The House of Favourite Newspapers

Utajiri Au Umaskini Unatokana Na Wewe!

0

SIKU moja nilifundisha mahali na nikatoa changamoto kuwa kila mtu anaweza kupata muda wa kusoma kitabu kama akiamua.

 

Nilieleza faida ya kusoma vitabu na nikatoa hamasa kubwa ya watu kusoma. Baada ya wiki moja kijana mmoja akasema ameshamaliza nusu ya kitabu alichokianza, nikampongeza na kumwambia aendelee na juhudi hiyo. Sikumsikia tena baada ya hapo, hivyo niliamua kumtafuta tena baada ya wiki mbili kumuuliza maendeleo yake, sikuamini jibu lake; “Bado sijamaliza kitabu, tangu siku ile sikupata nafasi ya kusoma tena!”

 

Watu wengi wanakabiliwa na matatizo makubwa mawili; Moja ni kukosa nidhamu (indiscipline) ya kufanya jambo unalotakiwa kufanya bila kujali kama unajisikia kufanya au la.

Pili ni kukosa nguvu ya mwendelezo (incosistence) yaani ukianza kubomoa ukuta kwa nyundo, inawezekana nyundo ya mia moja ndipo ukuta ukaanguka. Swali ni kwamba, ni pigo la nyundo la mara mia moja ndilo limeangusha ukuta? La hasha, ni mkusanyiko wa mapigo yote (cummulative effect). Ndivyo ilivyo kwenye maisha.

 

Maisha unayoishi sasa, kwa sehemu kubwa yanatokana na uamuzi ulioufanya kipindi cha nyuma na maisha utakayoishi kesho pia yanategemea sana uamuzi unaoufanya leo kwenye maisha yako.

 

Una uwezo wa kuboresha maisha yako kwa kufanya uchaguzi sahihi wa hatua unazozichukua kila siku.

JIFUNZE KUTAWALA PESA

Moja ya kitu unachotakiwa uanze nacho ili uweze kuchukua hatua sahihi, ni kujifunza juu ya kutawala pesa zako.

 

Hivi pengine nikuulize, umeshawahi kujiuliza katika maisha yako; pesa ngapi zimepita mikononi mwako? Ukiangalia, ni pesa nyingi sana, lakini cha ajabu kwa wengi zimewaacha jinsi walivyo wakiwa hawana kitu.

 

Sasa basi, ili kuendelea kukosa pesa kusitokee kwako, unahitajika sana kujifunza juu ya kuwa na uamuzi sahihi wa kutawala pesa zako. Ukiipata elimu hii na ukaielewa vizuri, utakuwa umefanya uamuzi sahihi wa kukupeleka kwenye utajiri wako moja kwa moja.

 

Kwa mujibu wa uchunguzi mdogo nilioufanya, asilimia kubwa ya watu walio maskini hawaweki akiba kabisa. Hiyo ikiwa na maana kipato chote kinachobakia kinaingizwa kwenye matumizi.

 

Mpaka hapo kwenye uamuzi huo, ni sehemu ya uamuzi mbaya unaowapeleka wengi kwenye umaskini. Akiba au kujilipa mwenyewe kiasi kidogo cha kila pesa unayopata ni kitu cha msingi sana kama unataka kesho yako iwe ya mafanikio.

 

Ni kweli suala la matumizi ya pesa zako liko mikononi mwako, lakini ili uwe tajiri ni lazima ujue namna ya kutawala pesa zako. Siyo kwa sababu una pesa unanunua vitu hovyo na kujikuta hakuna hata kiasi kidogo cha pesa ulichobaki nacho.

 

Angalia usije ukajikuta ukajuta kesho kutokana na uamuzi mbovu unayoyafanya leo juu ya pesa zako. Fanya uamuzi leo bora, utakaokufanya kesho ukajiona shujaa mkubwa kwa kujiona ulifanya kitu cha maana kwa sababu ya pesa zako.

 

Ikiwa unataka kuendelea kimaisha na hata kuwa tajiri, elewa vizuri juu ya kutawala pesa, yote haya unatakiwa ujifunze ukiwa bado kijana, kama hautafanya uamuzi huo sahihi, ni wazi hautafanikiwa.

 

Utajiri au umaskini wako, siku zote upo mikononi mwako kutokana na uamuzi unaoufanya juu ya pesa. Leo jiwekee kiapo kwamba, kwa pesa yoyote unayoipata, ni lazima uweke kidogo kwa ajili yako.

 

Kwa kuanzia, anza hata na asilimia kumi ya kile unachokipata, umeshindwa kabisa, anza na kiasi chochote. Pesa hiyo kumbuka ni yako, unakuwa hujapoteza popote, hivyo usiwe na wasiwasi, chukua uamuzi sahihi leo utakaokupa utajiri.

Leave A Reply