The House of Favourite Newspapers

UVCCM Songwe Waanza Kusaka Kura Nyumba kwa Nyumba

0

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM) Mkoa wa Songwe wamezindua kampeni ya mkoa mzima ya kutafuta kura za wagombea Urais, Ubunge na Madiwani kwa tiketi ya CCM.

 

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Southern Garden uliopo katika Mji wa Vwawa Wilayani Mbozi mkoani Songwe, ulianza kwa maandamano kuanzia makao makuu ya CCM Songwe na kupokelewa ukumbini hapo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Ellyniko Mkola.

Mratibu wa Kampeni za kusaka kura hizo Mkoa wa Songwe, Ombeni Nanyaroo amesema kuwa kampeni hizo zitafanyika mkoa mzima wa Songwe na zitafanywa nyumba hadi nyumba, mtaa kwa mtaa.

“Kampeni hii tutahakikisha tunawaeleza watanzania popote Mkoani Songwe mambo yote mazuri yaliofanywa na Rais wetu Magufuli na kuwaeleza watanzania kwanini wanapaswa kumchagua tena” alisema Ombeni Nanyaro.

 

Kwa Upande wake Mwenyekiti UVCCM Mkoa Andrew Kadege amewasihi Wanasongwe kuiamini CCM kwa kuwapa kura kwa wingi wagombea wa chama hicho ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais.

“Mwaka huu ni wa Uchaguzi, kwa haya yaliofanywa na CCM chini ya Rais wetu Dk. John Magufuli tunakila sababu ya kuaminiwa tena na tupuuze uongo unaofanya na wapinzani walikosa hoja za msingi majukwaani,” alisema Kadege.

 

Kadege pia alieleza Jeshi la Polisi kuongeza umakini zaidi kwani wao wamepata taarifa za uwepo wa vijana zaidi ya 100 walioletwa na chama kimoja upinzani ili kuanzisha maandamano katika mji wa Tunduma yenye lengo la kuvuruga Uchaguzi.

 

” Tunaliomba Jeshi la Polisi kulidhibiti mapema kundi hilo na sisi kama UVCCM tutawapelekea Polisi ushahidi tulionao, alisema.

Akifunga ufunguzi huo wa Kampeni Mwenyekiti CCM Mkoa, Ellyniko Mkola amewataka Vijana Mkoani humo na watanzania kwa ujumla kuwapuuza wanasiasa wanaofanya upotoshaji wa miradi mikubwa iliofanywa na serikali ya awamu ya tano.

 

“Katika kampeni hizi kumezuka tabia ya wapinzani kuanza kugombania miradi ya serikali na kudai wao ndio wameileta miradi hiyo, hilo si kweli miradi hii imeletwa na serikali ilio chini ya CCM” alisema Mkola.

Leave A Reply