The House of Favourite Newspapers

Waamuzi: Tuna ‘Stress’ za Mishahara

0

“TUNa stress, hatujalipwa mwaka mzima.” Hiyo ni kauli ya mmoja wa waamuzi wanaochezesha mechi za Ligi Kuu bara msimu huu akifungukia sakata la baadhi ya waamuzi kuonekana wakiboronga kwenye mechi za hivi karibuni.

 

Hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko makubwa kwa waamuzi hasa wanaochezesha mechi za Ligi Kuu Bara kufanya maamuzi yasiyo sahihi huku kubwa likiwa ni kwenye kutafsiri sheria ya kuotea.

 

Wakati sakata hilo likiendelea, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juzi lilitangaza kumfungia miaka mitatu mwamuzi namba mbili, Kasim Safisha aliyezua utata katika mchezo wa ligi kuu kati ya Simba na Namungo kwa kukubali bao lililofungwa na Meddie Kagere wa Simba ambalo lilionekana mfungaji kabla ya kufunga alikuwa ameotea.

Akizungumza na Championi Jumamosi kwa sharti la kutoandikwa jina lake, mmoja wa waamuzi hao alisema: “Unajua nini, mara ya mwisho tumelipwa Januari, mwaka jana, hadi leo Februari 2020, hatujalipwa tena.

 

“Yaani hivi sasa tuna stress (msongo) za mishahara ndiyo maana unaona kunatokea matatizo kama hayo kwa sababu tunachezesha mechi huku mawazo yakiwa nje ya kile tunachokifanya, tunaziwaza familia zetu, mimi binafsi nadai zaidi ya milioni moja, wapo ambao wanadai fedha nyingi zaidi yangu.

 

“Kwa bahati mbaya pia tumekuwa hatupewi majibu mazuri na viongozi pindi tunapojaribu kudai maslahi yetu, waamuzi tumekuwa tukijigharamia wenyewe nauli, malazi na chakula pindi inapotokea umepangwa kwenda kuchezesha mechi nje ya mkoa wako.

 

“Watu watusamehe tu, hatufanyi makusudi, inatokea tu bahati mbaya kama ilivyo kwa binadamu wengine, kwa sababu mtu anakuwa anawaza atarudije nyumbani huku akiwa hana fedha na wakati mwingine tunakopa ili tuweze kusafiri,” alisema mwamuzi huyo.

 

Championi Jumamosi lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto kuweka sawa mzani juu ya madai hayo ya malipo ya waamuzi kwa muda mrefu ambapo alikiri kweli wanadaiwa. “Kweli waamuzi wanatudai, hivi sasa tunafanya mchakato wa kuwalipa stahiki zao zote, lakini hilo lisiwe sababu ya wao kuchezesha vibaya,” alisema Mguto.

Leave A Reply