The House of Favourite Newspapers

Unyama Wa Kutisha: Mwenyekiti wa Kitongoji Kibiti Atobolewa Macho (Video)

0
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo, Kijiji cha Mwangwi Kata ya Mchukwi, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Michael Martin.

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Londo, Kijiji cha Mwangwi Kata ya Mchukwi, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Michael Martin (29) ameelezea jinsi alivyotekwa, kufanyiwa unyama wa kutisha na kuvuliwa nguo mbele ya familia yake kisha kutelekezwa katikati ya maiti za viongozi wenzake na watu wasiojulikana.

 

Mwenyekiti huyo akizungumza na Gazeti la Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita alipohifadhiwa na Msamaria mwema Magomeni jijini Dar alisema kuwa, katika maisha yake hawezi kuisahau Juni 27, mwaka huu baada ya kuvamiwa na watu saba wasiojulikana waliovalia kininja na kuuvunja mlango wa nyumba yake na kumteka.

 

JINSI ALIVYOTEKWA

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema; “Ilikuwa kama saa nne usiku mimi na familia yangu tukiwa ndani tumeshaanza kulala, ghafla nilishtukia mlango wa nyumba yangu umevunjwa na tayari watu hao walikuwa wameshaingia ndani.

“Hapo sikuwa na ujanja wa kuweza kujihami kwa lolote, walipoingia tu swali walilokuwa wakiniuliza kwa kurudia kila mara ni wewe si ndiyo Michael, si ndiyo wewe Michael?

“Niliwajibu ndiyo.”

NYUMBA YAKE YATEKETEZWA

Michael aliendelea kuelezea mkasa huo ambapo alisema baada ya kuwajibu kuwa ndiyo yeye, walimtoa nje na familia yake na wote wakawavua nguo ambapo wengine waliwaambia walale kifudifudi wakati huo yeye walimteka na kwenda naye kusikojulikana.

 

“Walinifunga kamba shingoni kama mbwa, na mikono walinifunga kwa nyuma na kuanza kunipeleka kusikojulikana huku wakinitesa kwa kunipiga, hapo nilikuwa tayari nimeshachanganyikiwa ambapo nikiwa hatua chache kutoka nyumbani kwangu nilianza kuona mwanga mkali wa moto nilipoangalia nyuma, nikaona nyumba yangu inateketea kwa moto.

 

KIPIGO KAMA MWIZI

“Baada ya muda tena nikasikia mlipuko mkubwa wakati pikipiki yangu ikibutuka ilipokuwa ikichomwa moto.

“Nilipofika kule waliponipeleka niliwakuta viongozi wenzangu Mwenyekiti wa Kijiji, Hamisi Mkima na Mtendaji wa Kijiji, Shamte Makawa nao wakiteswa ambapo baada ya kunifikisha hapo walinifunga kama wao huku wakitutesa kwa kutupiga kama wezi.

 

“Ghafla nilishtukia nimepigwa na gongo upande wa jicho la kulia hapohapo nikasikia mlipuko kwenye jicho langu la kupika kelele, hapo nilipoteza fahamu na kujishtukia niko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo niliambiwa kabla ya kuletwa hapa nilipelekwa katika Hospitali ya Mishini ya Mchukwi iliyopo Kibiti.

 

“Niliambiwa na wasamaria wema kuwa wakati naokotwa porini nilikuwa katikati ya maiti mbili za viongozi wenzangu.”

 

APOFUKA NA KUTIMULIWA

Michael alisema hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya kutibiwa majeraha na kuambiwa na madaktari kuwa tayari ameshapona majereha ila daktari wa kulifanya jicho lake la kulia ambalo halikuharibika sana hawana mtaalamu wa kulifanya liwe na uwezo wa kuona tena kwani lingine liliondolewa.

“ Walinitaka niondoke hospitalini hapo na mimi kwa kuwa sikuwa tayari kurudi tena Kibiti na familia yangu, tulihifadhiwa na rafiki yangu Tandika, Dar lakini baada ya muda huyo jamaa alinitimua akisema hawezi kunilea mimi na familia yangu.

 

“Nilichanganyikiwa na kuanza kuomba kila kona mwenye nafasi anipe sehemu ya kujibanza na familia yangu ambapo kwa sasa nimehifadhiwa hapa Magomeni lakini huyu aliyenihifadhi hapa naye anasema amenichoka anataka niondoke kwa maana hakujua kama nitakaa kwa kwake kwa muda mrefu.”

 

ANAVYOIMUDU FAMILIA

Mwenyekiti huyo alisema kuwa, kwa sasa anaendesha familia yake kwa kuombaomba mitaani akiongozwa na mkewe ambaye anamshika mkono na kumuongoza.

“Nimegeuka ombaomba kazi ambayo nilikuwa nikiilaani kwenye maisha yangu,” alisema.

 

VIPI KUHUSU KURUDI KIBITI?

Michael alisema kamwe hawezi kurudi Kibiti na kila kitu alichoacha yakiwemo mashamba ameyaacha huko.

“Kule siwezi kurudi tena kwa maana walionifanyia unyama huu siwajui hivyo, sina mpango tena wa kurudi Kibiti kwa maana hata sasa nikilikumbuka lile tukio huwa nachanganyikiwa, nilionja kifo.

 

OMBI LAKE KWA WATANZANIA

“Nawaomba Watanzania wanisaidie nipate mtaji wa kufanya biashara maana mke wangu anaona, mwenye nia ya kunisaidia atumie namba 0783814506. Pia naliomba Jeshi la Polisi chini ya IGP Saimon Sirro kuwatafuta walionifanyia unyama huu ili wafikishwe mbele ya sheria,” alisema.

STORI: RICHARD BUKOS | GAZETI LA UWAZI NOV 7, 2017

Leave A Reply