The House of Favourite Newspapers

Wakazi wa Polisi Mabatini Dar walia na ujenzi mbovu wa mifereji, wamuita Makonda

Ujenzi wa mifereji katika barabara inayotokea Shule ya Mapambano kuelekea Shule ya Sinza Maalum inavyoonekana kuwa juu.
Eneo la Shule ya Sinza Maalum inavyoonekana mifereji yake kuwa juu.
Taswira ilivyoonekana eneo hilo baada ya mvua kupungua.
Maji ya mvua yakiwa katika makazi ya watu.

 

 

WAKAZI wa eneo la Kituo cha Polisi cha Mabatini kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam, wamelalamikia ujenzi mbovu wa mifereji inayopitisha maji barabarani na kusababisha adhaa kubwa katika makazi yao.

 

 

Adha hiyo inatokana na ujenzi wa mifereji katika barabara inayotokea Shule ya Mapambano kuelekea Shule ya Sinza Maalum.

 

Hilo limejiri leo baada ya mvua kubwa kunyesha maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar ambapo katika eneo hilo, maji yametuwama na kuingia kwenye nyumba zilizopo karibu na barabara hiyo kutokana na kushindwa kupita kwenye mifereji iliyojengwa.

 

Wakazi wa eneo hilo wameutaka uongozi wa ngazi za juu kuingilia kati suala hilo na kulitatua haraka iwezekanavyo ili kuzuia maafa makubwa ambayo yanaweza kutokea hapo baadaye.

 

“Awali hakukuwepo na adha hii, kipindi cha mvua kama hiki, maji yalikuwa yakipita kwenye mifereji vizuri tu, lakini baada ya kujengwa hii mifereji mipya kabla ya barabara kumalizika ndiyo shida ilipoanzia.

 

“Tunauomba uongozi wa ngazi za juu hata akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aweze kupita eneo hili na ajionee adha ambayo tunaipata, maji yameelekezwa kwenye nyumba zetu badala ya kupita kwenye mifereji.

 

“Tunataka kabla ya barabara hii haijakabidhiwa kwa wahusika, mkandarasi aweze kulirekebisha jambo hili, vinginevyo tutaishi kwa shida kipindi cha mvua na faida ya barabara hii hatutaiona,” alisema mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Abdul.

Comments are closed.