The House of Favourite Newspapers

Wabunge 15 Waliohenyeshwa Mahakamani 2018

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,  Zitto Kabwe.

TUNAKARIBIA kuufunga 2018 huku ukiacha historia kwa wabunge 15 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT Wazalendo ambao walipandishwa kizimbani katika mahakama mbalimbali nchini. Wanasiasa hao wa upinzani nchini wameendelea kutumia muda wao mwingi kulalamika kile wanachokiita kuminywa kufanya shughuli zao za kisiasa.

 

Wakati huohuo, wanasiasa hawa wamejikuta upande mbaya wa sheria ambapo wapo wengi hivi sasa wanaozongwa na utitiri wa kesi za uchochezi. Kinachoendelea kuwashangaza wengi pia si tu idadi ya kesi zinazowakibili, lakini pia idadi ya wanasiasa wanaokabiliwa na kesi hizo.

 

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo amekuwa ni miongoni mwa watu waliojikuta matatani kwa misingi ya sheria ya makosa ya takwimu. Sheria hii imekuwa ikipingwa vikali na wanaharakati kuwa ni kandamizi kwa watoaji na wapokeaji wa taarifa.

Mchungaji Peter Msigwa wa Jimbo la Iringa Mjini.

Lakini mwaka huu Zitto Kabwe alipokuwa katika ziara ya kichama katika mikoa mbalimbali nchini, alijikuta matatani na vyombo vya usalama kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kosa la kufanya mikutano ya kisiasa bila kuwa na kibali rasmi cha Polisi.

 

Chama kikuu cha upinzani cha Chadema ndicho kinachoonekana kuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wake waliopandishwa mahakamani mwaka huu kutokana na kuwa na kesi mbalimbali za uchochezi. Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, kuna wabunge 13 wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali. Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema, Tundu Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu, anakabiliwa na kesi sita.

Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la kazi zake za usanii, Sugu ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini.

Kesi zote zinahusiana na uchochezi. Lissu inasemekana kuwa ndiye mwanasiasa aliyekamatwa mara
nyingi zaidi ya wengine. Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la kazi zake za usanii, Sugu ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini, alitiwa hatiani na kutupwa gerezani kwa kipindi cha miezi mitano baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kutumia lugha za matusi dhidi ya Rais Dk John Magufuli.

 

Kwa upande wake, Halima Mdee, Mbunge wa Kawe jijini Dar, yeye anazo kesi nne, zote zikiwa za uchochezi ikiwemo ile aliyotuhumiwa kutumia lugha mbaya kumpinga Rais Magufuli baada ya kutangazwa kwa marufuku ya kuwaruhusu wanafunzi wa kike kurudi shuleni mara wapatapo ujauzito.

 

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema yeye anakabiliwa na kesi nne pia huku zote zikiwa za uchochezi. Siku za nyuma Lema aliwahi kukaa mahabusu kwa muda wa siku 121 kwa kosa la uchochezi. Hivi sasa Lema amekuwa akihudhuria mahakamani mara kwa mara. Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ana kesi mbili za uchochezi.

Halima Mdee, Mbunge wa Kawe jijini Dar

Kwa sasa yupo gerezani Segerea baada ya kufutiwa dhamana na mahakama akiwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya. John Mnyika, Mbunge wa Kibamba jijini Dar kwa upande wake mwaka huu alionja joto ya jiwe baada ya kutakiwa kuhudhuria polisi kila wiki tangu jaribio la kufanyika kwa maandamano ya chama hicho kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi kupinga walichodai kunyimwa fomu za mawakala. Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, aliwahi kushikiliwa na Polisi kwa kosa la kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake, jambo ambalo Polisi walidai kuwa lilikuwa ni uvunjifu wa sheria, baadaye alifunguliwa kesi.

 

Licha ya kuwa wanaharakati na asasi za kutetea haki za binadamu kuwa mstari mbele kuwatetea
wanasiasa hao bado Serikali hiyo imekuwa ikibaki kwenye msimamo wake kuwa wanasiasa hao wanavunja sheria. Katika uchunguzi zaidi wa safu hii imebainika kuwa wabunge wengine ‘walioonja’ kesi mwaka huu ni Peter Lijualikali wa Jimbo la Kilombero, huyu aliwahi kufungwa, akakata rufaa na kushinda, Susan Kiwanga wa Jimbo la Mlimba na Zubeda Sakuru wa Viti Maalum.

 

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa wa Jimbo la Iringa Mjini, Kunti Yusuph wa Viti Maalum, Cecil Mwambe wa Jimbo la Ndanda na Saed Kubenea wa Jimbo la Ubungo. Wengine wenye kesi za uchochezi au kuikashfu Serikali au viongozi waliopo madarakani ni Pascal Haonga wa Jimbo la Mbozi na Frank Mwakajoka wa Jimbo la Tunduma.

 

Kwa upande wake Mchungaji Msigwa, yeye anakabiliwa na kesi kadhaa ikiwamo ile iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa akishtakiwa kwa kesi mbili. Mbunge huyo ni mshtakiwa wa saba katika kesi hizo, kesi moja iliyompeleka mahakamani hapo ni ile ya madai ya kuchoma moto nyumba ya Mary Tesha aliyokuwa akiishi Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Alphonce Muyinga na ya pili, mbunge huyo na wenzake sita wanadaiwa kupanga njama ya kutenda uhalifu kinyume cha sheria.

Comments are closed.