda. “Shika adabu yako we nani? Kwanza huna mke, huna kitanda, ntakupiga halafu nakupa paspot uhame mtaa.” Nakumbuka kale kajamaa kaliniuliza swali moja tu, Umesema nini wewe?”

Kakaanza kukunja shati lake na mie nikajikunja staili ya Blusi Li, nikapanga ngumi ya kwanza nikabamize mdomo, ya pili ya shavu kama Jems Bondi, halafu nikapige teke la kiblus li, kazi kwisha. Hata sijui kilitokea nini, wakati najipanga nilipigwa ngumi ya pua, maumivu yalikuwa makali mpaka machozi yakatoka, nikawa sielewi hata niko wapi, nikapigwa ngumi tatu mfululizo, mbili za mdomoni moja ya kwenye shingo, najua nilianguka maana ghafla kajamaa kalikuwa sasa kamenikalia tumbo kanashusha ngumi za usoni bila pingamizi.

Majirani walivyo wabaya, badala ya kuamulia nawasikia, “Mshikishe adabu huyo si ndiyo wimbo wake mkuu.” Nilianza kuomba kimoyomoyo, jamaa anisamehe. Baadaye nikaona nipige kelele. “Nisamehe ndugu yangu, mimi ni binadamu mwenzio.” Kajamaa kakanitandika bao moja la mwisho na kuniambia shika adabu yako…acheni jamani ngumi si mchezo!

Leave A Reply