The House of Favourite Newspapers

UNYAMA, UKATILI KWA WATOTO MAMA YAMKUTA MAZITO!

MOROGORO: Mwanamke aliyefahamika kwa jina maarufu la Mama Naa, yamemkuta mazito baada ya kunusurika kifo laivu, Risasi Mchanganyiko lina kisa na mkasa.  

 

Mwanamke huyo alijikuta akipokea kichapo ‘hevi’ kutoka kwa wanawake wenzake waliokerwa na kitendo chake cha kudaiwa kumfanyia ukatili wa kumpiga hadi kumpasua kichwani mtoto wake wa kufikia.

 

Tukio hilo lililojaza umati mkubwa huku wengi wakiwa ni akina mama, lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita, majira ya asubuhi katika Mtaa wa Mtagwa Kata ya Kiwanja cha Ndege mjini hapa.

 

UMATI WAZINGIRA NYUMBANI

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa mwandishi wetu aliyefika fasta katika mtaa huo uliopo jirani na soko la matunda na mbogamboga la Mawenzi na kushuhudia umati ukizingira nyumbani kwa mwanamke huyo kisha kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Hamad Momboka.

 

Habari zilizopatikana eneo hilo la tukio zilieleza kuwa, mwenyekiti huyo ndiye aliyeokoa maisha ya mtuhumiwa huyo kwa kumficha ndani ya nyumba yake hivyo shukurani ziende kwake.

SHUHUDA ASIMULIA

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Asha Ally alikuwa na haya ya kusema: “Sisi kama wazazi na majirani wa mama huyu tumechoshwa na vitendo vya kikatili anavyomfanyia mtoto wake huyo wa kufikia.

 

“Leo alimtuma mtoto huyo dukani akanunue kibiriti.  alimpa shilingi mia tano, mtoto akaenda kununua vibiriti vitano badala ya kimoja. “Kwa kosa hilo tu alimvamia mtoto na kumtandika vibao kisha kumpasua kichwani kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali.

 

“Sisi kama majirani ambao tumejazana mtaani kufanya usafi wa mwisho wa mwezi, tuliamua kumvaa huyu mama na kumuokoa mtoto huyu. “Wenzetu wengine walipatwa na hasira sana wakashindwa  kujizuia na kujikuta wakimshushia kichapo.

 

AKIMBILIA KWA MWENYEKITI

“Mama Naa alipoona kundi la watu linaongezeka na kumshambulia ndipo akaamua kukimbilia kwa mwenyekiti wetu ambaye ndiye amemuokoa. “Kiukweli Mama Naa anatakiwa amshukuru sana mwenyekiti ambaye amemfungia ndani lasivyo sasa hivi tungekuwa tunazungumza mengine. “Sisi tupo hapa nje tunasubiri atoke tumshushie kichapo kwani hasira zetu hazijaisha.”

 

MSAMARIA MWEMA

Wakati hayo yakiendelea, msamaria mwema, Halima Nasoro ambaye ni mfanyabiashara wa mbogamboga sokoni hapo, alijitolea kukodi bodaboda na kumkimbiza mtoto huyo Kituo cha Afya cha Sabasaba kinachomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwani alikuwa akivuja damu nyingi kichwani.

KITUO CHA AFYA

Mwandishi wetu alitinga kwenye kituo hicho cha afya na kushuhudia wauguzi wakimuhudumia mtoto huyo. Hata hivyo, wahudumu hao waligoma kumpa ushirikiano mwandishi wetu kwa maelezo kwamba wakubwa wao hawakuwepo kazini. “Kaka samahani sisi hatuna kibali cha kukuruhusu kupiga picha mgonjwa wodini. “Ni kweli huyo mtoto yupo na tunaendelea kumtibu labda usubiri hadi atakapotoka ndipo umhoji,” alisema mmoja wa wahudumu hao.

 

MTOTO NA BANDEJI

Kweli, baada ya muda, mtoto huyo ambaye jina linahifadhiwa, mwenye umri wa miaka mitano alitoka nje akiwa na bandeji kichwani huku akiwa amebebwa na Halima.

Akizungumza kwa taabu na gazeti hili, mtoto huyo alisimulia kisa na mkasa: “Mama yangu wa kambo alinipa shilingi mia tano nikanunue kibiriti, nilijisahau nikanunua vibiriti vingi. “Nilipomkabidhi aliniambia kwa nini nimenunua vibiriti vingi ndipo akaanza kunipiga.

 

“Nilimponyoka nikaanza kukimbia ndipo akaokota kitu chenye ncha kali na kunipiga nacho kichwani. “Nilihisi maumivu makali sana na kujikuta nikilia kwa uchungu hadi watu wenye huruma akiwemo huyu mama (Halima) wakaja kuniokoa.”

 

MWENYEKITI SASA

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa huo, Momboka alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake na kueleza alivyotumia nguvu kubwa kumuokoa mama huyo asiuawe na wananchi waliokuwa na hasira kali.

 

“Yaani bila mimi kutumia ubabe na kumficha ndani, watu wangemuua mama huyu. “Nilikuwa nasimamia usafi kwenye mtaa wangu, ghafla nikaona zogo na huyu mama akaja mbio akiomba msaada ndipo nikamkimbiza na kumficha humu ndani. “Nimewajulisha Polisi wako njiani wanakuja,” alisema mwenyekiti huyo.

 

BABA MZAZI

Katika hali ya kushangaza, baba mzazi (pichani) wa mtoto huyu alipohojiwa na gazeti hili aligoma kutoa ushirikiano. “Nikueleze ili iweje? Zaidi ya yote nitakuwa ninamdhalilisha mke wangu. “Kifupi mimi kama baba wa familia hii sina cha kuongea kwenye tukio hili,” alisema baba huyo.

 

POLISI NA SILAHA NZITO

Baada ya majibu hayo, baadhi ya watu waliokuwa jirani wakisikiliza mazungumzo hayo walimzomea baba huyo. Muda mfupi baadaye, difenda lilifika eneo la tukio likiwa na Polisi wenye silaha nzito ambapo mkuu wa difenda, Betrice Lyamuya alimuamuru Afande Mwajabu kuingia ndani na kumtoa mtuhumiwa huyo.

 

Baada ya kutolewa nje, mtuhumiwa huyo na mumewe walipandishwa kwenye difenda na kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi ambako huko ndipo watakapofunguliwa mashitaka.

Comments are closed.