The House of Favourite Newspapers

Vodacom Yakabidhi Kompyuta Zenye Thamani Ya Sh. 115m Kwa Shule 16 Kilimanjaro

0
Baadhi ya wanafunzi wa moja ya shule zilizonufaika na msaada wa kompyuta kutoka kampuni ya Vodacom Tanzania wakionyesha moja ya kompyuta hizo kwenye hafla ya makabidhiano yaliyofanyika siku ya Alhamisi Moshi mjini.

Kilimanjaro – Februari 23, 2023. Katika jitihada za kukuza sekta ya elimu na kufanikisha lengo lake la kujenga jamii ya kidijitali, kampuni ya teknolojia na mawasiliano nchini, Vodacom Tanzania PLC imekabidhi kompyuta zenye thamani ya shilingi milioni 115 kwa shule 16 zilizopo wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ili kuwezesha wanafunzi na walimu kupata maudhui ya elimu ikiwamo vitabu vya kiada na ziada pamoja na vingine vingi bila malipo yeyote.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea baadhi ya vifaa hivyo iliyofanyika shule ya Sekondari Mrereni iliyoko Kilema Kusini, Afisa Tarafa wa Vunjo Magharibi Khamisuu Uledi aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mh. Kisare Makori ameishukuru na kuipongeza Vodacom Tanzania kwa jitihada zake za kuhakikisha wanakuwa kinara katika utoaji wa elimu kwa njia ya mifumo ya TEHAMA.

Meneja mauzo wilaya ya Moshi na Rombo, wa Vodacom Tanzania Kanankira Nanyaro (kulia) akikabidhi kompyuta kwa mwalimu wa kompyuta wa shule ya Sakayo Mosha, Ivan Temu kwenye hafla fupi ya makabidhiano ambapo kampuni ya Vodacom imetoa msaada wa kompyuta kwa shule 16 mkoani Kilimanjaro.

“Elimu katika dunia ya sasa imebadilika kwa kiasi kikubwa kutoka kutegemea walimu kuingia madarasani na vitabu mpaka shughuli zote kuhamia mtandaoni. Ningependa kuwapongeza Vodacom Tanzania kwa kutoa msaada huu mkoani kwetu ambao utakuwa msaada kwa walimu ambapo utawarahisishia utendaji wao wa kazi na hili litafanikiwa kwa kuwa tumepata vifaa vya kiteknolojia kama vile kompyuta hizi mlizozikabidhi leo.” Alisema Mh. Uledi.

“Ningependa kutoa wito kwa shule ambazo zimekabidhiwa kompyuta hizi kuzitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa ili kuendeleza kuboresha mfumo wa utoaji wa elimu nchini. Bila shaka zitakuwa chachu kwa walimu kusaidia ufanisi katika ufundishaji wao,” alisema Mh. Uledi.

Meneja mauzo wilaya ya Moshi na Rombo, wa Vodacom Tanzania Kanankira Nanyaro (kulia) akikabidhi kompyuta kwa mwalimu wa kompyuta wa shule ya Sakayo Mosha, Ivan Temu kwenye hafla fupi ya makabidhiano ambapo kampuni ya Vodacom imetoa msaada wa kompyuta kwa shule 16 mkoani Kilimanjaro.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya aliongeza, “Sisi kama serikali tunawapongeza sana Vodacom Tanzania na tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika jitihada zao za kuendelea kuboresha upatikanaji wa elimu nchini. Lakini pia tunatoa wito kwa wadau wengine kuzidi kujitokeza zaidi kwani bado jitihada za pamoja zinahitajika ili kuendana na kasi ya teknolojia duniani.”

Katika hafla ya makabidhiano hayo jumla ya kompyuta 10 zilikabidhiwa kwa shule 5 ambazo ni Shule za Sekondari Marlex, Sakayo, Mrereni, Mangoto, na Mwika. Kwa ujumla shule 16 zitanufaika mkoani Kilimanjaro kwa kupatiwa vifaa vya Tehama vyenye thamani ya shilingi milioni 115, Shule hizo ni pamoja na Kirongo, Mashati, Kwakoko, Mkuu, Tarakea, Nanjara, Mbomai, Umarini, Ndueni, Motamburu na Urauri, ambapo takribani shule 300 nchini zimo ndani ya mpango huo.

Akielezea malengo ya kukabidhi vifaa hivyo Mkuu wa kanda ya kaskazini, Vodacom Tanzania PLC, Bw. George Venanty amesema kuwa, “Ni fahari kwetu kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika upatikanaji wa elimu bora nchini kwa kuwawezesha walimu na wanafunzi kujipatia vitabu bila ya malipo kwa njia ya mtandao.”

“Kompyuta hizi ambazo tumezikabidhi leo ni mwendelezo wa program ya e-Fahamu tuliyoizindua tangu mwaka 2017 ambapo mpaka sasa takribani wanafunzi 300,000 wananufaika nayo. Tunaamini kuwa vifaa hivi vitawasaidia jamii ya shule hizi za Sekondari kwa kuwarahisishiakazi na majukumu yao ya kila siku,” alisema Bw. Venanty.

Mkuu huyo wa Kanda ya Kaskazini aliongezea, “kama Vodacom tunaishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana nasi katika sekta tofauti za maendeleo ikiwemo elimu ambayo ni nguzo kwa ukuaji wa taifa lolote duniani. Tutaendelea kutimiza malengo ambayo tulijiwekea wakati tunazindua program hii ili kuona kila mwanafunzi nchini anapata fursa sawa ya kupata elimu bora.”

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mrereni iliyopo Kilema Kusini, Bi. Mary Gladstone Masuki aliishukuru kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kutekeleza kwa vitendo adhma yake ya kuwa kampuni inayoongoza kwa mawasiliano ya kiteknolojia na dijitali nchini huku ikizinufaisha jamii za Watanzania kwenye nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

“Kwa niaba ya uongozi wa shule na wanafunzi wote wa Sekondari ya Mrereni, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa serikali na kampuni ya Vodacom kwa kutuchagua kuwa miongoni mwa shule zilizonufaika na mpango huu wa kutusaidia kupata vitendea kazi ambavyo vitaturahisishia utendaji kazi wa majukumu yetu ya kila siku,” alihitimisha Mwl. Masuki.

Programu ya bure ya e-Fahamu ilianzishwa na Vodacom Foundation mnamo mwaka 2017 kwa lengo la kuwasaidia walimu na wanafunzi kupata vitabu vya ziada na kiada kwa shule za msingi na sekondari ambayo inafuata mitaala ya kutoka maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania na masomo ya kimataifa bure kwa njia ya mtandao. Lengo la Tovuti hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Mnamo mwaka 2022, Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na taasisi ya African Child Projects (ACP) walizindua rasmi upanuzi wa mradi wa uunganishwaji wa shule kidijitali, mradi uliolenga kuunganisha shule kadhaa nchini kwenye mtandao wa intaneti.

Chini ya makubaliano ya ushirikiano huo, taasisi ya ACP ilitekeleza shughuli hizo katika shule 50 za umma zilizoko kwenye mikoa 10 nchini. Shule hizo zilipokea jumla ya kompyuta 186, tablet 246 pamoja na kupata vifurushi vya intaneti vya 50GB kila mwezi kwa mwaka mmoja.

Leave A Reply