The House of Favourite Newspapers

Vigogo Wizara ya Kilimo Wadaiwa Kutafuna Mamilioni!

0

nchemba1Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Lameck Nchemba

Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI

DAR ES SALAAM: Kimbembe Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi! Kuna madai kwamba, wizara hiyo iliyo chini ya waziri wake, Mwigulu Lameck Nchemba (pichani) inadaiwa kutafuna malipo ya kiasi cha shilingi milioni 500 kutoka kwa wasambazaji wa pembejeo za kilimo, Uwazi limechimba.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, pesa hizo zinadaiwa na Kampuni ya Kuzalisha Mbegu, Utafiti na Kusambaza ya Tropical Seeds ambayo ilikopa Benki ya NMB kiasi cha shilingi milioni 150 kwa ajili ya kupata tenda wizarani ya kusambaza pembejeo za kilimo kwenye vikundi vya wakulima Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Iringa na Ruvuma ambapo wizara ingelipa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa kazi hiyo.

Ilielezwa kuwa, deni hilo ambalo wizara hiyo inadaiwa ni la msimu wa kilimo wa mwaka 2014/ 2015 ambapo hadi sasa walengwa hawajalipwa malipo yao na kusababisha benki hiyo kutaka kutaifisha dhamana zao.

 Mnyetishaji wetu alisema habari za ndani ni kwamba, hazina imeshatoa pesa hizo kwenda kwenye wizara hiyo ili iwalipe wadau hao lakini anahisi kuwa, zimetafunwa na baadhi ya vigogo wa wizara hiyo.

Joseph Alikamkalaba wa Sumbawanga, yeye anawakilisha wenzake wa Iringa, Njombe Mbeya na Morogoro anasema kuwa, wanaidai Tropical Seeds zaidi ya shilingi milioni 50 za pembejeo za kilimo ambapo nao wanasema wanaidai wizara shilingi milioni 500.

Alisema kuwa, kila wanapompigia simu Mkurugenzi wa Tropical Seeds, Odran Lazaro Chaula kumkumbushia madai hayo wanajibiwa kuwa, Wizara ya Kilimo haijawalipa ingawa alidai wanazo taarifa kuwa, hazina imeshatoa pesa hizo lakini zimekwama mahali.

 “Kila tukifuatilia kule Tropical wanatuambia wizara bado haijawalipa pesa zao ili watulipe na sisi hii sasa ni hatari kwa sababu tulikopa benki na dhamana yetu inafikia ukomo karibuni. Tuna wasiwasi kuwa tutafilisiwa,” alisema Alikamkalaba.

Uwazi lilimtafuta mkurugenzi huyo, ambaye alikiri kudaiwa na watendaji mbalimbali wa mikoa hiyo lakini alisema kuwa, anasubiri malipo yatoke wizarani.

“Mimi sijadhulumu mtu kwani ndiyo nashughulikia malipo hayo wizarani, ninadai pale shilingi milioni 500, nadhani watanilipa hivi karibuni na nitatatua tatizo hilo,” alisema Chaula.

Wiki iliyopita, Uwazi lilitinga Wizara ya Kilimo ili kukutana na Katibu Mkuu, Dk. Florens Turuka lakini liliambiwa hayupo, ila kwa habari za kikazi wa kuonana naye ni Afisa Habari Msaizidi, Samkana Simkoko.

Hata hivyo, afisa habari huyo aliliunganisha Uwazi kwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Pembejeo aliyejitambulisha kwa jina moja la Ngonyani.

Mkurugenzi huyo alikiri kulitambua deni hilo pia kuitambua Kampuni ya Tropical Seeds na kusema kuwa, pesa hizo zitalipwa ila kwa sasa zipo katika mchakato kwa vile kuna vitu vingi vitazingatiwa katika malipo.

“Wizara  haijatafuna pesa yoyote kwani tunawaheshimu sana hao, tumefanya nao kazi vizuri sana. Kwa hiyo tutawalipa tu hakuna shaka juu ya hilo tupo katika mchakato huo na umefika pazuri. Hata juzi walikuja, tukaongea nao,” alisema Ngonyani.

Leave A Reply