The House of Favourite Newspapers

Waangola Wameisha… Simba Yakodi Dege la Kishua, Watatu Waachwa Dar

0

KATIKA kuhakikisha wanategua mitego yote ya fitina za nje ya uwanja na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Simba umebainisha kwamba, kikosi chao kinatarajiwa kuondoka keshokutwa Jumamosi alfajiri na ndege ya kukodi mpaka Angola.

 

Jumapili ya wiki hii, Simba inatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Novemba 11, nchini Angola kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao, Clube Desportivo 1º de Agosto.

 

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, uongozi wa timu hiyo umepenyezewa taarifa kutoka Angola kuwa wenyeji wao wana mipango ya kuanza vita nje ya uwanja, hivyo mabosi fasta wameshtukia mchongo na kupangua fitina hizo kibabe.

 

“Unajua mpira wa Afrika kwa kiasi kikubwa bado unaendeshwa na mipango ya nje ya uwanja, wote tunajua kilichowatokea Namungo walipokwenda Angola, hivyo uongozi tayari umepata taarifa kuwa wapinzani wetu wana mpango wa kuanza vita nje ya uwanja.

 

“Hii ndiyo sababu kubwa ya timu kupanga kuondoka Jumamosi wakati mchezo wetu utakuwa Jumapili, tena timu imepanga kuondoka na ndege binafsi hii yote ni katika kuhakikisha tunakwepa fitina zote.”

 

Akizungumzia safari yao, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Ni kweli kikosi kinatarajiwa kusafiri Jumamosi kwa ndege ya kukodi moja kwa moja kwenda Angola kwa ajili ya mchezo huo tukiwa tumechukua tahadhari zote dhidi ya wapinzani, kuhakikisha tunatinga makundi.

 

“Baada ya mchezo huo, msafara utarejea nyumbani kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa marudiano ambao tunaamini utakuwa mgumu, hivyo ni lazima tuanze maandalizi mapema.

 

“Nimesikia watu wengi wakihoji sana uamuzi wetu wa kwenda siku moja kabla ya mchezo, ila ukweli niwaambie tu kuwa, tayari uongozi ulishapitia mazingira yote ya eneo ambalo tunaenda kuchezea, hivyo tumegundua kuna ulazima wa kwenda siku hiyo na mambo yatakuwa sawa.

 

“Kuna watu walitangulia mapema Angola ili kuona mbinu za wenzetu ikiwa sambamba na uchezaji na mapokezi yao yanavyokuwa, tumejiridhisha na kuamua kuchukua ndege binafsi ili kuepuka usumbufu wowote kama tungeenda mapema kwa kuunga ndege.”

Wakati huohuo, Ally alibainisha kwamba watawakosa wachezaji watatu kwenye msafara huo kutokana na kutokuwa fiti ambao ni Jimmyson Mwanuke, Peter Banda na Shomari Kapombe.

WAANDISHI: JOEL THOMAS, WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

EXCLUSIVE: MWENYEKITI wa BODI SIMBA ‘TRY AGAIN’ AFUNGUKA ISHU ya DEJAN KUONDOKA SIMBA, MGUNDA..

Leave A Reply