The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Mfanyabiashara wa Tanzania Afariki Shambulio la Al-Shabaab

Mfanyabiashara Mtanzania,  Mahad Nur Gurguurte,  enzi za uhai wake.

MFANYABIASHARA Mtanzania,  Mahad Nur Gurguurte,  ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maisha Supermarket amefariki dunia Julai 12, 2019 katika shambulio la kigaidi la Al-Shabaab katika hoteli ya Asasey  mjini Kismayo huko Somalia.

 

Mahdi atakumbukwa zaidi kwa biashara za hoteli nchini, ikiwemo ile ya Paradise Beach ya Bagamoyo ambayo iliungua kwa moto, kiwanda cha unifomu na viatu vya viwandani na maduka makubwa (supermarket) kadhaa.

Meneja wa Maisha Supermarket,  Emodia Lloyd, amesema ni kweli Mahad Nur amefariki kwenye shambulio hilo.

”Alikuwepo kwenye hoteli ya Asasey ambayo imeshambuliwa, baada ya taarifa tulimtafuta hakuwa anapatikana kwenye simu, tukawasiliana na mtu mmoja huko akaenda kuangalia chumbani kwake hakumkuta ikabidi aende hospitali ndipo akakuta mwili wake”, ameeleza Emodia.

 

Emodia amesema kuwa kuna Mtanzania mwingine ambaye aliambatana na Mahad Nur, kwenye safari hiyo ya kibiashara,  yeye amejeruhiwa na yupo hospitali lakini bado hawajapata taarifa za maendeleo ya hali yake kwa sasa.

 

Mahad Nur alikwenda Somalia siku saba zilizopita na kufikia kwenye hoteli ya Asasey iliyopo mjini Kismayu ambayo ndiyo imeshambuliwa usiku wa kuamkia leo Julai 13, 2019.

 

Kuhusu taratibu za mazishi,  Emodia amefafanua kuwa msiba upo nyumbani kwa baba yake Kigamboni, lakini taratibu zinazoendelea huenda Mahad akazikwa leo huko Kismayu kutokana na taarifa  kuwa mwili umeharibika hivyo ni ngumu kuusafirisha.

Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.

Comments are closed.