The House of Favourite Newspapers

Wachimbaji Dhahabu Wachangishana Fedha kwenda Kumuona Waziri

0
Sehemu ya wachimbaji wakifuatilia yanayoendelea kwenye mkutano huo.

WACHIMBAJI wadogo wa madini ya dhahabu kutoka vijiji mbalimbali vilivyopo katika Kata ya Saza wilayani Songwe mkoani Songwe, wamechangishana fedha kwa ajili ya kusafirisha baadhi ya wajumbe wa chama chao kwenda jijini Dodoma kuonana uongozi wa Wizara ya maliasili na utalii kutoa kilio chao kuhusu mpaka wa eneo uchimbaji wa madini.

Hatua hiyo imekuja baada ya eneo la mpaka wa Patamela kusogezwa mbele ya mlima wa Elizabeth kinyume na taratibu na kusababisha wachimbaji hao kukosa maeneo ya machimbo.

Wakizungumza na GLOBAL walisema hali hiyo imesababisha waanze kuokota mawe maeneo ya misituni na kusababisha wachimbaji hao kukumbana na kipigo kutoka kwa maafisa misitu pindi wanapokutwa kwenye maeneo hayo.

Viongozi wakikusanya michango hiyo.

Mmoja wa wakazi hao Mapambano Mwakagile alisema baada ya kuhangaika sehemu mbalimbali kwa viongozi wa ngazi za wilaya bila majibu wameamua kuchangishana fedha kusaka nauli ya kwenda Dodoma kuonana na Katibu mkuu wa wizara hiyo.

Katibu wa chama cha wachimbaji wadogo Saza, Shamsi  Abeid alisema hatua ya watu hao wa maliasili kuwabana na kuwapa adhabu pindi wanapowakuta kwenye maeneo ya misitu inatokana na kusogezwa kwa mpaka wa awali hivyo waliamua kuchangisha fedha kwenda kwa waziri mwenye dhamana ili wapate msaada baada ya kukosa msaada ngazi ya wilaya.

Afisa maliasili wilayani humo, Ally Mkoma alipotafutwa ofisini kwake kujibu malalamiko ya maafisa wake kuwasumbua wananchi hakuwepo ofisini na alipopigiwa simu zaidi ya mara tano hakupokea ambapo wachimbaji hao bado wanaendelea na harakati zao kutafuta fedha kwa ajili ya safari kwenda Dodoma kwa katibu wa wizara hiyo ili kupata msaada.

Leave A Reply