The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Baba wa Watoto Waliozaliwa Wameungana Aomba Msaada

0
Watoto waliozaliwa wakiwa wameungana.

 

BABA wa watoto waliozaliwa mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwa wameungana miili yao katika Hospitali ya Misheni ya Berege, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, Luca Chimola amesema anaiomba serikali imsaidie ili wanawe waweze kufanyiwa upasuaji wa kuwatenganisha.

Akizungumza na gazeti hili, Chimola alisema mke wake Rebecca Mwendi (42) alijifungua kwa njia ya upasuaji pacha wa kike Julai 21, mwaka huu ambao wameungana kifuani hadi tumboni.

“Kwa kweli hali yangu kiuchumi ni mbaya, tumezaa na mke wangu watoto wanane lakini mimba zote hazijawahi kumsumbua ila hii imemsumbua sana na kutufanya kuja hospitali mara nyingi na imenigharimu,” alisema.

 

Watoto hao wakibwbwa na muuguzi.

 

Akifafanua zaidi Chimola alisema wakati wa kuilea mimba hiyo alilazimika kuuza shamba lake ili kugharamia matibabu ya mkewe, hivyo sasa hana kitu na kwa jinsi hali ilivyo, kuna gharama kubwa zitatakiwa ili kuwanusuru watoto wake ndiyo maana anaiomba serikali au watu wenye huruma kumsaidia.

Daktari aliyemfanyia upasuaji mama huyo, Alfred Chiponde alisema amekuwa akifanya kazi hiyo kwa miaka 15 sasa lakini hiyo ni mara yake ya kwanza kumzalisha mama mwenye watoto walioungana.

Mwandishi: Sasa nini hatima ya watoto hawa walioungana?

 

Wodi ya wazazi.

 

Dk: Tumefanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya utaratibu wa rufaa. Tunasubiri mama wa watoto hawa apate nafuu tumpe rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Morogoro ambako watamchunguza na wakiona hawawezi wanaweza kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mwandishi: Kwani watoto hawa wameungana nini na nini kitaalamu?

Dk: Wameungana kifuani hadi tumboni pia wana kitovu kimoja lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa na viungo vingine kila mmoja ana vyake.

Mwandishi: Vipi kuhusu afya yao kwa jumla?

Dk: Afya zao ni nzuri na walizaliwa wakiwa na kilo sita kwa jumla, tatizo kubwa ni kuungana.

Wazazi wa watoto hao.

 

Mwandishi: Je kuna uwezekano wa kuwatenganisha?

Dk: Kuhusu uwezekano wa kuwatenganisha hilo tuwaachie madaktari wa rufaa ambao watalazimika kukaa jopo maana si suala la daktari mmoja kuamua na ni lazima vipimo vya kina vifanyike.

Watoto hao wamewekwa kwenye chumba maalum katika hospitali hiyo ambapo muuguzi wa zamu, Rehema Simwali alisema wamefanya hivyo kwa kuwa kinga ya mwili ya watoto hao ni ndogo, hivyo ni rahisi kuambukizwa magonjwa ndiyo maana wamewaweka sehemu hiyo maalum na hawaruhusiwi watu wengine kuingia isipokuwa wazazi tu.

STORI: DUSTAN SHEKIDELE | UWAZI| MOROGORO

TAZAMA VIDEO YA WATOTO HAO

Leave A Reply