The House of Favourite Newspapers

Vitu Vitano Muhimu Anavyohitaji Mteja Kutoka Kwako

0

RAFIKI yangu mpendwa, kuanzisha biashara ni jambo moja halafu kuifanya biashara hiyo ikue, iwe bora na yenye mafanikio hilo ni jambo lingine.

 

 

Najua ulijitahidi sana kuanzisha biashara na kweli umefanikiwa kuanzisha lakini hivi sasa ndio unajisahau na hatimaye kuishia hapo, na kwa sababu umeishia hapo basi biashara zako hushindwa kuwa imara kwa sababu biashara hizo hukosa usimamizi mzuri ikiwa ni pamoja na mambo mengine ya msingi sana ambayo kwa ujumla ndio hufanya biashara kuwa bora.

 

 

Mteja anapokuja katika biashara yako siyo kwamba kakuona wewe tu peke yako ndio unayetoa hiyo huduma hapo bali kuna kitu kimemvutia kuja kwako au pengine yupo katika uchunguzi binafsi wa ni wapi ataweza kupata mahitaji yake ambayo ni bora tena kwa wakati muafaka.

 

 

Ni mara kadhaa sasa umekuwa ukikimbiwa na wateja kutokana na sababu mbali mbali ambazo pengine zingekuwa ni funzo kwao lakini kwa kuwa hujali hilo basi wateja wote hukukimbia na hatimaye unajikuta pengine ukifunga biashara hiyo au kuamua kuhama tu eneo hilo.

 

 

Je! Nini mteja anatarajia kupata kutoka kwako? Leo nitakuambia ni mambo gani ambayo mteja hutamani na hata kutaka sana kuyapata anapokuja kwako.

 

 

Moja, mteja anatarajia kupata huduma bora tena kwa wakati. Ndio, yaani kama hutoi huduma bora hata kama unatoa kwa wakati basi huyo mteja jua kabisa kuwa umeshampoteza maana akishagundua tu kuwa huduma zako zipo chini ya kiwango yaani hazina ubora basi ndiyo umeshampoteza tayari.

 

 

Na kama huduma zako zipo katika ubora lakini hutoi huduma hizo kwa wakati, yaani mteja akija kwako anakaa au atasimama mpaka atachokea kwako basi jua tu kuwa mteja huyo naye umeshampoteza.

 

 

 

Mbili, lugha nzuri na yenye staha. Unatambua kuwa watu hatufanani, kuna mteja ambaye yeye hata ukimjibu hovyo lakini huduma zake anapata kwa wakati na ni huduma bora anaweza kuvumilia au kutojali maneno yako lakini kuna mteja mwingine yeye anaona sasa lugha yako kwanza ni chafu yaani siyo nzuri hata kidogo kwake na akiangalia tena pesa ni yake, yaani ananyanyasika kwa pesa yake mwenyewe?

 

 

Mteja huyo huona ya nini aje kwako wakati wapo watu wengi tu wanaotoa huduma kama zako tena bora sana kuliko huduma zako, kitendo cha mteja huyo ile kukuona tu wewe kwanza anajisikia kichefu chefu akikumbuka tu maneno yako machafu, matokeo yake ni kwamba mteja huyo huamua kukuhama.

 

 

TATU, UAMINIFU

Ukitaka kugundua kuwa uaminifu ni kitu muhimu sana jiulize hivi ni nani anapenda kukaa au kufanya kazi na mtu ambaye siyo mwaminifu?

 

 

Jibu ni hakuna. Sasa wewe mteja kusahau chenchi yake kwa bahati mbaya na wewe unalijua hilo badala ya kumuita umpe au hata kumtunzia ili akikumbuka aje umpe lakini wewe hufanyi hivyo, unaona hapo ndiyo pakupatia, utauwa biashara yako. Nne, mtu mstaarabu na mwenye hekima.

 

 

Bila shaka kuwa na hekima tu kutafanya watu wapende hata kuwa karibu na wewe. Sasa wewe ni mzulumishi, jeuri, mkorofi, unaropoka kila kitu halafu ni mgomvi kweli kweli. Wewe umeshawahi kusikia wapi mtu anaetaka kufanya kazi na mtu mgomvi? Kila mtu anataka kufanya kazi na mtu mstaarabu hivyo amua kuwa hivyo mara moja kama ulipotea njia.

 

 

TANO, UHURU.

Kama ulikuwa hulijui hili basi ndio ulijue kuanzia sasa kuwa mteja anahitaji uhuru. Sasa mteja ndio kafika tu unaanza kumpelekesha hata hajaona kama anachokitaka kipo au la, hata hajajua ubora wa bidhaa zako upoje wewe umeshamkumrupusha,unamyima uhuru hata wa kujifikiria vema yeye mwenyewe, utauwa biashara yako mara moja.

 

Amua kubadilika sasa.

Ondoka na hili, Unaweza kuifanya biashara yako iwe bora au isiwe bora, kama unataka wateja waje kwako kwa wingi, fanyia kazi hayo mambo muhimu uliyojifunza hapa, kwa hakika utafanya watu wapende sana kuja kwako kwani wataona kuwa kwako ni sehemu ambayo wanapata huduma bora, kwa wakati ikiwa ni pamoja na lugha nzuri ya kuwavutia.

 

 

Uwe na siku njema sana na yenye mafanikio makubwa.Ni mimi rafiki na Mwalimu wako, Mseco Kidee.Unaweza kuwasiliana nami kwa namba 0672134512.

Leave A Reply