The House of Favourite Newspapers

VIFO MFUFULIZO VYA WASANII VILIVYOSHTUA

WIKI ya masikitiko! Hivyo ndivyo unaweza kusema kufuatia vifo mfululizo vya mastaa wanne Bongo, ambao ni muuza sura kwenye video za Kibongo, Agness Gerald ‘Masogange’, muigizaji Zena Dirp maarufu kwa jina la Bi Sauda au Mama Cheni, muigizaji aliyetikisa kwenye Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu, Dalilah na mwanamuziki Jebby, vilivyozua gumzo!

HOFU MPYA

Baada ya vifo hivyo, ukweli ni kamba kwenye mitandao ya kijamii pamoja na uchunguzi ambao Ijumaa limeufanya, lilibaini hofu kutanda kwa baadhi ya mastaa na watu mitandaoni kutokana na historia ya huko nyuma ya mastaa kuondoka mfululizo katika mwezi Aprili na Mei.

Historia ambayo inafananishwa ni ya vifo vilivyowahi kutokea kati ya mwaka 2012 hadi 2014 ambapo mastaa wengi walifariki dunia akiwemo Steven Kanumba, Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’, John Maganga, Albert Mangweha ‘Ngwea’, Rachel Haule, Adam Kuambiana, Juma Kilowoko ‘Sajuki’, Langa Kileo na wengine wengi.

“Hii ni ishara ya hatari, hivi vifo vya mfululizo namna hii vinatupa hofu kubwa sana maana vinatukumbusha miaka iliyopita ambayo tuliwapoteza wenzetu wengi ambao pengo lao halijazibika hadi sasa,” alisema msemaji wa Chama cha Waigizaji Kinondoni, Masoud Kaftany.

MISIBA MFULULIZO

Ndani ya wiki moja kulitokea misiba ya wasanii wanne wakiwemo wa muziki na filamu ambapo alianza msanii wa maigizo wa zamani kutoka Kundi la Kaole, Zena Dirp maarufu kwa jina la Bi Sauda au Mama Cheni ambaye alifariki dunia Aprili 17, mwaka huu.

Baada ya msiba huo, wa pili aliyefuatia ni aliyekuwa video queen na mwigizaji wa filamu Bongo, Agness Gerald Waya ‘Masogange’ ambaye kifo chake kilimshtua kila mtu kwani aliugua kwa siku nne tu na kufariki dunia Aprili 20, mwaka huu. Kifo kilichofuata ni cha msanii wa filamu aliyeshiriki kwenye Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu, Dalilah aliyefariki dunia katika Hospitali ya Temeke, Dar, Aprili 21, mwaka huu.

Kama haitoshi, naye msanii wa Muziki wa Bongo Fleva, Jebby ambaye alifariki dunia Aprili 22, mwaka huu nyumbani kwao, Dodoma. Vifo hivyo vingi ni vya ghafla na ambavyo havikutarajiwa kwani hakuna aliyekuwa ameugua kwa muda mrefu na kusababisha watu labda wamkatie tamaa, bali ni muda mfupi tu.

KUKOSEKANA KWA AMANI

kutokana na misiba mfululizo, mastaa wengi wamejikuta wakikosa amani na wengine kusema kuwa inabidi wabadili mfumo wao wa maisha huku wakiwataka na wengine kubadilika kwani kifo hakina taarifa.

“Kiukweli vifo hivi vimetushtua sana, ninawasihi wasanii wenzangu tubadili maisha yetu, tusiishi kwa mazoea, vifo vya wenzetu view funzo kwetu tuliobaki,” alisema Halima Yaya ‘Davina’ ambaye ni msanii wa filamu alipozungumza na gazeti dada ya hili la Risasi.

Naye muigizaji mwingine wa filamu Bongo, Daud Michael ‘Duma’ alisema: “Kuna wakati ukiona matukio kama haya unaogopa. Unajiuliza ni nani atafuata maana sisi pia ni watu. Kiukweli hali inatisha maana hata mastaa wenzangu tukiwa tunazungumza wanaonekana kabisa wanaogopa kuhusu suala hili!”

MCHUNGAJI AWATAKA WAJIANDAE

Akizungumza na gazeti hili juu ya hofu waliyo nayo baadhi ya wasanii juu ya vifo hivyo, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda-Nyantira jijini Dar, Nabii James Nyakia alisisitiza kuwa, kifo ni lazima kwa wanadamu hivyo ni lazima kujiandaa kwa ajili hiyo. “Kifo ni lazima kwa wanadamu, nawasihi kujisafishia njia na kujiandalia makao mbinguni kwa kukesha wakimuomba maana hakuna anayejua siku wala saa,” alisema Nabii Nyakia.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.