The House of Favourite Newspapers

Wadhamini Wamuomba Mbowe Amlete Lissu Mahakamani

0

WADHAMINI wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wamemwandikia barua Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ya kumuomba awasaidie kumleta mshitakiwa Lissu nchini.

 

Wakati wadhamini hao wakiandika barua hiyo, Mahakama imeendelea kusisitiza kuwa inamuhitaji Lissu mahakamani ili shauri linalomkabili yeye na wenzake wanne liweze kuendelea katika hatua nyingine.

 

Mdhamini wa Lissu, Robert Katula amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wamefanya juhudi za kuwasiliana na mshitakiwa na mara ya mwisho aliwaeleza kuwa anawasiliana na Wakili wa chama chake.

 

Ameeleza kuwa baada ya kuwaeleza hayo mpaka leo hawajafanikiwa kupata jibu lolote ndipo walipoamua kumuandikia barua Mbowe ili awasaidie kumleta mshitakiwa huyo nchini ili aweze kufika mahakamani, hivyo wanaomba kupewa muda wa kufatilia suala hilo.

 

Wameeleza kuwa wakati wanamdhamini Lissu hawakujua kama atapigwa risasi na kuondoka hapa nchini. Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto amedai kuwa jukumu la kuhakikisha mtuhumiwa huyo anafika mahakamani ni la wadhamini wenyewe na si la mtu mwingine.

 

Pia alidai wadhamini hao walikubali kumuwekea dhamana mshitakiwa hata kabla ya kuugua na walilidhia mtuhumiwa huyo hatasafiri na kuongeza kuwa walikuwa wanajukumu la kujitoa katika nafasi hiyo kabla Lissu hajasafiri.

 

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba alisema suala bado linabaki pale pale kuwa mshitakiwa huyo aletwe mahakamani kwani kupigwa kwake risasi hakumzuii kufika.

 

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2020 na kusisitiza Lissu kufika mahakamani na kwamba dhamana kwa washitakiwa wengine inaendelea. Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

 

Leave A Reply