The House of Favourite Newspapers

Usichokijua Kuhusu Vita Ya Marekani VS Korea Kaskazini-12

0
Rais Donald Trump wa Marekani

Katika vita hii inayonukia kati ya Marekani na Korea Kaskazini, wiki iliyopita nilieleza namna ambavyo mjadala ulikuwa umepamba moto. Swali lilikuwa ni je, ni nani ataibuka kidedea kwenye vita hii? Pia tulipata kuangalia uzoefu wa Korea Kaskazini namna ambavyo ni mdogo ukilinganisha na Marekani ambayo imeshiriki vita sehemu mbalimbali duniani. Sasa endelea…

 

WAKATI Korea Kaskazini ikiendelea na vitisho vyake, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson alikaririwa akisema kuwa hakuna mgongano wowote kati ya Marekani na China kama ambavyo imekuwa ikielezwa kuwa nchi hizo zipo kwenye msuguano uliosababishwa na Korea Kaskazini. Kiongozi huyo anasema kuwa katika mazungumzo yaliyofanyika Beijing kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa China, Xi Jinping walikubaliana kuwa hakuna tatizo kati yao.

 

Tillerson alisema kuwa, mazungumzo ya wawili hao yalilenga suala la vitisho vya Korea Kaskazini. Anasema viongozi hao wawili walikuwa wawazi katika mazungumzo yao juu ya masuala ya haki za binadamu na migogoro ya bahari katika eneo la South China Sea. Kuhusu Korea Kaskazini, Wachina waliweka wazi na bila ya kupinga katika mazungumzo ya siku mbili kuwa hawatakubali kuwepo Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia. “Hakuna mwanya wowote katika kufikia malengo ya pande zetu mbili,” anasema Tillerson na kuongeza: “Tunayo maoni yetu juu ya mbinu, muda na kwa kiwango gani tuweke shinikizo na juu ya hilo ndiyo tumetumia muda mwingi katika kubadilishana mawazo.”

 

Trump, kwa mujibu wa Tillerson, alimwambia Xi: “wewe ni mtu shupavu, ninaamini una uwezo wa kutatua tatizo hili kwa ajili yangu.” Kabla ya hapo Rais Trump alisema kuwa, Marekani na China ni lazima zifanye kazi kwa pamoja kulikomboa eneo hilo na dunia kwa kile alichokiita ni tishio baya mno linalofanywa na utawala unaofanya mauaji wa Korea
Kaskazini.

 

Katika maelezo yake Trump hakuruhusu maswali kutoka kwa waandishi wa habari ambao walitaka hasa kujua msimamo wa nchi mbili zenye nguvu kubwa duniani. Trump aliishia kutamba kuwa, Marekani na China wamekubaliana kutorudia makosa ya siku za nyuma katika kukabiliana na Korea Kaskazini ambapo mara kadhaa walijikuta kwenye msuguano mkubwa.

 

Kwa miaka kadhaa sasa, Marekani na China zinakiri kuwa, Korea Kaskazini wameweza kwa haraka kupiga hatua katika programu yao ya silaha za nyuklia na makombora ya balistika.

 

“Dunia nzima yenye ustaarabu lazima ishirikiane katika kukabiliana na hatari ya Korea Kaskazini,” alikaririwa akisema Trump ambaye baadhi ya wachambuzi wanadai kuwa alitaka kuungwa mkono kwa hofu kuwa, Korea Kaskazini yaweza kuwa vyema kwenye eneo hilo la silaha.

 

Katika maelezo yake yaliyokuwa yametayarishwa, kauli ya Xi ilikuwa siyo wazi sana juu ya Korea Kaskazini, akisema: “Tumesisitiza kuwa na msimamo thabiti katika kuondoa silaha za nyuklia katika rasi hiyo.” Trump alimjibu: “Ninaamini kuwa tuna suluhisho kuhusu hilo, kama mlivyokuwa nalo ninyi.”

Leave A Reply