The House of Favourite Newspapers

Uwezekano wa Kuyashitaki Makampuni ya Madini Kurejesha Hasara Tuliyoipata Huu Hapa

0

UWEZEKANO  WA  KUYASHITAKI  MAKAMPUNI  YA  MADINI KUREJESHA  HASARA TULIYOIPATA HUU  HAPA

Na  Bashir   Yakub

Mikataba yoote ya kimataifa huongozwa na wajibu wa aina mbili. Wajibu ulioandikwa(express obligation) na wajibu ambao haukuandikwa(implied obligation).

Wajibu ulioandikwa ni masharti yote ya mkataba yaliyo katika maandishi  ambayo wahusika husoma na kuridhia, wakati wajibu usioandikwa ni masharti ya mkataba ambayo hayakuandikwa katika mkataba lakini  yapo kwa asili au yapo kwakuwa tayari yalishasemwa na sheria na hivyo si lazima kuyaandika ktk mkataba.

Mathalan, mfanyakazi  wako wa duka hawezi kukuibia halafu akasema kwenye mkataba wangu wa ajira hakuna sharti la uaminifu. Laa hasha  uaminifu  ni sharti la asili “implied obligation” kwa hiyo liandikwe au lisiandikwe  bado lipo tu.

Kwenye mikataba ya kimataifa kama ile ya kwetu na makampuni  ya madini masharti yafuatayo ni ya  asili na hayahitaji kuwa yameandikwa ili kuyatekeleza :

  1. Wajibu wa kuanika taarifa zote muhimu kuhusu  shughuli inayotekelezwa katika mkataba( Implied covenant to disclose all necessary information over the subject matter).
  1. Wajibu wa kutekeleza na kutenda  kwa nia njema(Implied covenant to act in good faith and fair dealing).
  1. Wajibu wa kila mhusika katika mkataba kuwa  mkweli . Hili huwa ni katazo la udanganyifu(Fraud).

Haya yawe yameandikwa kwenye mkataba au hayakuandikwa yakikiukwa tafsiri  yake ni kukiuka masharti ya mkataba.

Matendo kama kulaghai kuhusu uzito wa madini yanayochukuliwa, kulaghai kuwa unachukua dhahabu huku ukijua unachukua zaidi ya dhahabu, kulaghai kuhusu bei , kutotoa taarifa sahihi za kipi unapata na kipi hupati,nk ni kukiuka wajibu  na masharti ya mkataba jambo ambalo  ni kinyume cha sheria.

Na ikiwa wamekiuka mkataba kwa misingi hiyo  basi Tanzania inaweza kufanya yafuatayo;

  1. Kuendelea na mkataba lakini kwa sharti la kurudisha kile chote kilichopotea kwa mda wote( specific performance).
  1. Kutoendelea na mkataba na kudai fidia, hasara tuliyopata,pamoja na riba zake kwa kipindi chote(breach of contract).

Ndugu zangu, wajibu wa  kutekeleza na kutenda kwa nia njema (implied covenant to act in good faith and fair dealing), kuwa mwaminifu na kutoa taarifa sahihi katika utekelezaji mikataba ni  matakwa ya lazima duniani kote.

Sheria ya biashara ya Amerika Uniform Commercial Code vifungu vya 1 – 12 habari hii imeelezwa kwa upana.

Sheria ya biashara ya Ufaransa na Ujerumani The German Civil Code(BGB) na Civil Code of France zimeeleza vitu hivi.

Pia mahakama kuu ya Uingereza katika kesi ya Yam Seng PTE vs International Trade Co. Ltd (2013) EWHC 111 ( QB) iliamua kuwa masuala ya uaminifu na kutoa taarifa sahihi katika kutekeleza mikataba ni wajibu ambao upo hata Kama haukuandikwa kwenye mkataba.

Halikadhalika sheria yetu ya Mikataba, Sura ya 345 vifungu  vya 18 na 13 vimeyafanya masuala ya udanganyifu na kutoa taarifa zisizo sahihi  kama mambo ambayo ni makosa  na yanayobatilisha mkataba.

Kamati ya Profesa Mruma  imebaini upotevu wa Bilioni 829.4 x Miezi 12 kwa miaka 18 =  Trilioni 829.4. Hizi ni pesa nyingi mno. Tunayo kesi nzuri ya madai  na uhakika wa kurejesha fedha tulizopoteza. Ni vema mda huu pamoja na mambo mengine, nguvu nyingi ikatumika kuona ni namna gani tunapata hii fedha. Makosa yapo na  yametendwa na hilo halina Shaka. Iko wapi haja kukhofu, hakika haipo.

Yumkini haitakuwa rahisi kutokana  na aina ya mabepari  ambao tunashughulika nao. Ni mabepari  hatari wenye mtandao mkubwa wa kisiasa na nchi wafadhili pamoja na taasisi kubwa kama IMF, WB, UN nk.

Hata hivyo tumeshasema hii ni vita na vita sharti ipiganwe ili waliosiginwa wawe huru.  Tunaweza kuumia kwa mda ila mwisho wa maumivu hayo itakuwa ni neema kubwa na ya milele.

Mungu ibariki Tanzania na Mungu mbariki rais kwa pamoja tushinde vita hii.

Kuhusu  sheria  za  ardhi, mirathi, makampuni, ndoa  n.k, tembelea  SHERIA   YAKUB   BLOG.

Leave A Reply