The House of Favourite Newspapers

Wadau Wakutanishwa Katika Warsha ya Kujenga Uelewa Katika Sekta ya Kidijitali

0

 

Ziada Seukindo, Meneja Programu wa Jamii Forums

 

Shirikisho la Wadau Wanaotetea Haki za Kidigitali Tanzania (Digital Rights Coalition), limeandaa Warsha ya kujenga uelewa kwa Wadau kuhusu Sheria, Sera na Kanuni zinazosimamia Masuala ya Kidigitali nchini Tanzania pamoja na kuwezesha majadiliano ya changamoto na fursa zilizopo.

Warsha hiyo imefanyika leo Jumanne Mei 30, 2023 katika Hoteli ya Protea Jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali.

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja Programu wa Jamii Forums, Ziada Seukindo, alisema: “Tunashiriki mkutano huu leo ambao umeratibiwa na Shirikisho la Wadau wa Kutetea Haki za Kidigitali lililoanzishwa Novemba 2022 kwa ajili ya Uchechemuzi wa Haki za Kidigitali.

 

Carol Ndosi, mwanzilishi wa The Launch Pad

 

“Wadau wa Shirikisho hili ni Taasisi ambazo zimeungana ili kuongelea Haki za Kidigitali kwa pamoja ili kuwa na sauti ya pamoja ambayo itasikika vizuri zaidi.

“Tunaangazia zaidi Sheria, hasa kwa kuwa tunaamini kwamba ndizo zitakazotoa haki mbalimbali lakini pia zitaweka mazingira rafiki ya watu kutumia vizuri fursa ambazo zipo mtandaoni.

“Tunafanya uchechemuzi wa Haki za Kidigitali kwa sababu zama hizi ambazo ambapo Watu wengi tunatumia vifaa vya kidigitali na mtandao na majukwaa ya kidigitali, utu wetu upo hatarini.

 

 

“Leo hii picha zako, taarifa zako binafsi ziko mtandaoni ambapo Mtu anaweza kuzitumia kwa namna yoyote ambayo inaweza kukuathiri au kuathiri Watu wa karibu yako.

“Tukumbuke kuwa Watu wanajipatia kipato kutokana fursa zinazopatikana mtandaoni, ambapo wanaweza kuathiriwa ikiwa Sheria au ‘Digital Space’ haipo vizuri.

“Hivyo Mkutano huu ni wa Wadau kujadili changamoto na fursa katika Ulimwengu wa Kidigitali, pia kupendekeza njia za utatuzi wa changamoto hizo ambapo baadaye tutaziwasilisha kwa Watu ambao tunaamini wanaweza kuzifanyia kazi.

 

 

“Kuna changamoto mbalimbali katika Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ikiwemo Tume inayosimamia Ulinzi wa Taarifa Binafsi (The Data Protection Commission), imepewa nguvu kubwa sana ambazo zinaweza kuathiri utendaji kazi wa Taasisi au Watu mbalimbali.

“Tume imepewa uwezo wa kuingia kwenye jengo lolote, na kuchukua kifaa chochote ambacho wao wanahisi kina taarifa wanazozihitaji bila kuwa na kibali chochote na pia imepewa nguvu za kutozingatia Sheria zozote wakati wanatimiza majukumu yao.”

Kwa upande wa Carol Ndosi ambaye ni muanzilishi wa The Launch Pad, amesema: “Haki za Kidigitali ni Haki za Binadamu. Haki za Kidigitali zinatetea Uhuru wa Kujieleza, Haki ya Kukusanyika na Haki nyingine za Binadamu.

“Kama Wadau, tunachopambania ni kuondoa Mstari uliopo kati ya Haki za Binadamu na Haki za Kidigitali.”

Leave A Reply