The House of Favourite Newspapers

UNYAMA! Wavuvi 4 Wauawa Baharini Kikatili, Kisa Kitakuliza – VIDEO

Amour enzi za uhai wake.

WATU wanne ambao walikuwa wavuvi, wanadaiwa kuuawa kinyama huku wengine kadhaa wakiwa hawajulikani walipo.

 

Katika tukio hilo lililojiri hivi karibuni, watu hao, wakazi wa Kigamboni- Vijibweni jijini Dar, walidaiwa kuuawa kikatili baada ya kupigwa na watu wasiojulikana kisha miili yao kutoswa baharini ambapo maiti zao ziliokotwa zikiwa zimeharibika vibaya.

Paul enbzi za uhai wake.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, mmoja wa manusura wa tukio hilo, Amri Issa aliwataja waliouawa kuwa ni Amour Abdallah (22), Paul George (52), Saidi Shaban na mwingine ambaye hakutambulika kutokana na mwili wake kuokolewa ukiwa umeharibika vibaya.

Amri alisimulia kuwa, siku ya tukio walikwenda kuvua kama kawaida yao majira ya saa 12:00 jioni.

Alisema walirejea kutoka baharini majira ya saa 7:00 usiku wakiwa wamepata samaki wengi.

Aliendelea kueleza kuwa, walipofika nchi kavu pembezoni mwa Bahari ya Hindi, walianza kuchambua samaki hao ndipo walipovamiwa na watu wasiojulikana.

Alisema, wakiwa wametaharuki, wenzake (wavuvi) kama kumi walikimbilia baharini na kupotelea humo.

“Tulikuwa tumeshavua samaki wengi kama ndoo 40 hivi, ndipo tulipovamiwa na watu hao. Wenzetu wengine walivyoona hivyo walikimbilia kwenye maji na sisi wengine tukabaki nchi kavu, tukaanza kupigwa.

“Watu hao walianza kutupiga tangu saa 7:00 usiku hadi saa 10:00 Alfajiri,” alisema manusura huyo.

Baada ya wenzake kukimbilia baharini, kulikuwa na boti iliyobeba watu hao waliowavamia ambayo iliwafuata wakiwa wanaogelea, walipowafikia walianza kuwapiga na vitako vya bunduki kichwani hivyo wengine walishindwa kuibuka kutoka majini.

Mwili ukitolewa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

“Tulishuhudia wenzetu wakipigwa na vitako vya bunduki ambapo wengine baada ya kupigwa na kuzama hawakuibuka ila tulimuona mwenzetu mmoja alikuwa anajitahidi kuinuka ndipo wakamchukua na kumwingiza kwenye boti yao na kuanza kumpiga hadi alipokufa kisha wakamrusha majini,” alisema Amri.

 

Alisimulia kuwa baada ya kuwapiga mno kwa kutumia mikanda watu hao waliwakamata na kuwapeleka Kituo cha Polisi cha Kivukoni, Kigamboni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa jamaa huyo, cha kushangaza baadaye waliwaachia na kuwaambia kuwa wamepewa mamlaka wakikuta wavuvi haramu ni kuwaua tu.

“Tuliachiwa tukiwa na maumivu makali huku tukishuhudia vifo vya wenzetu. Kwa kweli tuliumia sana kiasi kwamba ni vigumu kusahau mateso tuliyokutana nayo,” alisema.

Kwa upande wa mama wa kijana mmoja aliyeuawa kwenye tukio hilo, Amour Abdallah, Diana Mganda alisema kuwa mtoto wake alikuwa bado kijana mdogo aliyekuwa akijitafutia maisha.

“Tulimsubiri bila mafanikio ndipo baba yake akiwa anakwenda kwenye shughuli zake, akasikia kuna wavuvi wameuawa baharini. Aliporudi kuja kutoa taarifa, tuliingiwa na hofu,” alisema mama huyo.

Walimtafuta mtoto wao kwa siku tatu hadi walipopewa taarifa kuna maiti ilionekana pembezoni mwa bahari ikiwa imeliwa upande mmoja na samaki.

“Tulipopewa taarifa hiyo ya kupatikana kwa maiti ambayo haitambuliki ndipo nikawaambia wamwangalie mwanangu ana kovu begani na walipofanya hivyo walibaini ni yeye,” alisimulia mama huyo.

Baba wa marehemu Amour.

Kufuatia tukio hilo, huku maiti nne zikiwa zimezikwa na ndugu zao hadi juzi, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, ACP Andrew Satta ambaye alisema hakuwa na taarifa za tukio hilo.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema atalifuatilia tukio hilo baada ya kupokea taarifa ya mwandishi wetu.

STORI: Imelda Mtema, Dar

TAZAMA VIDEO YA NDUGU WAKIFUNGUKIA TUKIO HILO

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.