The House of Favourite Newspapers

WAKATI MO AKITAFUTWA, MAMA ATEKWA, AUAWA KIKATILI

WAKATI tukio la kutekwa kwa mfanyabishara bilionea namba moja nchini, Mohammed Dewji ‘MO’ likiwa bado ni la moto na msako mkali ukiendelea, tukio lingine baya limetokea mkoani hapa.

NI MAMA MFANYABISHARA

Ni tukio la mama mfanyabishara Elizabeth Kunambi naye kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kisha kuuawa kikatili na mwili wake kutupwa kwenye nyumba inayoendelea kujengwa (pagala). Tukio hilo la kutisha lilijiri hivi karibuni, majira ya saa 3:00 usiku kwenye Mtaa wa Maendeleo Kata ya Lukobe nje kidogo ya Mji wa Morogoro.

 

Baada ya kutokea kwa mauaji hayo yaliyoacha simanzi na mshtuko mkubwa kwa wakazi wa Kata za Lukobe na Kihonda, Ijumaa Wikienda lilifika eneo la tukio na kushuhudia umati mkubwa ulioongozwa na madenti wa Shule ya Sekondari ya Kihonda wakishiriki mazishi ya mama huyo.

 

MJI WAZIZIMA

Mazishi hayo yalifanyika katika Makaburi ya Kanisa la Mtakatifu Monica almaarufu Makaburi ya Mangweha na kusababisha mji kuzizima kwa majonzi. Akizungumza na Ijumaa Wikienda kwa uchungu, mama mzazi wa marehemu Elizabeth, Betha Simon alikuwa na haya ya kusema:

 

“Siku ya tukio mwanangu anayefanya biashara ya sabuni alinipigia simu muda wa saa 3:00 usiku akitokea kwenye mizunguko yake ya biashara. “Nilimwambia nipo maeneo ya Manyuki-Transfoma, akaja akiwa na madaftari matatu mapya aliyomnunulia mwanaye na chipsi ambazo alidai anawapelekea watoto wake.

“Basi, baada ya mazungumzo yetu kumalizika, tuliagana na kila mtu alielekea kwake. “Cha ajabu asubuhi ninapokea taarifa kwamba mwanangu ametekwa. “Kweli tulihangaika sana kumtafuta, lakini hatukumpata hadi siku ya pili alipopatikana akiwa ameuawa kikatili na mwili wake kutupwa kwenye pagala lililopo jirani na ofisi ya Kata ya Lukobe.

 

“Nilifika eneo la tukio na kukuta mwili wa mpendwa mtoto wangu ukiwa hauna nguo na kuonesha kwamba alipata mateso sana kutoka kwa watekaji kabla ya kuamua kumuua, kiukweli sitaki kukumbuka ile picha kwa sababu mwili ulikuwa kwenye hali mbaya sana,” alisema mama huyo na kuangua kilio.

 

MTOTO WA MAREHEMU

Kwa upande wake mtoto mkubwa wa marehemu, Winnifrida Romanus ambaye anasoma kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kihonda alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema: “Nakumbuka wanafunzi wote tulipewa barua za kikao cha wazazi ambacho kilifanyika Jumatano (wiki iliyopita), nilifika na barua hiyo nyumbani ambapo tunaishi na mama tu, tupo watoto watatu na kila mtu na baba yake.

 

MAMA HARUDI

Ilipofika saa 4:00 usiku nikawa naona mama harudi, nikaenda kwa jirani kuazima simu. Nilipiga sana namba ya mama, ikawa inaita tu haipokelewi, nikazidi kupiga zaidi ya mara tano bila kupokelewa.

 

“Baadaye simu ya mama ikazimwa. “Kuona hivyo, huku tukiwa na njaa, niliwaingiza ndani wadogo zangu, Frank Simon na Elia Evarist, tukalala. Kulipokucha tulianza kumtafuta mama yetu hadi siku inayofuata, tukaambiwa mama yetu tunayemtegemea kwa kila kitu akiwa ameuawa. “Kwa uchungu sikuwa na ujasiri wa kwenda eneo la tukio, kwa sasa nimebaki na kumbukumbu ya picha ya mama tu,” alisema mtoto huyo na kuangua kilio.

 

SERIKALI YA MTAA

Kaimu mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Pasisi Msambili Kidaso alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo kwenye mtaa wake.

KAMANDA WA POLISI

Akizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Wilbroad Mutafungwa alisema watu kadhaa wanashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo na msako wa kuwakamata wahalifu hao unaendelea. “Ni kweli hilo tukio limetokea, lakini tayari tumekamata watu wawili na kazi inaendelea kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani,” alisema Kamanda Mutafungwa.

 

MATUKIO YA UTEKAJI

Matukio ya utekaji yameendelea kushamiri nchini ambapo juu ya tukio la Mo tayari Jeshi la Polisi linawashikilia takriban watu 20.

STORI: Dunstan Shekidele, MOROGORO

Comments are closed.