The House of Favourite Newspapers

Vigingi Vya Mbelgiji Yanga Hivi Hapa!

0

KOCHA wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael kwa sasa anapasua kichwa kuona namna gani atakirejesha kikosi chake kwenye ubora wa kupata ushindi kutokana na mfululizo wa sare zinazowaandama kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Wakati sasa Yanga ikiendelea kupambana na sare hizo, akili yao yote ipo Machi 8, mwaka huu ambapo wanatarajiwa kupambana na Simba.

 

Mchezo wa mzunguko wa kwanza katika ligi baina ya timu hizo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar, ulikamilika kwa sare ya mabao 2-2, hivyo mchezo wa Machi 8, utakuwa ni balaa mwanzo mwisho.

Championi Jumatano, linakuletea vigingi ambavyo Mbelgiji huyo vinampasua kichwa ndani ya Yanga katika kuvitatua kabla ya kukutana na Simba.

DAKIKA 270 BANDIKA BANDUA

Kabla ya kumenyana na Simba, Luc atakiongoza kikosi chake kwenye mechi tatu ambazo ni sawa na dakika 270 kusaka ushindi kwanza ikicheza Uwanja wa Taifa.

Leo Jumatano ataanza na Gwambina FC mchezo wa Kombe la FA hatua ya 16 bora, kisha Alliance Februari 29 na Machi 3 ni dhidi ya Mbao. Mechi hizi mbili ni za Ligi Kuu Bara.

 

UBUTU WA SAFU YA USHAMBULIAJI

Luc anapambana na kuunda safu kali ya ushambuliaji lakini kisiki hiki kinazidi kuwa cha mpingo kwake. Yanga haijampata mshambuliaji mwenye urafiki na nyavu.

Ikiwa imecheza mechi 22, imefunga mabao 25 na kinara wa mabao ni David Molinga, ametupia mabao saba, anayemfuatia ni Patrick Sibomana mwenye mabao manne.

Kocha huyo kila akiiangalia safu yake ya ushambuliaji, inampasua kichwa akiifananisha na ile ya Simba inayoongozwa na Meddie Kagere mwenye mabao 14, akifuatiwa na Miraj Athuman na kiungo, Hassan Dilunga ambao kila mmoja ana mabao sita.

SAFU YA ULINZI

Inaonesha kwamba licha ya ubutu wa washambuliaji wake, bado hata mabeki nao wanafungika kwani kwenye jumla ya mechi 22 walizocheza ambazo ni sawa na dakika 1,980 wameruhusu mabao 18.

Safu ya ulinzi ya Yanga ina wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 110 jambo ambalo linamliza Luc anayependa kuona makipa wake wakitoka bila kufungwa.

KUPOROMOKA KWA NIDHAMU

Wachezaji wa Yanga wamekuwa wakishindwa kuzuia mihemko yao wakiwa uwanjani jambo ambalo limekuwa likiigharimu timu hiyo.

Nahodha Papy Tshishimbi ni kiungo muhimu, ana kadi yake moja ya njano aliyoonyeshwa kwenye mechi dhidi ya Coastal Union, asipokuwa makini kuwaongoza wachezaji wenzake ataigharimu timu kwa kupewa adhabu zaidi ya hiyo.

PUMZI KUKATA MAPEMA

Yanga imekuwa na kasi kubwa kipindi cha kwanza kwa kucheza soka la darasani ambalo linawafurahisha mashabiki, lakini wakiingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wakirudi kipindi cha pili wachezaji uwezo wao unabaki vyumbani.

 

Mechi dhidi ya Lipuli, walilinda ngome yao dakika 45 za mwanzo zile za kipindi cha pili waliruhusu bao, lakini mwisho wakashinda 2-1.

Mechi dhidi ya Ruvu Shooting, licha ya kushinda kwa bao 1-0, walicheza soka safi kipindi cha kwanza, kipindi cha pili walipoteana.

MABEKI KUJIFUNGA

Huenda kikawa ni kigingi chepesi lakini hapa makipa wote wa Yanga wanatakiwa kuzungumza vizuri na mabeki wao.

Lamine Moro alijifunga kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, ngoma ilikamilika 1-1 na Ally Mtoni alijifunga mbele ya Azam FC, Yanga ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

 

Luc ameliambia Championi Jumatano kuwa: “Tatizo kubwa ambalo linawasumbua wachezaji wangu kwenye safu ya ushambuliaji ni kushindwa kukaa kwenye nafasi na kumalizia mipira wanayopewa.

“Mabeki ninazungumza nao na nimewaambia kwamba nahitaji kuona tunatoka bila kufungwa, bado kikosi kinaimarika, kila kitu kitakuwa sawa.”

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam

Leave A Reply